Curry, Mavericks NBA kuna picha linasukwa?
Muktasari:
- Kwa mujibu wa kanuni za uhamisho wa wachezaji katika ligi hiyo timu inapomtaka mchezaji inatuma maombi moja kwa moja kwa shirikisho la timu miliki hutaarifiwa na ikiwezekana kuamriwa kufanya biashara.
DALLAS, MAREKANI: LIGI ya Kikapu Marekani (NBA), ina maajabu yake na imeshayaonyesha kwa miaka mingi sasa. Lakini, lililowashangaza mashabiki wengi wa mchezo huo miezi ya karibuni ni uhamisho (trades) uliofanyika ambapo mastaa ambao hawakutarajiwa waliamua kusepa katika timu zao na kutimkia kwingine, miongoni mwao bila kutarajia.
Kwa mujibu wa kanuni za uhamisho wa wachezaji katika ligi hiyo timu inapomtaka mchezaji inatuma maombi moja kwa moja kwa shirikisho la timu miliki hutaarifiwa na ikiwezekana kuamriwa kufanya biashara. Ni kwa msingi huo, wapo mastaa ambao hulazimika kuhama timu bila kupenda, lakini hawana jinsi.
Na ndivyo ilivyokuwa kwa Giannis Antetokounmpo aliyelazimika kuachana na Milwaukee Bucks iliyomchagua katika drafti kwa mara ya kwanza na ambayo aliitumikia kwa miaka 13 mfululizo, na ‘kulazimishwa’ kutimkia Miami Heat katika dirisha la usajili mwaka huu, ambako atakipiga kuanzia msimu ujao.
Ingawa hadithi yake ni tofauti na LeBron James ambaye aliachana na Los Angeles Lakes majuzi na kutimkia Philadelphia 76ers, Giannis hakutaka kuhamia timu nyingine kwa sasa. Mara nyingi uhamisho wa NBA huanza kama tetesi na ni kama ilivyo katika soka kabla ya shirikisho kuziuliza timu iwapo zipo tayari kufanya biashara.
Na sasa kuna tetesi nyingi zimeanza kuvuma juu ya pendekezo la kushangaza la usajili linaloweza kuwakutanishja pamoja Stephen Curry, Kyrie Irving na Cooper Flagg katika kikosi cha Dallas Mavericks, ingawa kuna mambo flani yanayoweza kuwa vikwazo.
Curry ametumia maisha yake yote ya miaka 17 katika NBA akiwa na Golden State Warriors, ambako amekuwa sura ya klabu hiyo na mmoja wa wachezaji bora zaidi katika historia ya ligi hiyo.
Hata hivyo, pendekezo la hivi karibuni la kubadilishana wachezaji, ambalo ni la kinadharia limeibua uwezekano kwamba Curry anaweza kuamua nafasi yake bora ya kushinda ubingwa mwingine iko nje ya Golden State.
Mavericks wametajwa kama moja ya maeneo yanayoweza kumpokea katika mpango wa kubadilishana wachezaji unaohusisha timu nne, ambao utampeleka Curry Dallas ambako ataungana na Irving na Flagg.
Kwa sasa hakuna dalili kama Mavericks na Warriors wanafanya mazungumzo kuhusu biashara hiyo, wala Curry hajaomba kuondoka. Hata hivyo, tetesi hizo hazipaswi kupuuzwa hasa kwa sababu Golden State imekiri kwamba ingemsikiliza Curry endapo siku moja ataamua kutaka mabadiliko.
Curry hana kifungu cha mkataba kinachompa haki ya kuzuia kuhamishwa, lakini Meneja Mkuu wa Golden State, Mike Dunleavy Jr hivi karibuni alisema Warriors waheshimu matakwa ya mchezaji iwapo nyota huyo ataomba kuuzwa au kuhamishwa kwenda timu nyingine.
Dunleavy pia alisisitiza kwamba Curry anataka kumalizia maisha yake ya kikapu akiwa Golden State, na mara kwa mara ameeleza nia yake ya kustaafu akiwa na klabu hiyo. Kwa hiyo, ingawa kikanuni anaweza kuhamishwa bila kuwa na haki ya kisheria ya kuzuia uhamisho huo, ni vigumu kufikiria Golden State ikamhamisha kinyume na matakwa yake. Na kwa sasa hakuna ushahidi kwamba Curry anataka kuondoka.
Hata hivyo, muda ambao uvumi huu umeibuka unavutia. Curry amebakiza msimu mmoja kwenye mkataba wake wa sasa wenye thamani ya takribani Dola 62.6milioni, na atakuwa na sifa ya kusaini mkataba wa kuongeza muda wa miaka miwili wenye thamani ya karibu Dola 136.7 milioni kuanzia Agosti 29. Hilo linaifanya miezi ijayo kuwa muhimu sana katika kuamua mustakabali wake wa muda mrefu.
