Uganda yajitoa AFCON U-23 kisa ukata wa fedha
Muktasari:
- Uganda ni miongoni mwa wenyeji wa AFCON 2027 pamoja na Kenya na Tanzania, hivyo maandalizi ya Uganda Cranes yamepewa kipaumbele katika bajeti ya serikali ya mwaka wa fedha 2026/2027.
Timu ya taifa ya Uganda ya vijana chini ya umri wa miaka 23 ‘Kobs’, imejitoa kwenye mashindano ya kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Vijana weny umri chini ya miaka 23 (AFCON U23) 2027.
Uamuzi huo umekuja baada ya Shirikisho la Soka Uganda (FUFA) kushindwa kupata fedha za kutosha kumudu gharama za mashindano hayo.
Uganda ilikuwa imepangwa kucheza dhidi ya Ethiopia katika raundi ya kwanza ya kufuzu.
Mchezo wa kwanza ulitarajiwa kuchezwa Ethiopia Septemba 28, huku mchezo wa marudiano ukipangwa kupigwa Uganda, Oktoba 6, mwaka huu.
Hata hivyo, FUFA imesema imeamua kuiondoa Uganda kwenye mashindano hayo kwa sababu hakukuwa na fedha za kutosha kuiwezesha timu kushiriki kikamilifu.
Kwa mujibu wa FUFA, Serikali ya Uganda imeweka kipaumbele kwenye maandalizi ya timu kubwa ya taifa, Uganda Cranes, kuelekea fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027.
Uganda ni miongoni mwa wenyeji wa AFCON 2027 pamoja na Kenya na Tanzania, hivyo maandalizi ya Uganda Cranes yamepewa kipaumbele katika bajeti ya serikali ya mwaka wa fedha 2026/2027.
Hali hiyo imeifanya serikali ishindwe kugharamia kikamilifu mahitaji ya timu nyingine za taifa, ikiwemo Uganda Kobs.
FUFA imeeleza kwamba uamuzi huo umefanywa sasa kwa sababu ilikuwa bora kujitoa mapema kuliko kusubiri hadi karibu na mashindano wakati timu ikiwa haina uhakika wa kupata fedha.
Hili si tukio la kwanza. Mwaka 2022, FUFA iliiondoa Uganda Kobs kwenye mchujo wa AFCON U23, wakati huo ikieleza ukosefu wa fedha kama sababu.
Kilichotokea sasa kinaibua mjadala mkubwa kuhusu ufadhili wa timu za taifa za Uganda, hasa namna ambavyo fedha zinavyogawanywa kati ya timu kubwa na timu za vijana.