Tuchel amvaa Palmer
Muktasari:
- Palmer ni miongoni mwa wachezaji wakubwa walioachwa kwenye kikosi cha England kitakachokabiliana na Croatia na Hispania katika michezo ijayo ya Ligi ya Mataifa (Nations League).
LONDON, ENGLAND; KOCHA wa timu ya taifa ya England, Thomas Tuchel, amempa ujumbe mzito kiungo mshambuliaji wa Chelsea, Cole Palmer, akisema mchezaji huyo anakosa nafasi nyingi za kujionyesha na kuthibitisha ubora wake ndani ya kikosi cha timu hiyo.
Palmer ni miongoni mwa wachezaji wakubwa walioachwa kwenye kikosi cha England kitakachokabiliana na Croatia na Hispania katika michezo ijayo ya Ligi ya Mataifa (Nations League).
Uamuzi huo umeibua maswali kwa kuwa Chelsea ilithibitisha kuwa nyota huyo yuko fiti kwa asilimia 100 na hana tatizo lolote la majeraha linaloweza kumzuia kucheza.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, kuachwa kwake hakukutokana na hali yake ya kiafya, bali ni uamuzi wa moja kwa moja wa Tuchel katika kuchagua wachezaji anaowaamini kwa sasa.
Akizungumza Ijumaa, Tuchel alisema Palmer anatamani kuichezea England kama ilivyo kwa wachezaji wengine, lakini amekuwa akikosa nafasi muhimu za kujidhihirisha.
"Nadhani kila mtu anatamani kuchezea England na Cole naye si tofauti. Lakini tunazungumzia mchezaji ambaye hayupo kambini.
"Nilisema mara ya mwisho kwamba anakosa nafasi nyingi za kujionyesha. Kambi ilikuwa ndefu, takribani wiki mbili na nusu, na wachezaji waliokuwepo walijenga kitu cha kipekee," alisema Tuchel.
Kocha huyo Mjerumani alisisitiza kuwa nafasi ya kuitumikia timu ya taifa inapaswa kuthibitishwa na mchezaji anapokuwa kambini, huku akiwapongeza waliokuwepo kwa kiwango walichoonyesha.
Aliongeza kuwa uamuzi huo si suala la binafsi dhidi ya Palmer, bali ni ushindani wa nafasi ndani ya kikosi.
"Si jambo la binafsi. Hatuwezi kudhani kwamba Cole hana hamu ya kuichezea nchi yake. Lakini ushindani upo na wale waliokuwa kambini walifanya kazi nzuri na wameendelea kubaki kwenye nafasi zao," aliongeza.
Mwezi uliopita, Tuchel aliwahi kuhoji mara kwa mara Palmer anakosa kambi za timu ya taifa, akidai mchezaji huyo amekuwa akikosa nafasi nyingi za kuungana na wenzake.
Nyota huyo mwenye umri wa miaka 24 alikosa michezo yote minne ya England iliyochezwa Septemba na Oktoba.
Kabla ya mapumziko hayo ya mechi za kimataifa, Palmer alicheza dakika zote 90 katika mchezo wa Chelsea dhidi ya Bournemouth, kabla ya kujiondoa kwenye kikosi cha England kutokana na jeraha dogo la misuli.
Baadaye alisafiri kwenda Caribbean akiwa na mpenzi wake, Olivia Holder, huku akisindikizwa na kocha wake binafsi wa mazoezi ya kurejea kwenye ubora wa kimwili.
Chelsea ilikuwa imemwandalia mpango maalumu wa mazoezi na kupona kulingana na aina ya jeraha lake.
Palmer alirejea katika kikosi cha Chelsea kwenye mchezo dhidi ya Brentford baada ya Ligi Kuu England kurejea, huku kocha wa Chelsea, Xabi Alonso, akisisitiza kuwa klabu hiyo inajua namna bora ya kumhudumia nyota huyo.
Alonso alisema ameridhishwa na kiwango, mwenendo na mchango wa Palmer ndani ya kikosi chake.
"Hatujazungumza kuhusu England. Tumekuwa tukizungumzia mchezo wetu wa Jumapili. Tunafurahia kuwa naye. Anafurahia soka lake, anaelewana vizuri na washambuliaji wengine na anaendelea kuisaidia timu," alisema Alonso.
Kocha huyo aliongeza kuwa kipaumbele chao ni kumsaidia Palmer kuwa mchezaji mwenye ushawishi mkubwa zaidi ndani ya Chelsea.
Alisisitiza kuwa mchezaji akiwa fiti anastahili kuchaguliwa na timu ya taifa, lakini anapokuwa na majeraha klabu inapaswa kutoa taarifa sahihi ili kufanya maamuzi kwa manufaa yake.