Golden State ilimaliza msimu uliopita ikiwa na ushindi 37 na kufungwa mara 45, hivyo kukosa nafasi ya kucheza hatua ya mtoano, huku Curry akicheza mechi 41 pekee kutokana na majeraha.
Pia walishindwa kuwasajili baadhi ya nyota bora waliokuwa wakiwafuatilia katika kipindi cha usajili. Hilo limechochea mjadala kuhusu iwapo Golden State inapaswa kufikiria kufanya mabadiliko makubwa siku zijazo. Lakini hilo halimaanishi kwamba Curry yupo sokoni.
DALLAS INAWEZA KUMFAA CURRY?
Hapa ndipo panapovutia zaidi. Mavericks wanajenga timu inayomzunguka Flagg, aliyechaguliwa namba moja katika Drafti ya NBA 2026, huku pia wakimjumuisha Irving katika mipango yao ya baadaye.
Dallas imeweka wazi kwamba inataka kujenga timu inayomzunguka Flagg na kumuwekea mazingira mazuri nyota huyo. Irving pia haonekani kuchukuliwa kama mchezaji wa kuuzwa.
Taarifa zimeeleza kwamba Mavericks inalenga kumbakiza na kuona kile anachoweza kufanya akiwa pamoja na Flagg. Kumleta Curry kutabadilisha kabisa hali hiyo.
Badala ya kutegemea Flagg kuibeba timu mara moja, Dallas itakuwa imemzungukwa na wachezaji wawili wenye uwezo mkubwa wa kutengeneza nafasi na kufunga. Fikiria uwezekano wa kuwa na Curry, Irving na Flagg kwenye kikosi kimoja.
Curry ataleta uwezo wa kutengeneza nafasi kwa mitupo ya mbali ambayo ni miongoni mwa bora zaidi katika historia ya NBA. Irving ataipa Mavericks mfungaji mwingine mwenye uwezo mkubwa wa kuc heza mmoja dhidi ya mmoja na kupora mipira, huku Flagg akileta ubora wa kimwili, uwezo wa kucheza nafasi mbalimbali na uwezekano mkubwa wa kuwa nyota bora katika pande zote mbili za mchezo.
Swali kubwa litakuwa kuhusu ulinzi na upatikanaji wa wachezaji kutokana na majeraha. Curry atakuwa na umri wa miaka 39 katika msimu wa 2026-27, huku Irving akitoka kwenye jeraha kubwa la goti lililomfanya akose sehemu kubwa ya msimu uliopita. Kwa hiyo, Mavericks itakuwa inaweka matumaini makubwa kwa nyota mwenye umri mkubwa, mlinzi anayerejea kutoka kwenye jeraha na kipaji cha kijana mdogo. Lakini kama wote watakuwa na afya bora kikosi cha Curry, Irving na Flagg kitaifanya Mavericks kuwa moja ya timu zinazovutia zaidi kuangaliwa NBA.
Kwa upande wa Curry, Mavericks inaweza kumpa kitu ambacho Golden State haiwezi kumhakikishia kwa sasa ikiwa ni timu iliyo tayari yenye uwezo wa kupigania ubingwa na iliyojengwa kuzunguka wachezaji kadhaa wenye uwezo mkubwa wa kushambulia.
Pia kuna sababu za wazi kwa nini Golden State itataka malipo makubwa kwa Curry. Hata akiwa na umri wa miaka 38, bado ni mchezaji bora katika upande wa ushambuliaji na ni miongoni mwa nyota wenye thamani kubwa zaidi kibiashara katika NBA.
Golden State pia watapaswa kuzingatia athari za kimichezo na kiutamaduni za kumuuza mchezaji anayehusishwa kwa karibu zaidi na kipindi bora zaidi katika historia ya klabu hiyo.
Kwa Mavericks italazimika kuhakikisha hesabu za mishahara zinaendana na kanuni za NBA kuhusu ukomo wa mishahara, jambo ambalo ni kikwazo kingine kikubwa. Mshahara wa Curry kwa msimu wa 2026-27 ni takribani Dola 62.6 milioni.
Dallas tayari ina sehemu kubwa ya bajeti iliyotengwa kwa wachezaji kama Irving, Washington, Klay Thompson, Daniel Gafford na Flagg.
Taarifa za sasa za mishahara zinaonyesha Irving anapokea takribani Dola 39.5 milioni, Washington Dola 19.8 milioni, Thompson Dola 17.5 milioni, Gafford Dola 17.3 milioni na Flagg Dola 14.5 milioni. Hii ina maana kwamba Dallas haiwezi kuamua tu kwamba inamtaka Curry na kisha kufanya uhamisho huo.