HAKUPOI…! Kuna matokeo ya kushangaza Ulaya
LONDON, ENGLAND: WAKUBWA Real Madrid, Arsenal, Napoli, Borussia Dortmund, Manchester City na Liverpool ni miongoni mwa timu 18 zinazoshuka viwanjani leo, Jumatano, kukipiga katika mechi tisa za Ligi ya Mabingwa Ulaya ikiwa ni za raundi ya nne ya hatua ya ligi baada ya zingine tisa kuchezwa jana.
Ufuatao ni utabiri wa kila mechi kwa mujibu wa Opta.
FENERBAHCE VS LIVERPOOL
Katika mechi za leo, Fenerbahce na Liverpool ambazo hazijawahi kukutana katika mashindano yoyote, zitakuwa na matumaini ya kuboresha rekodi ya matokeo, ambapo Liverpool itakuwa mzigoni nchini Uturuki.
Liverpool inaweza kuwa ilishatwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya 2005 katika fainali ya kukumbukwa jijini Istanbul, lakini haijawahi kushinda mchezo wowote kati ya sita ya ugenini dhidi ya timu za Uturuki katika Kombe la Ulaya au Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Imepoteza michezo mitano na kutoka sare moja, ikiwemo mechi nne za mwisho mfululizo. Hata hivyo, itakutana na mpinzani ambaye naye anapitia wakati mgumu katika kutafuta ushindi.
Baada ya kutoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Slavia Prague katika mchezo wa tatu, Fenerbahce sasa imeweka rekodi mbaya zaidi ya kutoshinda katika historia ya ushiriki wake kwenye Kombe la Ulaya au Ligi ya Mabingwa Ulaya, ikiwa na michezo 10 bila ushindi (sare 4, vipigo 6).
Na licha ya Liverpool kupata kipigo nyumbani cha bao 1-0 dhidi ya Arsenal Jumapili iliyopita katika Ligi Kuu England, kikosi hicho kinapewa nafasi kubwa ya kuvunja rekodi yake mbaya nchini Uturuki, kikipewa asilimia 57.8, huku Fenerbahce ikiwa na 20.4.
AEK ATHENS VS REAL MADRID
Katika mchezo mwingine, wakati hali ya furaha na matumaini ikitawala Real Madrid tangu ilipoifunga Barcelona, wapinzani wake wakubwa katika El Clasico, zaidi ya wiki moja iliyopita, watakuwa mzigoni leo. Kikosi hicho cha Jose Mourinho kimeonyesha ari mpya, jambo ambalo linaweza kuwa habari mbaya kwa AEK Athens katika mchezo huo.
Real Madrid imefunga mabao manne katika mechi mbili zilizopita za Ligi ya Mabingwa Ulaya (ushindi wa 4-3 dhidi ya Roma na 4-1 dhidi ya RB Leipzig). Mara ya mwisho kufunga mabao manne au zaidi katika mechi tatu mfululizo za Ligi ya Mabingwa Ulaya ilikuwa kati ya Aprili na Septemba 2014, ilipofanya hivyo katika michezo mitatu. Mwisho wa msimu huo, ilitwaa ubingwa wa mashindano hayo.
Hata hivyo, AEK Athens imepoteza mchezo mmoja pekee kati ya sita ya nyumbani katika mashindano makubwa ya Ulaya tangu kuanza kwa msimu uliopita, ikishinda minne na kutoka sare mmoja.
Pia, ilishinda mchezo wake mwingine pekee wa nyumbani katika Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu, ikiifunga LASK mabao 1-0 katika mchezo wa kwanza. Timu hiyo ya Ugiriki inapewa nafasi ya asilimia 12.7 kuisumbua Real Madrid, huku mabingwa wa Ulaya mara 15, Madrid, ikipewa nafasi ya kushinda kwa asilimia 70.8.
LEIPZIG VS MAN CITY
Ngoma nyingine itakunisha RB Leipzig na Manchester City ambazo zimekuwa na mazoea ya kukutana katika Ligi ya Mabingwa Ulaya. Huo utakuwa mchezo wa saba kukutana, huku katika sita iliyopita zikifungana jumla ya mabao 30 (RB Leipzig mabao 9, Man City mabao 21).
Katika mechi za Kombe la Ulaya au Ligi ya Mabingwa Ulaya ambazo timu zimekutana mara tano au zaidi, ni michezo kati ya AC Milan na Rapid Vienna pekee yenye wastani mkubwa zaidi wa mabao kwa kila mchezo (5.8), ikiwa na mabao 29 katika mechi tano.
Leipzig italazimika kumwangalia kwa karibu Erling Haaland ambaye amefunga mabao 12 katika mechi nane alizocheza dhidi yao. Mabao yake sita dhidi ya Leipzig katika Ligi ya Mabingwa Ulaya ndiyo idadi kubwa zaidi aliyowahi kufunga dhidi ya mpinzani mmoja, sawa na mabao sita aliyofunga dhidi ya Sevilla. Hata hivyo, matano kati ya sita alifunga katika mchezo mmoja, wakati Man City iliposhinda 7-0, Machi 2023.
Kikosi hicho cha Man City kinapewa nafasi kubwa ya kushinda mchezo huo kwa asilimia 57.7 huku asilimia 20.8 zikiwa za Leipzig.
SLAVIA VS ARSENAL
Arsenal itakuwa ugenini tena baada ya kutoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Bayern Munich katika mchezo uliopita. Hata hivyo, kwa heshima zote, safari hii inaonekana kuwa mechi nyepesi kidogo ikilinganishwa na ile ya Munich, kwani itakutana na Slavia Prague katika mchezo wa nne.
