Colombia ina malengo ya ubingwa Kombe la Dunia U20
Muktasari:
- Ortegon mwenye umri wa miaka 20, ambaye anakipiga katika klabu ya Independiente Santa Fe, ameteuliwa kuwa nahodha wa Colombia katika michuano hiyo, nafasi inayokuja baada ya kuwa na uzoefu mkubwa katika mashindano ya kimataifa ya vijana.
KIUNGO wa Colombia, Juana Ortegon, amesema kikosi hicho kimejipanga kupambana hadi mwisho katika Kombe la Dunia la Wanawake la U-20 litakalofanyika Poland, huku akifichua kuwa ndoto yao kubwa ni kulitwaa taji hilo.
Ortegon mwenye umri wa miaka 20, ambaye anakipiga katika klabu ya Independiente Santa Fe, ameteuliwa kuwa nahodha wa Colombia katika michuano hiyo, nafasi inayokuja baada ya kuwa na uzoefu mkubwa katika mashindano ya kimataifa ya vijana.
Kiungo huyo tayari ameshiriki Kombe la Dunia la Wanawake la U-17 mwaka 2022, kabla ya kuendelea kuwa sehemu ya timu ya Colombia katika Kombe la Dunia la U-20 mwaka huo huo na mwaka 2024, lililofanyika nchini kwao.
Akizungumzia malengo yao nahodha huyo alisema “Malengo yetu ni kubeba taji kwa sababu tayari tumepata uozefu kwenye mashindano makubwa kilichobaki ni kulibeba na tunaamini msimu huu inawezekana.”
Ortegon alisema uzoefu alioupata tangu akiwa na miaka 15 umemsaidia kukua siyo tu kisoka, bali pia katika uongozi na namna ya kukabiliana na presha ya mashindano makubwa.
Alisema kuwa anapoitazama safari yake ya miaka iliyopita, anaona tofauti kubwa kati ya msichana aliyekuwa na miaka 15 na mchezaji ambaye sasa anaongoza kikosi cha taifa.
Ortegon pia ameeleza kuwa uzoefu wa Colombia katika Kombe la Dunia la U-20 mwaka 2024 umewapa somo kubwa, hasa baada ya kucheza mbele ya mashabiki wengi katika uwanja wa nyumbani.
Colombia ilifanya vizuri katika michuano hiyo, lakini ikaishia katika hatua ya robo fainali baada ya kuondolewa kwa mikwaju ya penati 3-0 kufuatia sare ya 2-2 dhidi ya Uholanzi.
Colombia imepangwa Kundi E pamoja na Costa Rica, Korea Kaskazini na Ureno.
“Ndoto ni kwenda mpaka mwisho. Hakuna heshima kubwa kwa timu ya taifa kama kuwa mabingwa wa dunia,” amesema Ortegon.
Colombia pia ina kizazi kinachotazamiwa kuendeleza mafanikio ya wachezaji kama Linda Caicedo, Mayra Ramirez na Leicy Santos, ambao tayari wamejijengea majina katika timu ya taifa ya wakubwa.