Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ushindi wa kihistoria wampa Carrick matumaini Old Trafford

Muktasari:

  • Wakati huo, mashabiki wa Roma walikuwa wakishangilia huku Manchester United ikiwa nyuma kwa mabao 2-0, hali iliyotafsiriwa kama pigo kubwa kwa klabu hiyo na huenda ungekuwa mwisho wa safari ya Carrick kama kocha mkuu.

LONDON, England: MICHAEL Carrick anaweza asiweze kutambua kwa sasa umuhimu wa Bryan Cristante kuingia ndani ya eneo la hatari la AS Roma wakati Bruno Fernandes akipiga penalti yake ya kwanza kwenye Uwanja wa Old Trafford.

Wakati huo, mashabiki wa Roma walikuwa wakishangilia huku Manchester United ikiwa nyuma kwa mabao 2-0, hali iliyotafsiriwa kama pigo kubwa kwa klabu hiyo na huenda ungekuwa mwisho wa safari ya Carrick kama kocha mkuu.

Hata hivyo, mwamuzi wa video (VAR), Carlos del Cerro Grande, aliingilia kati na kushauri penalti irudiwe baada ya Cristante kuingia eneo la hatari kabla ya muda kuruhusiwa.

Fernandes hakupoteza utulivu, akapiga penalti ya pili na kufunga, kabla ya Matheus Cunha kufunga mabao mawili ndani ya dakika saba za mwisho katika mazingira ya presha kubwa.

Hata bila kuangalia yaliyotangulia kabla ya mchezo huo, ulikuwa miongoni mwa miujiza mikubwa ya matokeo katika historia ya soka.

Hata kutolewa kwa Cunha kwa kadi nyekundu muda mfupi baadaye hakukuzuia United kupata ushindi wake wa kwanza baada ya mechi 10, matokeo yaliyoipa nafuu baada ya wiki kadhaa za misukosuko.

Swali kubwa ni Carrick alijisikiaje wakati penalti ya kwanza ya Fernandes ilipopanguliwa? Na alizungumza nini wakati wa mapumziko baada ya kiwango kibovu cha kipindi cha kwanza kilichowafanya mastaa wa zamani wa United, Wayne Rooney na Nicky Butt, waliokuwa wachambuzi wa mchezo huo kupitia Amazon Prime, kutoa lawama kali?

Kwa wakati fulani, hali hiyo ilikumbusha yaliyowahi kutokea wakati wa aliyekuwa kocha wa United, Ole Gunnar Solskjaer.

Septemba 2023, Solskjaer alikumbuka namna alivyohisi wakati wa mapumziko katika mchezo dhidi ya Watford, miaka kadhaa kabla ya kuondolewa kwake kwenye nafasi ya ukocha.

“Wakati wa mapumziko dhidi ya Watford nilijua mambo yalikuwa yamefikia mwisho. Niliwaambia wachezaji kuwa huenda hiyo ilikuwa mara ya mwisho kufanya kazi pamoja,” alisema.

Siku hiyo, United ilikuwa nyuma kwa mabao 2-0 dhidi ya Watford katika Uwanja wa Vicarage Road. Carrick alikuwa benchi akiwa mmoja wa makocha wasaidizi wa Solskjaer. Mwisho wa mchezo, United ilipoteza kwa mabao 4-1.

SAFARI HII ILIKUWA TOFAUTI.

Licha ya hali ngumu iliyokuwa mbele yake, Carrick alionekana kuwa na mtazamo chanya zaidi.

“Wakati wa mapumziko nilitaka wachezaji wawe na mtazamo chanya zaidi, badala ya kukata tamaa na kukasirika kupita kiasi.

“Jambo rahisi unapojaribu kufanya kitu na mambo yakienda vibaya ni kujionea huruma. Unakatishwa tamaa na hali hiyo, lakini haitamsaidia yeyote. Kama tungekuwa hivyo, basi ingekuwa bora wote turudi nyumbani.

“Tunapaswa kuendelea kutafuta nafasi inayofuata na suluhisho jingine.

“Siwezi kuendelea kuwaambia vijana kuhusu ukubwa wa uwanja huu, historia yake na mambo yaliyowahi kutokea hapa, lakini yote hayo yapo.

