Uchaguzi Real Madrid waivuruga Man City
Muktasari:
- Mgombea Enrique Riquelme na mfanyabiashara mkubwa wa sekta ya nishati jadidifu anayempinga rais wa sasa wa Real Madrid, Florentino Perez alionekana kwenye televisheni Jumatano iliyopita akiwa ameshika jezi ya Real Madrid yenye jina la Haaland.
LONDON, ENGLAND: MANCHESTER City wanafikiria kuchukua hatua za kisheria baada ya mgombea wa urais wa Real Madrid kuahidi kumsajili mshambuliaji wao, Erling Haaland.
Mgombea Enrique Riquelme na mfanyabiashara mkubwa wa sekta ya nishati jadidifu anayempinga rais wa sasa wa Real Madrid, Florentino Perez alionekana kwenye televisheni Jumatano iliyopita akiwa ameshika jezi ya Real Madrid yenye jina la Haaland.
Akinukuliwa amesema: “Ana kipengele cha kuachiliwa kwenye mkataba wake na angependa kujiunga na Real Madrid. Nikichaguliwa kuwa rais, atacheza Real Madrid.”
Muda mfupi baadaye, baba wa Haaland na wakala wake walitoa taarifa ya pamoja kukanusha madai hayo, huku Manchester City nao wakiyapinga vikali.
Taarifa ya City ilisema: “Habari zilizoibuka nchini Hispania kuhusu mustakabali wa Erling Haaland si za kweli. Hakuna uwezekano wa jambo hili kutokea na hakuna kipengele chochote cha kimkataba kinachoruhusu hilo.
Tunazingatia kuchukua hatua za kisheria kutokana na matumizi ya picha na jina la mchezaji wetu katika muktadha huu.”
Enrique pia aliahidi kumsajili kiungo wa Manchester City, Rodri, akisema: “Ni mchezaji bora katika nafasi ambayo Madrid inahitaji kuimarisha.
"Tumezungumza na wakala wake. Tunapaswa kuheshimu klabu yake, lakini nikikuwa rais atacheza Madrid. Nitafanya kila linalowezekana.”
Baba wa Haaland, Alf-Inge Haaland, pamoja na wakala wake, Rafaela Pimenta, wamesema katika taarifa yao ya pamoja:
“Yote haya yanaburudisha, lakini si kweli. Tunawatakia kila la heri wagombea wote wawili katika uchaguzi wa Real Madrid.”
Kinachoendelea katika uchaguzi wa Real Madrid
Enrique Riquelme amempa changamoto rais wa sasa wa Real Madrid, Florentino Perez, katika uchaguzi wa urais wa klabu hiyo. Hii ni mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 20 kwa Perez kupata mpinzani rasmi badala ya kupita bila kupingwa.
Hatua hiyo imekuja baada ya misimu miwili ambayo Real Madrid haijashinda taji lolote kubwa.
Riquelme mwenye umri wa miaka 37 ameendesha kampeni yenye ahadi nyingi kubwa kwa wanachama wa klabu. Miongoni mwa ahadi zake ni kujenga “mji wa wanachama” karibu na eneo la mazoezi la klabu, utakaokuwa na mabwawa ya kuogelea, viwanja vya padel na ukumbi wa mpira wa kikapu.
Pia ameahidi kupunguza ada ya uanachama kwa hadi asilimia 50 iwapo timu haitashinda ubingwa wa Ligi ya Mabingwa msimu ujao.
Aidha, Riquelme amepinga uamuzi wa Perez wa kumteua Jose Mourinho kuwa kocha wa Real Madrid. Uteuzi huo unaweza kuthibitishwa rasmi tu ikiwa Perez atashinda uchaguzi huo.
Timu ya kampeni ya Riquelme imeashiria kuwa kocha wa zamani wa Liverpool FC, Jurgen Klopp, ndiye chaguo lao kuu kwa nafasi ya ukocha.
“Kocha wangu ni yule ambaye mashabiki wa Real Madrid wanamtaka,” amesema Jumatano bila kutaja jina.
Alipoulizwa kuhusu Klopp katika mahojiano na The Athletic mwezi uliopita, Riquelme amesema: “Kwa kawaida, ningependa makocha wenye hadhi kama hiyo, na wengine wa kiwango kama hicho, kuinoa klabu hii.”
Kwa upande mwingine, kampeni ya Perez imejaribu kupuuzilia mbali mkakati wa Riquelme wa kuahidi kuwasajili nyota wakubwa mara moja, ikisema kuwa mpango huo si wa uhalisia.
Kuhusu mustakabali wake, kiungo wa Manchester City, Rodri, mwenye umri wa miaka 29, hivi karibuni amesema atafanya uamuzi kuhusu hatma yake baada ya Kombe la Dunia.
Amesema: “Mchezaji anapokaribia kipindi cha mwisho cha mkataba wake, ni kawaida majina ya klabu mbalimbali kutajwa.
Nimetulia sana, najua vizuri ninaposimama kwa sasa. Na naweza kusema kwamba pengine kama kusingekuwa na Kombe la Dunia, mambo yangekuwa tofauti kwa wakati huu.”