Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ushindi Stamford Bridge wabadili mwelekeo wa Tottenham

Muktasari:

  • Kwa uhalisia, ilikuwa ni pointi tatu. Kile ambacho ilipata kutokana na ushindi wake dhidi ya Chelsea ni ongezeko muhimu la pointi katika msimamo wa ligi.

MAMBO ni moto! Ligi Kuu England (EPL), inaendelea leo, lakini pamoja na mechi zingine saba, ile ya nane kati ya Tottenham Hotspur dhidi ya Crystal Palace inayoanza saa 2:30 usiku ina utamu wake. Spurs ilionyesha kiwango bora zaidi chini ya kocha Robert De Zerbi na kupata ushindi wa kihistoria wa mabao 2-0 ugenini dhidi ya Chelsea wiki iliyopita.

Kwa uhalisia, ilikuwa ni pointi tatu. Kile ambacho ilipata kutokana na ushindi wake dhidi ya Chelsea ni ongezeko muhimu la pointi katika msimamo wa ligi.

Hata hivyo, hilo halizuii hisia kwamba ushindi huo ulikuwa na umuhimu mkubwa zaidi ya hapo. Katika mechi 34 za ugenini dhidi ya Chelsea kabla ya mchezo huo, Spurs ilikuwa imeshinda mara moja tu. Pia ulikuwa ushindi wake wa kwanza bila kuruhusu bao katika Uwanja wa Stamford Bridge kwenye mashindano yoyote tangu Desemba 1986, karibu miaka 40 iliyopita.

Kushinda ugenini dhidi ya Chelsea ni jambo kubwa. Mashabiki wengi wa Spurs wamewahi kushuhudia timu yao ikifanya hivyo mara moja tu hapo kabla, Aprili 2018, chini ya kocha Mauricio Pochettino wakati ilikuwa timu yenye nguvu kubwa.

Tottenham iliingia katika mchezo huo ikiwa kwenye eneo la kushuka daraja, ikiwa na ushindi mmoja tu msimu huu, dhidi ya Coventry City iliyopanda daraja. Hali hiyo ilikuja baada ya kumaliza misimu miwili mfululizo katika nafasi ya 17, huku baadhi ya wachezaji muhimu wa kikosi chake bora wakiwa hawapo. Ni wachache waliotarajia matokeo hayo, hivyo ina haki ya kufurahia ushindi huo.

Hata hivyo, sababu halisi iliyoufanya ushindi huo uonekane kuwa na uzito mkubwa zaidi, mbali na kuipandisha Spurs hadi nafasi ya 12 kwenye msimamo wa ligi kabla ya kushuka hadi nafasi ya 14 kutokana na matokeo ya siku iliyofuata ni matumaini kwamba matokeo hayo na kiwango bora kilichoambatana nayo vinaweza kuwa mwanzo wa mabadiliko ya kupoteza mwelekeo katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.


PESA, NAMBA ZIKOJE?

Kwa kutumia kiasi kikubwa cha fedha katika dirisha la usajili la majira ya kiangazi, Spurs iliunga mkono mawazo ya kocha Roberto De Zerbi  kubadilisha muundo na sura ya kikosi. Matokeo ya mwanzoni mwa msimu yalionyesha kwamba, kama ilivyo kawaida, huenda timu hiyo ingehitaji muda kuzoeana. Spurs ilisubiri hadi dakika ya 86 ya mchezo wake wa tano, ikiwa tayari imefungwa mabao 3-0 na Aston Villa, ndipo ilipopata bao lake la kwanza la ligi msimu. Hata hivyo, tangu mapumziko ya mechi za kimataifa yaliyofuata kipigo hicho imeonyesha maendeleo makubwa. Ilitoa sare ya bao 1-1 dhidi ya Man United ugenini ingawa ilistahili kushinda kabla ya ushindi wake wa kwanza wa msimu dhidi ya Coventry.

Tottenham ilihitaji pointi hizo kuliko kitu kingine chochote. Hata hivyo, mabao yake yote matatu yalifungwa kwa mashuti kutoka nje ya eneo la hatari, huku ikizalisha nafasi za mabao zilizotarajiwa 0.86. Huenda ilistahili ushindi huo, lakini haikuwa na kiwango cha kuridhisha sana.

Ingawa ilipokutana na mazingira magumu zaidi na yenye presha kubwa ugenini dhidi ya Chelsea, Spurs ilifanya kile kilichohitajika wakati muhimu zaidi. Timu hiyo ilidhibiti mpira kwa ufanisi na kumaliza mchezo ikiwa na asilimia 68.9 ya umiliki wa mpira. Ingawa haikutengeneza nafasi nyingi za wazi za kufunga, ilipata ushindi kupitia bao la kujifunga lisilo la kawaida la Mike Penders na bao zuri binafsi la Mathys Tel, ambalo huenda ikawa vigumu kulirudia, baada ya mchezaji huyo kukokota mpira umbali wa mita 45.

