Umeiona Real Madrid ya jose Mourinho?
Muktasari:
- Tayari ameshacheza mechi tatu za Ligi Kuu Hispania (LaLiga), akishinda zote akianza na Espanyol ugenini alikoondoka na ushindi wa mabao 2-1, kisha nyumbani akaizaba Real Sociedad 4-1 na juzi akiichapa Malaga 4-0.
MADRID, HISPANIA: REAL Madrid inachezaje chini ya Mourinho? Mfumo, kikosi cha kwanza na mambo yalivyo! Kimsingi, majaribio yamekwisha na sasa ni wakati wa “mambo mazuri uwanjani,” kama Jose Mourinho mwenyewe anavyosema, ambapo kocha huyo mpya wa Real Madrid alipata mechi sita za kuwajaribu wachezaji wake kabla ya mchezo wa kwanza wa LaLiga dhidi ya Espanyol.
Tayari ameshacheza mechi tatu za Ligi Kuu Hispania (LaLiga), akishinda zote akianza na Espanyol ugenini alikoondoka na ushindi wa mabao 2-1, kisha nyumbani akaizaba Real Sociedad 4-1 na juzi akiichapa Malaga 4-0.
Itakumbukwa kwamba wakati wa mechi za maandalizi ya msimu (pre-season), Madrid ya Mourinho ilimaliza bila kufungwa ikishinda mechi tano na kutoka sare moja, huku ikionyesha dalili kwamba inaanza kuzoeana taratibu. Lakini, kiuhalisia uchezaji wa mastaa wa kikosi hivho ni uleule.
Kumekuwa na dalili za kutia moyo na ushahidi wa moja kwa moja kwamba haina jipya isipokuwa labda maingizo mapya ya wachezaji yanaweza kuleta vitu vipya kikosini, lakini kwa Mourinho bado hajafichua kila kitu alichonacho.
Kwa ujumla, jambo moja linaonekana kuwa wazi; mfumo wa uchezaji. Mourinho ameukumbatia mfumo wa 4-2-3-1, ambao, mbali na yale ambayo tayari yameonekana unaonekana kuwa wa kizamani zaidi.
VIUNGO WAWILI WA ULINZI, MABEKI WANNE
Katika safu ya kiungo, bado kuna swali kuhusu jozi ambayo Mourinho ataipendelea katika mfumo wa viungo wawili wa chini. Mapambano ya nafasi mbili za kuanza yanaonekana kuwa kati ya Aurelien Tchouameni, Federico Valverde na Bernardo Silva, huku Eduardo Camavinga akiwa chaguo jingine. Hali ya Mfaransa huyo ni ya aina yake, kwani Camavinga ndiye mchezaji wa nne aliyepata dakika nyingi zaidi chini ya Mourinho, ingawa mazingira yamekuwa yakimsaidia.
Kukosa Kombe la Dunia kulimaanisha kwamba alikuwa tayari kuanza maandalizi ya msimu kuanzia siku ya kwanza, tofauti na wachezaji wengine watatu. Na kiwango chake, badala ya kumaliza mjadala uliokuwepo kuhusu msimu uliopita, kimeufanya mjadala huo uendelee.
Katika safu ya ulinzi, upande wa kushoto, Marc Cucurella, ambaye ametoka kutwaa ubingwa wa dunia inatarajiwa kwamba ataifanya nafasi hiyo kuwa yake kwani ameonyesha hivyo katika mechi zote alizocheza akipanda juu mara nyingi zaidi kupeleka mashambulizi ingawa Mourinho inaonekana kwamba amemzuia kutopendelea kubaki eneo la juu ili kurudi haraka nyuma kwa ajili ya ulinzi.
Uwapo wake pamoja na jeraha la Ferland Mendy kumempa nafasi Alvaro Carreras kuwa mchezaji mwingine anayeweza kupata namba eneo la mabeki, lakini uzoefu unaweza kumtoa na kuwaacha wakongwe wakitamba kama ilivyo sasa, hasa eneo la katikati ambapo Antionio Rudiger, Ibrahim Konate na Dean Huijsen wanapishana. Upande wa kulia, Mourinho amekuwa akiwabadilishana Trent Alexander-Arnold na Denzel Dumfries, ambapo wawili hao wamecheza pamoja.
Katikati ya ulinzi, majeraha yamemfanya Eder Militao akose maandalizi yote ya msimu na hata mechi za ligi. Mbrazili huyo anatarajiwa kurejea baada ya mapumziko ya kwanza ya mechi za kimataifa. Raul Asencio naye amecheza tu katika michezo ya mazoezi.
WASHAMBULIAJI WANNE
Hakuna maswali kuhusu nafasi ya kipa, ambapo Thibaut Courtois ndiye chaguo lisilo na mjadala. Pia kuna mjadala mdogo kuhusu washambuliaji wanne; Yan Diomande, Jude Bellingham, Vinicius Jr na Kylian Mbappe. Hata hivyo, wachezaji wanaowazunguka wameonyesha viwango vizuri.
Arda Guler ameonekana kuwa huru na mwenye kujiamini katika namba 10 ambayo imepangwa kwa ajili ya Bellingham na juzi alishaonyesha ubora katika ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Malaga alipofunga mojawapo.
Gulee, mchezaji wa timu ya taifa ya Uturuki ameanza mechi mbili na ametoa asisti mbili, huku mfumo wa Mourinho ukimpa nafasi ya wazi ya kucheza kama kiungo mshambuliaji wa kati, ambapo anaweza kutumia vizuri dakika ambazo Bellingham hatakuwepo uwanjani. Brahim Diaz pia anaonekana kuwa na nafasi ya kupata jukumu lililo wazi zaidi katika winga ya kulia na juzi alifanya vizuri zaidi.
Kwa wachezaji hao wawili, hilo litakuwa badiliko kutoka misimu iliyopita, ambapo walikuwa wakihamishwa kutoka nafasi moja kwenda nyingine wakati Madrid ikijaribu kuwatosheleza katika mfumo wa 4-3-3. Kwa Mourinho kuna maswali na majibu kadri maisha yanavyoendelea uwanjani.
Kwa ujumla, wachezaji wote wa Real Madrid wanaonekana kucheza mpira wao, huku mbinu za kocha zikiwa hazijaanza kuonekana wazi. Kila eneo unapowaangalia unagundua kwamba ulivyokuwa msimu uliopita ndivyo maisha yanavyosonga kikosini.