Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Morgan Rogers atakavyoibeba Chelsea

ROGERS Pict

Muktasari:

  • Usajili huo unaelezwa sio wa kuongeza jina kubwa pekee kwenye kikosi hicho, bali ni sehemu ya mpango mpya wa kocha Xabi Alonso wa kuijenga Chelsea inayoweza kurejea kupigania ubingwa wa Ligi Kuu England baada ya misimu tisa kuyumba.

LONDON, ENGLAND: CHELSEA imetikisa tena soko la usajili baada ya kukamilisha uhamisho wa mshambuliaji wa Aston Villa, Morgan Rogers kwa ada ya pauni milioni 117, dili ambalo limewashangaza wengi kutokana na ukweli kwamba Arsenal ndiyo iliyokuwa ikipewa nafasi kubwa ya kumpata nyota huyo wa England.

Usajili huo unaelezwa sio wa kuongeza jina kubwa pekee kwenye kikosi hicho, bali ni sehemu ya mpango mpya wa kocha Xabi Alonso wa kuijenga Chelsea inayoweza kurejea kupigania ubingwa wa Ligi Kuu England baada ya misimu tisa kuyumba.

Rogers amesaini mkataba wa miaka sita wenye chaguo la kuongeza mwaka mmoja zaidi baada ya kufanyiwa vipimo vya afya jijini London mara tu aliporejea kutoka Marekani alipokuwa akiitumikia England katika Kombe la Dunia la 2026.

ROGE 01

WAPI ILIANZIA

Tofauti na wengi walivyodhani kuwa dili hilo lilitokea ghafla, ukweli ni kwamba Chelsea imekuwa ikimfuatilia Rogers kwa zaidi ya miaka miwili.

Vyanzo vya ndani ya klabu vinaeleza kuwa viongozi wa Chelsea walisubiri kwa makusudi hadi England ilipomaliza safari yake ya Kombe la Dunia ili kuepusha usumbufu kwa mchezaji huyo wakati wa mashindano.

Baada ya England kutolewa nusu fainali na Argentina, Chelsea ilianza mazungumzo ya mwisho yaliyohusisha wakurugenzi wa michezo, kocha Xabi Alonso na mmiliki mwenza Behdad Eghbali huku nahodha Reece James pamoja na Cole Palmer wakitajwa kuwa miongoni mwa waliomshawishi Rogers kuhamia Stamford Bridge. Ndani ya saa zisizozidi 48, makubaliano yalikuwa yamekamilika.

ROGE 06

ARSENAL ILIVYOZIDIWA KETE

Ingawa Arsenal ilipewa nafasi ya kulingana na ofa ya Chelsea, viongozi wake walikataa kuongeza thamani waliyoamini kuwa ndiyo sahihi.

Hatua hiyo ilifungua mlango kwa Chelsea kukamilisha moja ya usajili mkubwa zaidi katika historia ya klabu hiyo.

Kwa sasa Arsenal inalazimika kuelekeza nguvu zake kwa malengo mengine yakiwemo Bradley Barcola wa Paris Saint-Germain pamoja na Junior Kroupi wa Bournemouth.


DILI LILIVYOPIKWA

Moja ya sababu zilizorahisisha mazungumzo ni uhusiano mzuri uliopo kati ya mmiliki mwenza wa Chelsea, Behdad Eghbali na mmiliki wa Aston Villa, Nassef Sawiris.

Mahusiano hayo yalisaidia pande zote kufikia makubaliano haraka licha ya ukubwa wa fedha zilizohusika.

Villa pia ilikuwa chini ya presha ya kanuni za kifedha za UEFA, jambo lililoifanya iwe tayari kusikiliza ofa kubwa kwa mmoja wa wachezaji wake muhimu.

ROGE 03

SILAHA KWA ALONSO

Kwa mtazamo wa kiufundi, Rogers anaonekana kuwa mmoja wa wachezaji muhimu ambavyo Xabi Alonso anahitaji ili kutekeleza falsafa yake ya soka.

Kocha huyo Mhispania anapendelea timu inayobadilika haraka kutoka nyuma kwenda mbele huku viungo washambuliaji wakipewa uhuru mkubwa wa kutengeneza nafasi.

Rogers anafaa kwenye mfumo huo kutokana na uwezo wake wa kucheza kama kiungo mshambuliaji, winga wa kushoto au mshambuliaji wa pili.


NAFASI YA PALMER

Swali kubwa ambalo limeibuka ni kama ujio wa Rogers utaathiri nafasi ya Cole Palmer.

Kwa wengi wanaowaona kama wachezaji wenye majukumu yanayofanana, ukweli ni kwamba Alonso anaamini wanaweza kucheza pamoja.