Spurs iliingia katika maeneo hatari mara kwa mara kiasi cha kutengeneza nafasi za kutosha kushinda mchezo. Takwimu zake za mabao yanayotarajiwa za 0.74 hazikuonyesha namna ilivyotawala mchezo. Haikuwa bahati kwamba huu ulikuwa mchezo wa kwanza ambao kiungo Mateus Fernandes, aliyesajiliwa kwa Pauni 85 milioni alianza akicheza katika nafasi ya kiungo mkabaji.

Fernandes ndiye aina ya viungo wanaoweza kuhimili presha ya wapinzani na ambaye De Zerbi anamhitaji ili kutekeleza falsafa yake ya soka. Hata hivyo, kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo majeraha, kutokuwa katika utimamu kamili wa kucheza na kuzaliwa kwa mtoto wake wa kwanza hivi karibuni, alikuwa bado hajaanza mchezo wowote katika nafasi nyingine isipokuwa kiungo mshambuliaji. Alikuwa pia amepata dakika za kucheza katika maeneo ya pembeni.

Na katika mchezo huo kila kitu kilipitia kwake, na alithibitisha bila kuacha shaka kwamba anafanya vizuri zaidi anapocheza katika nafasi ya kiungo wa ndani aliye nyuma zaidi. Alikuwa katika nafasi anayoipendelea akicheza pamoja na kiungo Sandro Tonali, ambaye pia alisajiliwa kwa gharama kubwa katika dirisha la majira ya kiangazi. Hivyo, wawili hao waliunda kwa mara ya kwanza safu mpya ya kiungo ya Spurs.

Fernandes alikuwa bora sana. Aligusa mpira mara nyingi zaidi kuliko mchezaji mwingine yeyote wa timu yoyote aliyocheza ugenini katika mechi ya Ligi Kuu England msimu huu, mara 124. Pia aliongoza kwa idadi ya ukabaji wa mpira akiwa na mitano, na alikamilisha asilimia 92.2 ya pasi zake 102. Mara kwa mara alikuwa akijinasua yeye mwenyewe na kuisaidia Spurs kutoka katika mazingira magumu.

Aligusa mpira mara 89 akiwa chini ya presha ya mpinzani, idadi iliyokuwa ya tano kwa wingi kwa mchezaji yeyote katika mchezo mmoja wa ligi hiyo msimu huu. Vilevile aligusa mpira mara 48 akiwa chini ya presha kubwa, hali ambayo inamaanisha mpinzani alikuwa ndani ya umbali wa mita mbili kutoka kwake, katika eneo lake la nusu ya uwanja. Hiyo ilikuwa idadi kubwa zaidi iliyorekodiwa na mchezaji yeyote katika ligi hiyo.

Jambo la kuvutia zaidi ni kwamba alikamilisha asilimia 91.2 ya pasi zake alipokuwa chini ya presha ya mpinzani.

Pasi zake nyingi ziliisaidia timu yake kuendelea kumiliki mpira, lakini pia alisogeza mchezo mbele kwa ufanisi. Alipiga pasi 27 zilizovunja mistari ya wapinzani, idadi iliyokuwa ya 12 kwa wingi kwa mchezaji yeyote katika mchezo mmoja wa Ligi Kuu England msimu huu. Jambo muhimu zaidi ni kwamba pasi 21 kati ya hizo zilipigwa akiwa chini ya presha ya wapinzani. Hakuna mchezaji mwingine katika ligi hiyo aliyefikia au kuzidi idadi hiyo msimu huu. Na Fernandes alifanya hivyo akiwa ugenini dhidi ya Chelsea.

Inaonekana kwamba ikiwa Spurs ilihitaji kitu cha kuifungulia njia ili iweze kutekeleza matakwa ya De Zerbi, basi Fernandes anaweza kuwa mchezaji muhimu katika kufanikisha hilo. Aliiwezesha Spurs kuishawishi Chelsea kupeleka wachezaji wake wengi kwenye presha ya kuzuia mashambulizi, kisha kuipenya kwa pasi na kuendeleza mashambulizi. Alifanya hivyo kwa kupeleka mpira kutoka safu ya ulinzi hadi safu ya ushambuliaji kwa uthabiti, jambo ambalo Tottenham ilikuwa haijalifanya kwa muda mrefu.

