Romaine Gandonou awasha moto Kombe la Dunia U-20
Muktasari:
- Gandonou mwenye miaka 15, alionyesha kiwango bora licha ya kuwa miongoni mwa wachezaji wadogo zaidi kwenye mashindano hayo. Benin ilikuwa nyuma kwa mabao 2-0 kabla Gandonou hajasawazisha akifunga mabao mawili yaliyoipa pointi moja timu hiyo.
NYOTA wa Benin, Romaine Gandonou, ameanza vizuri kampeni za Kombe la Dunia la Wanawake U-20 baada ya kufunga mabao mawili na kuisaidia timu hiyo kupata sare ya 2-2 dhidi ya Mexico katika mchezo wa Kundi A.
Gandonou mwenye miaka 15, alionyesha kiwango bora licha ya kuwa miongoni mwa wachezaji wadogo zaidi kwenye mashindano hayo. Benin ilikuwa nyuma kwa mabao 2-0 kabla Gandonou hajasawazisha akifunga mabao mawili yaliyoipa pointi moja timu hiyo.
Kiungo huyo amesema: “Nimefurahi kufunga mabao mawili katika mchezo wangu wa kwanza. Tutaendelea kufanya kazi kwa bidii kujiandaa kwa mchezo wetu wa pili timu nzima itatoa kila kitu kuhakikisha tunashinda na kupata pointi tatu.”
Mchezaji huyo wa AS Tambours FC, amesema yuko katika hali nzuri ya kujiandaa na michezo inayofuata akiamini wanayo nafasi ya kuandika historia kwenye mechi mbili zilizobaki.
Gandonou mwenyewe aliweka wazi kwamba lengo lake ni kuwa mfungaji bora wa Kombe la Dunia U-20, akisema mabao mawili aliyofunga kwenye mchezo wa kwanza ni mwanzo tu na anataka kuendelea kufunga katika michezo inayofuata.
Kocha wa Benin, Ouzerou Abdoulaye, amemsifu Gandonou akisema ni kipaji cha kipekee kinachohitaji kuendelea kupewa nafasi na mpira ili aweze kutumia uwezo wake.
Abdoulaye amesema nguvu kubwa ya Gandonou ni kasi, uwezo wa kubeba mpira, kutumia miguu yote miwili, ustadi na uwezo wa kusoma mchezo, lakini alisisitiza kuwa bado ana mambo ya kuboresha, anaamini kwamba akipewa mazingira mazuri ya kuendelea kukua kwa miaka miwili au mitatu ijayo, anaweza kufikia kiwango kikubwa na hata kuwa miongoni mwa wanaowania tuzo ya Mchezaji Bora wa Afrika.
“Ni mchezaji mzuri lakini anapaswa kuboresha baadhi ya maeneo hasa kwenye wakati wa kufanya maamuzi, timu inamuhitaji kiungo mchezeshaji ambaye hatakuwa na mambo mengi,” amesema.
Mchezo wa pili wa kundi A utapigwa leo Jumanne ambapo Benin itakutana na Argentina kabla ya Septemba 11, 2026 kupambana na wenyeji Poland.