Ukurasa mpya ndugu zake Ronaldo Kombe la Dunia U-20
Muktasari:
- Timu hiyo imefuzu baada ya kupata nafasi miongoni mwa timu tano za Ulaya zilizopata tiketi kupitia michuano ya UEFA ya Wanawake U-19 ya mwaka 2025. Ureno ni miongoni mwa timu 24 zinazoshiriki mashindano hayo makubwa duniani na imepangwa Kundi E pamoja na Korea Kaskazini, Costa Rica na Colombia, jana Jumatatu ilianza kampenzi yake dhidi ya Korea Kaskazini.
JINA la Cristian Ronaldo limeifanya Ureno kutambulika duniani katika soka la wanaume, lakini sasa upande wa wanawake wa nchi hiyo imeanza safari ya kuandika historia yake yenyewe, baada ya kufuzu kwa mara ya kwanza kushiriki Kombe la Dunia la Wanawake U-20, michuano inayofanyika Poland.
Timu hiyo imefuzu baada ya kupata nafasi miongoni mwa timu tano za Ulaya zilizopata tiketi kupitia michuano ya UEFA ya Wanawake U-19 ya mwaka 2025. Ureno ni miongoni mwa timu 24 zinazoshiriki mashindano hayo makubwa duniani na imepangwa Kundi E pamoja na Korea Kaskazini, Costa Rica na Colombia, jana Jumatatu ilianza kampenzi yake dhidi ya Korea Kaskazini.
Nahodha wa Ureno, Mafalda Mariano, amesema anajivunia kuiongoza timu katika tukio hilo la kihistoria, akisisitiza kuwa wachezaji wote wamefika Poland wakiwa tayari kutoa kila kitu.
“Ni heshima kubwa kuwa sehemu ya mashindano haya Poland. Tuko tayari na kila mmoja anatamani kucheza. Tumekuja kutoa kila kitu tulichonacho kama nahodha, ni muhimu kuhakikisha kila mmoja anatulia na kubaki makini,” amesema Mariano.
Kiungo wa timu hiyo, Carolina Santiago amesema kushiriki Kombe la Dunia ni jambo kubwa kwao na wanataka kutumia nafasi hiyo vizuri kwa kuipigania nchi yao. Santiago tayari ameshacheza katika timu ya taifa ya wakubwa ya Ureno na hata kufunga bao lake la kwanza la kimataifa katika kampeni za kufuzu Kombe la Dunia la Wanawake 2027.
Aliongeza kuwa bao hilo lilimfanya aanze kuota ndoto kubwa zaidi, ikiwemo kupata nafasi ya kuiwakilisha Ureno katika Kombe la Dunia la wakubwa. Kwa upande wake, Mafalda Mariano ametambua ugumu wa mchezo wao wa kwanza dhidi ya Korea Kaskazini akiamini pamoja na ushindani utakaonekana ndani ya dakika 90 bado wana nafasi ya kufanya vizuri.