“Uwanja huu una uwezo wa kufanya mambo ya ajabu. Umewahi kufanya hivyo na utaendelea kufanya hivyo tena siku zijazo. Kuna kitu cha kipekee hapa, hasa katika usiku kama huu ambao mara nyingi mambo huwa magumu kabla ya kugeuka.

“Lakini tukio moja linaweza kubadilisha kabisa mwelekeo wa kila kitu. Nilizungumza na wachezaji kuhusu hilo. Niliwaambia tunahitaji tukio moja litakaloweza kuamsha mabadiliko. Na tulilipata,” alisema Carrick.

Rooney, ambaye wakati wa kipindi cha kwanza alikuwa karibu kuwasihi wachezaji wa United waonyeshe “shauku na dhamira ya kupambana” baada ya kile alichokielezea kama kiwango kisicho na kitu, alibadili mtazamo wake baada ya mchezo na kumsifu Carrick.

“Nadhani Michael Carrick anastahili pongezi nyingi, kwa sababu ukiwa katika nafasi yake unajiuliza utawezaje kubadilisha hali hiyo?

“Chochote alichowaambia wachezaji wakati wa mapumziko kiliwafanya waanze kushambulia zaidi na kuwajengea imani kuwa wanaweza kushinda mchezo,” alisema Rooney.

Carrick hakukata tamaa hata baada ya Fernandes kukosa penalti yake ya kwanza.

“Sikucheka wala kutabasamu, sikuwa na furaha kuhusu kilichotokea. Lakini kwa namna fulani nilihisi bado kulikuwa na tukio jingine linaloweza kutokea.

“Wakati huohuo nilikuwa mtulivu kwa sababu nilikuwa na hisia kuwa wachezaji walitoka vyumbani wakiwa na mtazamo kwamba kuna jambo linaweza kutokea.

“Lazima nimpongeze Bruno kwa kuweza kupiga penalti hiyo mara ya pili, kuwa na ujasiri na kufunga. Anastahili pongezi nyingi,” alisema.

Pamoja na ushindi huo wa kishujaa, bado kuna maswali mengi kuhusu mustakabali wa United.

Kabla ya mchezo na hata wakati wa kipindi cha kwanza, mashabiki walifanya maandamano ya kupinga umiliki wa klabu hiyo, huku baadhi wakitumia rangi za kijani na dhahabu kuonyesha msimamo wao.

Nyimbo na kauli za kuipinga familia ya Glazer, mmiliki mwenza Sir Jim Ratcliffe na mkurugenzi wa soka Jason Wilcox hazitakoma kwa sababu tu United imepata ushindi huo, bila kujali namna ulivyopatikana.


Tathmini ya kina inapaswa pia kukumbuka kuwa United iliwahi kutoka nyuma na kuifunga Atalanta kwa mabao 3-2 katika Uwanja wa Old Trafford wakati wa utawala wa Solskjaer. Hata hivyo, siku nne baadaye ilifungwa mabao 5-0 nyumbani na Liverpool. Ndani ya mwezi mmoja, Solskjaer alikuwa amefutwa kazi.

Oktoba 2018, Jose Mourinho naye alikuwa katika hatari ya kufutwa kazi kabla ya mchezo wa Ligi Kuu England dhidi ya Newcastle. United iliruhusu mabao mawili ndani ya dakika 10 za mwanzo, lakini iligeuza matokeo na kushinda. Mourinho aliendelea kubaki kazini kwa mechi nyingine 13 pekee.

Hakuna anayejua kwa uhakika ushindi huo dhidi ya Roma umemwongezea Carrick muda kiasi gani katika nafasi yake.

“Sina uwezo wa kutabiri yajayo ili kujua nini kitatokea. Tunaendelea na maandalizi ya mchezo wa mwishoni mwa wiki. Tuna mechi muhimu sana dhidi ya Aston Villa hapa nyumbani ambayo tunapaswa kuiandaa vizuri,” alisema Carrick kupitia Amazon Prime.

Mtendaji mkuu wa United, Omar Berrada, na Wilcox walionekana kuwa na furaha zaidi baada ya filimbi ya mwisho kuliko walivyokuwa katikati ya kipindi cha kwanza.

