Tzolis bado kidogo tu kutua Arsenal
Muktasari:
- Taarifa zinaeleza nyota huyo mwenye umri wa miaka 24 anatarajiwa kukamilisha taratibu za mwisho za uhamisho wake baada ya Arsenal kuongeza kasi ya mazungumzo baada ya kuondoka kwa Leandro Trossard aliyesajiliwa na Besiktas kwa pauni milioni 17.
Arsenal imefikia makubaliano na Club Brugge ya Ubelgiji kumsajili mshambuliaji wa kimataifa wa Ugiriki, Christos Tzolis, kwa ada ya Pauni 34 milioni.
Taarifa zinaeleza nyota huyo mwenye umri wa miaka 24 anatarajiwa kukamilisha taratibu za mwisho za uhamisho wake baada ya Arsenal kuongeza kasi ya mazungumzo baada ya kuondoka kwa Leandro Trossard aliyesajiliwa na Besiktas kwa pauni milioni 17.
Hata hivyo, Arsenal bado inapanga kuongeza wachezaji wengine wa safu ya ushambuliaji kabla ya dirisha la usajili kufungwa.
Kocha Mikel Arteta anaaminika kuvutiwa na uwezo wa Tzolis wa kucheza nafasi mbalimbali za ushambuliaji, ikiwamo winga wa kushoto, kulia na mshambuliaji wa kati, jambo linalotarajiwa kuongeza ushindani katika kikosi hicho.
Tzolis amekuwa akionyesha kiwango bora katika misimu ya karibuni akiwa Club Brugge, akichangia mabao na pasi nyingi za mwisho katika mashindano ya ndani na Ulaya.
Arsenal inaamini usajili huo utaiimarisha safu yake ya ushambuliaji msimu ujao kwa ajili ya mashindano ya Ligi Kuu England na Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Sávio Moreira Savinho
Tottenham inaendelea na mazungumzo ya mwisho ya kumsajili winga wa Manchester City, Savinho, kwa dau linalokadiriwa kufikia Pauni milioni 65.
Taarifa zinaeleza kuwa pande zote mbili zinaonyesha matumaini ya kufikia makubaliano kamili hivi karibuni ili mchezaji huyo ajiunge na kikosi kabla ya kuanza kwa msimu mpya.
Aurele Amenda
Coventry City imemtambulisha rasmi beki wa kimataifa wa Uswisi, Aurele Amenda, kutoka Eintracht Frankfurt kwa mkataba wa miaka minne wenye thamani ya Pauni 17 milioni.
Mchezaji huyo anatarajiwa kuimarisha safu ya ulinzi ya klabu hiyo msimu ujao, huku kocha akiamini uzoefu wake Bundesliga utasaidia kuongeza ushindani katika kikosi chake.
Amenda amesema anafurahia changamoto mpya na yuko tayari kuisaidia Coventry City kufikia malengo yake katika msimu ujao.
Chrislain Matsima
Crystal Palace imeanza harakati za kumsajili beki wa kati wa Augsburg, Chrislain Matsima, huku ikisubiri ofa ya zaidi ya Pauni 50 milioni kutoka Chelsea kwa beki wake, Maxence Lacroix.
Palace inaamini Matsima anaweza kuziba pengo litakaloachwa na Lacroix endapo ataondoka dirisha hili la usajili. Mazungumzo baina ya pande husika yanaendelea.
Carl Rushworth
Newcastle inaendelea na mazungumzo ya kuwasajili makipa wawili, Carl Rushworth wa Brighton na James Trafford wa Manchester City ili kuimarisha kikosi chake msimu ujao.
Uongozi wa klabu hiyo unamchunguza kwa karibu kila mmoja kabla ya kufanya uamuzi wa mwisho, huku ukitaka mmoja wao awe kipa namba moja.
Trevoh Chalobah
Como ya Italia inatarajia kufanya mazungumzo mapya na Chelsea ili kumsajili beki Trevoh Chalobah, anayekadiriwa kugharimu Pauni 35 milioni, baada ya mapendekezo mawili ya awali kukataliwa.
Klabu hiyo bado inaonyesha nia kubwa ya kumpata mlinzi huyo na inaandaa ofa mpya ili kupeleka tena Chelsea.
Joao Gomes
Aston Villa imefikia hatua za mwisho za kumsajili kiungo Joao Gomes kutoka Wolves kwa ada ya Pauni 38 milioni. Pia inaendelea na mipango ya kumsajili Johan Manzambi, huku ikionyesha nia ya kumrejesha Joao Palhinha kutoka Bayern Munich.
Klabu hiyo inalenga kuimarisha safu ya kiungo kabla ya kuanza kwa msimu mpya.
Tarik Muharemovic
Leeds United ipo mbioni kukamilisha usajili wa beki Tarik Muharemovic kutoka Sassuolo kwa ada inayokadiriwa kufikia Pauni 34 milioni, huku makubaliano ya masilahi binafsi kati ya mchezaji na klabu tayari yakifikiwa.
Hatua zilizobaki zinahusisha kukamilisha vipimo vya afya na kusaini mkataba rasmi.
Conor Chaplin
Leicester City imekamilisha usajili wa kiungo mshambuliaji Conor Chaplin wa miaka mitatu kutoka Ipswich Town, ikiwa ni sehemu ya mipango ya kuimarisha kikosi chake msimu ujao.
Sambamba na hilo, klabu hiyo pia imemtambulisha rasmi kipa mkongwe Alex McCarthy ambaye amejiunga kwa uhamisho wa bure.
Crysencio Summerville
AS Roma imeongeza mazungumzo na West Ham kuhusu winga Crysencio Summerville, anayekadiriwa kuwa na thamani ya kati ya Pauni 45 hadi 50 milioni.
Wakati huohuo, klabu hiyo pia inafuatilia uwezekano wa kumpata Alejandro Garnacho kwa mkopo wenye kipengele cha kumnunua moja kwa moja.