Mpango unaotajwa ni Palmer kucheza katikati kama namba 10 huku Rogers akitokea upande wa kushoto, hali itakayoruhusu wote kutumia ubunifu wao bila kuingiliana.

Endapo Chelsea itatumia mfumo wa mabeki watatu ambao Alonso aliufanikisha Bayer Leverkusen, basi Palmer na Rogers wanaweza kucheza pamoja nyuma ya mshambuliaji mmoja kama viungo washambuliaji wawili.

ROGE 02

URAFIKI NA PALMER

Mbali na masuala ya kiufundi, Rogers anakwenda Chelsea akiwa tayari ana mazingira rafiki.

Yeye na Cole Palmer ni marafiki wa karibu tangu walipokuwa katika akademi ya Manchester City.

Aidha, anawafahamu vizuri Reece James, Levi Colwill, Romeo Lavia, Tosin Adarabioyo, Jamie Gittens pamoja na Liam Delap, jambo litakalorahisisha kuzoea maisha mapya Stamford Bridge.

ROGE 05

ATAONGEZA MABAO

Msimu uliopita Chelsea ilikumbwa na tatizo kubwa la kushindwa kufunga mabao katika vipindi muhimu.

Kulikuwa na mechi tano mfululizo ambazo timu ilishindwa kabisa kufunga, hali iliyochangia kuondolewa kwa aliyekuwa kocha Liam Rosenior.

Rogers anakuja akiwa na rekodi ya mabao 14 pamoja na pasi 12 za mabao katika mechi 55 alizoichezea Aston Villa msimu uliopita.

Takwimu hizo zinaonyesha uwezo wake wa kutengeneza nafasi na pia kufunga hivyo anaweza kuongeza makali katika safu ya ushambuliaji ya timu hiyo.

Pamoja na ujio wa Rogers, Chelsea sasa ina idadi kubwa ya wachezaji kwenye safu yake ya ushambuliaji.Mbali na Palmer na Rogers, kikosi hicho kina Estevao Willian, Pedro Neto, Geovany Quenda na Jamie Gittens katika nafasi za pembeni.

Kwa upande wa washambuliaji wa kati, Joao Pedro, Nicolas Jackson, Liam Delap, Emmanuel Emegha pamoja na Marc Guiu wote wanagombea nafasi moja au mbili.Hali hiyo ina maana kuwa baadhi ya nyota hao watalazimika kuondoka kwa mkopo au kuuzwa kabla ya dirisha kufungwa.

ROGE 04

MKWANJA KWA CHELSEA

Licha ya ada ya pauni milioni 117 kwa Rogers, Chelsea bado imeendelea kufanya usajili mwingine akiwemo beki Marco Palestra kutoka Atalanta huku ikihusishwa na Pep Chavarria, Maxence Lacroix pamoja na Valentin Barco.

Swali ambalo wengi wanauliza ni namna klabu hiyo inavyoweza kumudu matumizi hayo makubwa. Jibu lake ni kwamba Chelsea imewekeza sana katika kuuza wachezaji.

Msimu uliopita ilikusanya karibu pauni milioni 300 kutokana na mauzo ya wachezaji ili kukidhi kanuni za kifedha za Ligi Kuu England na UEFA.

Ingawa hali ya kifedha ya Chelsea imeimarika, UEFA bado inaifuatilia kwa karibu kutokana na ukiukaji wa kanuni za matumizi uliowahi kutokea.

Hata hivyo, adhabu ya mwaka huu imepungua kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na mwaka uliopita, ishara kwamba klabu inaanza kurekebisha hesabu zake.

Ndiyo maana viongozi wake wanaendelea kusisitiza kuwa wachezaji wasiokuwa sehemu ya mipango ya Alonso lazima wauzwe ili kuendelea kulinda afya ya kifedha ya klabu.


CHELSEA MPYA

Usajili wa Morgan Rogers unaonyesha wazi kuwa Chelsea imebadili mkakati wake wa usajili.

Badala ya kutegemea vipaji vya baadaye pekee, sasa inalenga pia wachezaji ambao tayari wamethibitisha uwezo wao katika Ligi Kuu England na kwenye kiwango cha kimataifa.

Kwa Xabi Alonso, Rogers si usajili wa kuongeza ukubwa wa kikosini tu, bali ni mchezaji anayetarajiwa kuwa sehemu ya mhimili wa mashambulizi ya Chelsea kwa miaka mingi ijayo.

Iwapo ataendeleza kiwango alichoonyesha Aston Villa na England, anaweza kuwa mmoja wa nyota watakaobadili kabisa sura ya Chelsea katika enzi mpya za Alonso, huku mashabiki wa Stamford Bridge wakiamini kuwa dili hilo linaweza kuwa hatua muhimu ya kuirudisha klabu hiyo kwenye hadhi yake.