Ghafla, United imeonekana kuwa na nafasi nzuri ya kufuzu hatua inayofuata ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Kwa mara ya kwanza tangu Septemba, wachezaji wa Carrick wameanza tena kufurahia hisia za ushindi.

Hata hivyo, furaha hiyo haitakuwa na maana kubwa kama hawataendeleza kiwango hicho katika mchezo dhidi ya Aston Villa, ambayo wakati United ikipambana na Roma, ilikuwa ikichapwa vibaya mabao 3-0 na Barcelona.

Alipoulizwa kama ushindi huo utamfanya alale vizuri zaidi, Carrick alijibu kwa uwazi kuwa hilo halitabadilika.

“Kwa kweli hapana. Sidhani. Sijui kama hilo ni jambo sahihi au lisilo sahihi, la kawaida au lisilo la kawaida, lakini sikuhisi nafuu baada ya ushindi huo. Nilifurahi zaidi kwa ajili ya wachezaji.

“Najua wanavyojali na kiasi cha juhudi wanazoweka. Wakati mwingine mambo yanaonekana hivyo, wakati mwingine hayaonekani. Kuna nyakati tunacheza vizuri na nyingine tunashindwa kufanya hivyo, na ninaelewa hali hiyo.

“Lakini niliweza kuona utayari wao wa kufanya vizuri. Walilazimika kupambana kwa nguvu zote na kuona kila mmoja akifurahia hisia za ushindi ambazo sote tunazitamani. Ndiyo maana tupo hapa,” alisema Carrick.

Kwa upande wa wachambuzi, licha ya wote kukerwa na kiwango cha United katika kipindi cha kwanza, wengi walipongeza mabadiliko makubwa yaliyoonekana kipindi cha pili.

Aliyekuwa kipa wa Denmark, Kasper Schmeichel, alisema:

“Nilisema wakati wa mapumziko kwamba kama mtafungwa, basi mpambane hadi mwisho. Unaweza kukubali kushindwa ikiwa umejitolea kwa kila kitu. Hawakufanya hivyo katika kipindi cha kwanza, lakini walifanya hivyo katika kipindi cha pili.

“Mambo yanaonekana kuwa mazuri kidogo. Hata hivyo, nisieleweke vibaya, kiwango cha kipindi cha pili kimeficha mapungufu yaliyoonekana katika kipindi cha kwanza. Sasa wanapaswa kutumia kiwango hicho kama kipimo na kuendelea kufanya mazungumzo zaidi ya kutatua matatizo yao.

“Lazima waweke tofauti zao pembeni kwa sababu kwa sasa hawawezi kubadilisha wachezaji walionao. Wanahitaji kila mmoja awe upande mmoja na wote wawe na mtazamo na lengo moja.”

Kuwa na mtazamo mmoja kumekuwa changamoto kwa Carrick na wachezaji wake. Lisandro Martinez na Bruno Fernandes wamekuwa wakitoa ukosoaji hadharani katika wiki za hivi karibuni, wakigusa masuala mbalimbali kuanzia uongozi wa klabu hadi mbinu za kocha.

Hata hivyo, aliyekuwa beki wa England, Stephen Warnock, anaamini ushindi dhidi ya Roma umeweka mazingira mazuri kabisa kwa Carrick.

“Manchester United iliingia uwanjani ikiwa timu iliyo katika mazingira magumu na isiyojiamini, kisha ikajikuta nyuma kwa mabao 2-0. Swali lilikuwa, ingeweza kuitikiaje hali hiyo?

“Sasa tumeona mwitikio wake na tunajua uwezo huo upo ndani ya timu. Wachezaji wanampigania kocha wao na wanapambana kubadilisha matokeo.

“Unapaswa kupambana na kuonyesha dhamira. Unapoonyesha juhudi na kuanza kusaidiana uwanjani, unaanza kuaminiana zaidi na kujenga imani kwamba unaweza kufanikisha jambo.

“Mashabiki wa Old Trafford waliongeza hamasa katika kipindi cha pili mara tu bao la kwanza lilipofungwa, na kuwasaidia wachezaji kuamini kuwa wangeweza kupata matokeo mazuri.

“Kwa Carrick, ulikuwa usiku mzuri kabisa,” alisema Warnock.