Kazi iliyofanyika walipofika katika theluthi ya mwisho ya uwanja ilionyesha ni kiasi gani bado wanapaswa kufanya. Spurs iliingia katika theluthi ya mwisho ya uwanja mara 58 lakini ikazalisha mabao yanayotarajiwa 0.74 pekee, uwiano ambao ni miongoni mwa mibaya zaidi kurekodiwa na timu yoyote katika mchezo wa Ligi Kuu England msimu huu. Hata hivyo, namna ilivyofika mara kwa mara katika maeneo ya kushambulia ikiwa na idadi kubwa ya wachezaji kuliko wapinzani ni ishara nzuri ya kile ambacho timu hiyo inaweza kufanikisha.

Hakuna mchezaji katika kikosi hicho aliyefunga zaidi ya bao moja la ligi msimu huu. Kwa hiyo, wanahitaji angalau mmoja kati ya Dominic Solanke, Omar Marmoush, Savio, Mohammed Kudus au Tel kuanza kufunga mabao mara kwa mara. Hata hivyo, hakuna shaka kwamba mambo yanaanza kwenda vizuri.


MAMBO MAGUMU, MEPESI?

Mabadiliko yanatokea wakati muafaka kwa Spurs, ambayo inakabiliwa na mfululizo wa mechi zinazoweza kuipa nafasi nzuri ya kupata matokeo.

Kwa kutumia wastani wa alama za Opta za wapinzani watano watakaokutana nao katika mechi zijazo, Spurs ina ratiba rahisi zaidi kuliko timu nyingine yoyote katika ligi hiyi. Itakutana na Crystal Palace (nyumbani), Leeds (ugenini), Ipswich (nyumbani), Sunderland (ugenini) na Fulham (nyumbani).

Kati ya timu hizo, tatu ziko chini ya Spurs kwenye msimamo wa ligi, moja mbele yake kwa pointi moja, huku nyingine ikiwa mbele kwa pointi mbili. Kwa kuzingatia kiwango ilichoonyesha dhidi ya Chelsea, siyo kupitiliza matumaini kusema kwamba Spurs inapaswa kuamini inaweza kushinda mechi zote tano. Hata hivyo, baada ya kushinda  mbili zilizopita, kushinda mechi nyingine tano mfululizo kutaifanya iwe na ushindi saba mfululizo. Ni Aston Villa pekee iliyofanikiwa kufanya hivyo katika msimu mzima uliopita.

Ukweli ni kwamba kuna uwezekano mdogo wa Spurs kushinda mechi nyingi kiasi hicho mfululizo. Lakini kushinda mechi tatu kati ya tano zinazofuata? Hilo linawezekana, na litaiweka timu hiyo katika nafasi nzuri. Spurs bado iko pointi tatu tu juu ya eneo la kushuka daraja, hivyo haijatoka kabisa katika hatari hiyo. Hata hivyo, kwa ghafla, sasa iko pointi mbili tu nyuma ya timu zilizo katika nafasi sita za juu.

Kuna sababu za kutosha kwa timu hiyo kuanza kuangalia uwezekano wa kupanda kwenye msimamo wa ligi badala ya kuendelea kuwa na wasiwasi wa kushuka daraja. Hata hivyo, kuna umuhimu mkubwa pia wa kupata matokeo mazuri katika mfululizo wa mechi tano zijazo. Ratiba nzuri inayowakabili sasa inafuatwa na mfululizo mgumu zaidi wa mechi. Wapinzani watano watakaofuata baada ya hapo ni Arsenal, Liverpool, Brighton na Bournemouth. Kuanzia Desemba 4, baada ya kumaliza mfululizo wa mechi wenye ratiba rahisi zaidi, Spurs itakabiliwa na ratiba ngumu zaidi kuliko timu nyingine zote za Ligi Kuu England.

Na baada ya mfululizo huo wa mechi, itasafiri kwenda Uwanja wa Etihad kukutana na Manchester City. Mfululizo huo utakuwa mtihani mkubwa sana, na huenda Spurs ikahitaji kuwa na akiba ya kutosha ya pointi ili kukabiliana nao. Hii ni kwa sababu, hata baada ya kufanya jambo lisilotarajiwa kwa kushinda dhidi ya Chelsea, inaweza kupata ugumu mkubwa wa kuvuna pointi dhidi ya wapinzani hao.

Baada ya kuonyesha kiwango kizuri Stamford Bridge, sasa ni wakati wa Spurs kuanza kufikiria kile inachoweza kufanikisha msimu huu badala ya kuwa na wasiwasi kuhusu iwapo itaepuka vita vingine vya kuwania kubaki kwenye ligi. Hata hivyo, ni muhimu kukumbuka kwamba ilikuwa ni ushindi mmoja tu, na mambo yanaweza kubadilika haraka na kuharibika. Lakini Tottenham angalau imeonyesha kwamba ina msingi mzuri wa kujenga, na kikosi hiki kina uwezo wa kutekeleza kile ambacho De Zerbi anataka kifanye.