Slavia Prague ya Jamhuri ya Czech ni miongoni mwa timu sita ambazo bado hazijapata ushindi katika hatua ya ligi msimu huu, ingawa ilipata sare nzuri ugenini dhidi ya Fenerbahce wiki mbili zilizopita.
Na takwimu zinaonyesha kwamba Slavia Prague haijashinda katika mechi 22 zilizopita za Ligi ya Mabingwa Ulaya (sare 8, vipigo 14), tangu ilipopata ushindi wake wa kwanza katika mashindano hayo 2007.
Kufungwa katika mchezo huu kutaiwezesha kufikia rekodi mbaya zaidi ya kutoshinda katika historia ya Kombe la Ulaya au Ligi ya Mabingwa Ulaya, ambayo kwa sasa ni michezo 23. Rekodi hiyo inashikiliwa kwa pamoja na AEK Athens (1989–2006) na FCSB (2006–2013).
Timu hizo pia zilikutana jijini Prague, Czech katika hatua ya ligi ya msimu uliopita, ambapo Arsenal ilishinda 3-0. Washika Bunduki wanapewa nafasi ya kushinda tena na kuondoka na pointi zote kwa asilimia 69.0, huku Slavia ikipewa 13.0.
PORTO VS NAPOLI
Mchezo mwingine unaoweza kuwa na ushindani mkubwa utachezwa nchini Ureno, ambapo Porto ya kocha Francesco Farioli itakuwa mwenyeji wa Napoli ya Massimiliano Allegri.
Porto itakuwa na matumaini ya kuepuka kipigo cha tatu mfululizo nyumbani katika mashindano hayo baada ya kupoteza mbili za nyumbani katika Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu. Ilifungwa mabao 2-0 na Manchester City na 1-0 na PSV.
Ni mara moja pekee kabla ya hapo ambapo Porto imepoteza mechi tatu mfululizo za nyumbani katika mashindano makubwa ya Ulaya na hiyo ilitokea katika michezo mitatu ya kwanza ya kihistoria katika mashindano hayo, kati ya 1956 na 1962.
Porto ndiyo inayopewa nafasi kubwa ya kushinda mchezo huu, ikiwa na nafasi ya asilimia 43.0 ya kuifunga Napoli. Timu hiyo ya Italia ilipoteza kwa mabao 2-0 dhidi ya Juventus Jumapili katika Ligi Kuu Italia (Serie A), lakini inapewa nafasi ya kuibuka na pointi zote katika mchezo huu kwa asilimia 31.6.
DORTMUND VS REAL BETIS
Huko ujerumani utachezwa mchezo mwingine wa ligi hiyo ambako Borussia Dortmund itakuwa mwe nyeji wa moja ya timu zilizoshangaza wengi msimu huu, Real Betis, ambapo timu hiyo ya Ligi Kuu Hispania (La Liga) ni miongoni mwa tano ambazo bado zina rekodi ya ushindi wa asilimia 100, ikiwa imeshinda mechi tatu za Ligi ya Mabingwa Ulaya ilizocheza, na itakuwa ikitafuta ushindi wa nne mfululizo uwanjani Signal Iduna Park.
Huo utakuwa mchezo wa kwanza kabisa kwa timu hizo kukutana, huku Betis ikipewa nafasi ya chini ya moja kati ya nne ya kuendeleza rekodi yake nzuri ya ushindi, ikiwa ni asilimia 23.7.
Baada ya kutoka sare katika mchezo mgumu wa Klassiker dhidi ya Bayern Munich mwishoni mwa wiki, Dortmund inapewa nafasi kubwa ya kuibuka na ushindi katika mchezo huo kwa asilimia 53.7.
PSV VS CLUB BRUGGE
Huu nao utakuwa mchezo mwingine wa kwanza kabisa kukutanisha timu mbili ambao utafanyika Eindhoven, ambako PSV itakuwa mwenyeji wa Club Brugge. Wababe wa Uholanzi, PSV, wamepoteza kila mmoja wa michezo yao minne iliyopita dhidi ya timu za Ubelgiji katika historia ya Kombe la Ulaya au Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Mchezo wa mwisho kati ya hiyo ulipigwa msimu uliopita dhidi ya Union Saint-Gilloise, ambapo PSV ilifungwa mabao 3-1 nyumbani Septemba 2025.
Brugge inaingia katika mchezo huu ikiwa na morali ya ushindi mkubwa dhidi ya Inter Milan katika Uwanja wa San Siro, Italia. Brugge inapewa nafasi ya kupata ushindi mwingine kwa asilimia 32.2, huku PSV ndiyo inayoonekana kuwa wababe nyumbani, ikiwa na asilimia 44.4.
LENS VS COMO
Como itakuwa Ufaransa ambako inakaribishwa na Lens, na katika mchezo huo wa inapewa asilimia 43.1, ambayo itakuwa ni matumaini ya kuendeleza ushindi wake mkubwa dhidi ya Manchester United katika mchezo uliopita huku Lens ikipewa asilimia 32.6.
VIKING VS SABAH
Viking ya jijini Stavanger nchini Norway inapewa asilimia 60.9 ikiikaribisha Sabah ya Azerbaijan inayopewa asilimia 19.3 za ushindi katika mchezo unaokutanisha timu vibonde katika hatua hii ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.