Ushindi 100, mabao 335, huu ndiyo ubabe wa Flick Barcelona
Muktasari:
- Ushindi huo wa Flick unadhihirisha ukubwa wa mchango wake katika klabu hiyo, akiongoza timu hiyo kushinda kwa asilimia 76.34, kiwango ambacho hakijawahi kufikiwa na kocha mwingine yeyote wa klabu hiyo.
BARCELONA, HISPANIA: KOCHA Hansi Flick amefikisha rekodi ya ushindi 100, baada ya kuiongoza Barcelona kuichapa Aston Villa kwa mabao 3-0 katika Ligi ya Mabingwa.
Ushindi huo wa Flick unadhihirisha ukubwa wa mchango wake katika klabu hiyo, akiongoza timu hiyo kushinda kwa asilimia 76.34, kiwango ambacho hakijawahi kufikiwa na kocha mwingine yeyote wa klabu hiyo.
Kocha huyo Mjerumani amekuwa wa pili kufikisha ushindi huo kwa idadi ndogo ya mechi, akitanguliwa na Luis Enrique pekee.
Hata hivyo, mbali na asilimia kubwa ya ushindi, takwimu zinaonyesha namna Barcelona ilivyokuwa na nguvu ya kutisha chini ya Flick, huku rekodi tano kutoka katika ushindi wake 100 zikieleza ubabe wa timu hiyo.
Katika ushindi 43 kati ya 100, Barcelona imefunga mabao manne au zaidi, huku mara 24 ikifunga angalau mabao matano.
Hiyo ina maana kuwa karibu ushindi mmoja kati ya minne imeambatana na Barcelona kufunga mabao matano au zaidi, hali inayoonyesha ubora wa mfumo wa soka la kushambulia wa Flick na uwezo wa wachezaji alionao.
Katika ushindi huo 100, Barcelona imefunga mabao 335, wastani wa mabao 3.35 kwa kila ushindi.
USHINDI WA MABAO MENGI
Barcelona ya Flick haijazoea ushindi wa tabu, kwani ni mechi 28 tu kati ya ushindi wake 100 ambazo imeshinda kwa tofauti ya bao moja, huku 72 zikiwa za tofauti ya mabao mawili au zaidi.
Cha kushangaza zaidi, katika ushindi wa mechi 12 iliyopata msimu huu, hakuna hata mmoja uliohitaji tofauti ya bao moja.
Pamoja na hilo, ushindi wa bila kuruhusu bao haujawa jambo la kawaida katika mechi za Barcelona, kwani imeshinda kwa mabao 1-0 au 0-1 mara 10 tu, sawa na asilimia 10 ya ushindi wake wote.
MATOKEO YANAYOJIRUDIA
Matokeo ya ushindi yaliyojitokeza mara nyingi chini ya Flick ni 3-0 nyumbani na 2-0 ugenini, kila moja likitokea mara saba.
Kwa upande mwingine, ushindi wa 1-0, 2-0 na 3-0, ukiwemo ule wa ugenini wa 0-1, 0-2 na 0-3, kila mmoja umetokea mara 10.
Real Valladolid ni miongoni mwa timu zilizopata kipigo kikubwa zaidi kutoka kwa Barcelona ya Flick.
Katika msimu wa 2024-25, Barcelona iliifunga timu hiyo mabao saba, huku Raphinha akipiga hat-trick yake ya kwanza chini ya kocha huyo.
Huo pia ulikuwa ushindi pekee wa Barcelona wa mabao saba ambao wapinzani wake hawakufunga bao lolote.