Kiungo ahofia hatma yake Argentina
Muktasari:
- Paredes, mwenye umri wa miaka 32, alipewa adhabu hiyo kutokana na vurugu zilizotokea baada ya Argentina kufungwa 1-0 na Hispania katika fainali ya Kombe la Dunia 2026.
BUENOS AIRES, ARGENTINA: KIUNGO wa Argentina, Leandro Paredes amedokeza anaweza kuachana na timu ya taifa baada ya kufungiwa mechi 10 na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
Paredes, mwenye umri wa miaka 32, alipewa adhabu hiyo kutokana na vurugu zilizotokea baada ya Argentina kufungwa 1-0 na Hispania katika fainali ya Kombe la Dunia 2026.
Katika tukio hilo, Paredes alidaiwa kumshika beki wa Hispania, Eric Garcia shingoni na kumwangusha Gavi chini, kabla ya kuonekana kumpiga mchezaji huyo usoni.
Adhabu hiyo, pamoja na uamuzi wa Lionel Messi kustaafu soka la kimataifa, sasa inaweza kuwa na nafasi kubwa katika uamuzi wa Paredes kuhusu mustakabali wake akiwa na Argentina.
“Itakuwa vigumu kwangu kuendelea na timu ya taifa,” alisema Paredes, anayekipiga Boca Juniors.
“Kwa sababu ya adhabu hii, pia kwa sababu ya uamuzi wa Leo. Itakuwa vigumu mambo kuendelea kama yalivyokuwa awali.”
Paredes amesema bado hajazungumza na kocha Lionel Scaloni kuhusu suala hilo, lakini anatarajia kufanya hivyo kabla ya kufikia uamuzi wa mwisho.
“Bado sijazungumza na kocha kuhusu hilo, lakini tutazungumza na kuona uamuzi nitakaoufanya.”
MESSI AAGA TIMU YA TAIFA
Kauli ya Paredes imekuja muda mfupi baada ya Messi, mwenye umri wa miaka 39, kutangaza kustaafu soka la kimataifa.
Messi alisema amefikisha mwisho wa kile alichokuwa nacho kwa Argentina baada ya “kutoa kila kitu” kwa timu hiyo.
Nyota huyo aliiongoza Argentina kutwaa Kombe la Dunia nchini Qatar mwaka 2022, lakini hakufanikiwa kurudia mafanikio hayo katika mechi yake ya mwisho akiwa na taifa lake baada ya Argentina kushindwa na Hispania katika fainali.
Messi anaondoka akiwa mfungaji bora wa muda wote wa Argentina na mchezaji aliyevaa jezi ya taifa hilo mara nyingi zaidi, akiwa amefunga mabao 125 katika mechi 207.
URITHI WA MESSI UTAISHI MILELE
Paredes amemuelezea Messi kama mchezaji ambaye urithi wake utaendelea kuwepo kwa vizazi vijavyo kutokana na mafanikio yake akiwa Argentina.
“Urithi wa Leo utaishi milele kwa sababu ya yote aliyoyafanikisha, kwa kutokata tamaa na kwa kuonyesha kwamba ndoto zinahitaji kupiganiwa na hatimaye zinaweza kutimia,” alisema.
Paredes alifichua kuwa wachezaji wa Argentina walikuwa wamezungumza katika siku za mwisho za Kombe la Dunia kuhusu uwezekano wa fainali hiyo kuwa mechi ya mwisho ya Messi akiwa na timu ya taifa.
Hata hivyo, alisema bado hawakuwa tayari kihisia kukabiliana na tangazo hilo.
“Tulizungumza katika siku za mwisho za Kombe la Dunia kwamba fainali hiyo huenda ikawa mechi yake ya mwisho. Lakini hata hivyo, hatukuwa tumejiandaa kwa hilo kwa sababu ya maana ambayo Leo anayo kwetu.”
Sasa Paredes mwenyewe anakabiliwa na swali kuhusu mustakabali wake Argentina, huku adhabu ya mechi 10 na kuondoka kwa Messi vikifanya kizazi hicho cha timu ya taifa kuingia katika kipindi kipya kisicho na uhakika.