Ushindi waipa Mamelodi zawadi ya bingwa wa CAF

Muktasari:
- RS Berkane ya Morocco ndio mabingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kuifunga Simba kwa ushindi wa jumla wa mabao 3-1 na kubeba kitita hicho ambacho ni Dola 2 milioni za Kimarekani ambazo ndizo zinazotolewa kwa timu inayoshinda mechi yoyote ya hatua ya makundi ya Kombe la Dunia la Klabu 2025.
USHINDI wa bao 1-0 ilioupata Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini dhidi ya Ulsan HD ya Korea Kusini katika michuano ya Kombe la Dunia la Klabu 2025 inayofanyika Marekani, imeipa klabu hiyo Sh Bilioni 5.2 ambayo ni sawa na zawadi waliyovuna mabingwa Kombe la Shirikisho Afrika.
RS Berkane ya Morocco ndio mabingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kuifunga Simba kwa ushindi wa jumla wa mabao 3-1 na kubeba kitita hicho ambacho ni Dola 2 milioni za Kimarekani ambazo ndizo zinazotolewa kwa timu inayoshinda mechi yoyote ya hatua ya makundi ya Kombe la Dunia la Klabu 2025.
Mamelodi imekuwa klabu ya kwanza ya Afrika msimu huu kupata ushindi katika michuano hiyo inayofanyika Marekani kwa kuifunga timu ya Korea Kusini na kujihakikishia kitita hicho ikiwa Kundi F na kuifanya iongoze msimamo mbele ya Borussia Dortmund ya Ujerumani iliyotoka sare ya 1-1 na Fluminense ya Brazili.
Bao lililowapa mabingwa hao wa African Football League (AFL) ushindi wa pesa nyingi, liliwekwa kimiani na mshambuliaji Iqraam Rayners aliyemaliza kazi nzuri ya Lucas Ribeiro katika dakika ya 36 na kuipa Mamelodi pointi tatu za kwanza katika kundi hilo.
Mshambuliaji huyo, pia aliweka wavuni mabao mawili katika dakika ya 29 na 39 lakini yalikataliwa kwa V.A.R, la kwanza likionekana alitumia mkono na jingine akiwa ameotea.
Awali, Al Ahly ya Misri, moja ya timu nne kutoka Afrika ilianza michuano hiyo kwa kutoka suluhu na Inter Miami ya Marekani iliyo na nyota wawili maarufu kutoka nchi za Argentina na Uruguay, Lionel Messi na Luis Suarez na kujihakikisha kitita cha dola 1 milioni ambazo ni sawa na Sh2.6 bilioni.
Esperance ya Tunisia yenyewe ilinza michuano hiyo vibaya kwa kufumuliwa mabao 2-0 na Flamengo RJ ya Brazili na leo Jumatano kuanzia saa 1:00 usiku, wawakilishi wengine wa Afrika, Wydad Casablanca ya Morocco yenye nyota waliowahi kutamba Ligi Kuu Bara, Mtanzania Seleman Mwalimu 'Gomez' na Stephane Aziz KI wa Burkina Faso itashuka uwanjani kuivaa Manchester City ya England.
Gomez aliyekuwa Mfungaji Bora wa Ligi Kuu Zanzibar, msimu uliopita akiwa na KVZ alisajiliwa na Wydad kutoka Singida Black Stars akiwa anaitumikia kwa mkopo Fountain Gate, wakati Aziz KI alitua kwa wababe hao wa Morocco akitokea Yanga.
Michuano hiyo ya Kombe la Dunia kwa Klabu inashirikisha klabu 32 katika mfumo mpya unaotumika kwa mara ya kwanza mwaka huu na bingwa wake atajinyakulia Dola 40 milioni (zaidi ya Sh105 bilioni).
Zawadi zilivyo:
Ushindi makundi: Dola 2M
Sare makundi: Dola 1M
Hatua ya 16 Bora: Dola 7.5M
Robo Fainali: Dola 13.125M
Nusu Fainali: Dola 21M
Mshindi wa Pili: Dola 30M
Bingwa: Dola 40M