Emery: Man United ni sawa na Barcelona
Muktasari:
- Kauli hiyo ya Emery imekuja wakati Aston Villa ikijiandaa kuivaa Manchester United Jumapili, ikiwa imetoka kupokea kichapo cha mabao 3-0 dhidi ya Barcelona katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya katikati ya wiki.
LONDON, ENGLAND; KOCHA wa Aston Villa, Unai Emery, ameweka wazi kuwa Manchester United ni timu yenye hadhi na ubora unaolingana na Barcelona, licha ya klabu hiyo ya England kupitia kipindi cha kutokuwa na matokeo ya kuridhisha katika baadhi ya michezo ya Ligi Kuu.
Kauli hiyo ya Emery imekuja wakati Aston Villa ikijiandaa kuivaa Manchester United Jumapili, ikiwa imetoka kupokea kichapo cha mabao 3-0 dhidi ya Barcelona katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya katikati ya wiki.
Emery, ambaye amekuwa akihusishwa na uwezekano wa kuinoa Manchester United, alisema wapinzani wao wana uwezo mkubwa na wanastahili kuheshimiwa kama Barcelona.
"Tulipoteza dhidi ya Barcelona kwa sababu tulikutana na timu yenye kiwango cha juu kabisa katika Ligi ya Mabingwa. Manchester United iko kwenye kiwango hicho hicho cha Barcelona," alisema Emery.
Kocha huyo raia wa Hispania alikiri kuwa kucheza katika Uwanja wa Old Trafford kumekuwa changamoto kwake, akifichua kuwa hajawahi kupata ushindi katika mechi zake 11 zilizopita kwenye uwanja huo.
"Tumekuwa hatupati ushindi huko kwa miaka minne. Hata mchezo wetu wa kwanza wa Kombe la Carabao tulipoteza Old Trafford kwa mabao 4-2.
"Manchester United ni klabu kubwa na yenye historia. Wamekuwa wakifanya vizuri na wamewahi kufikia mafanikio makubwa katika Ligi ya Mabingwa," alisema.
Hata hivyo, Emery alibainisha kuwa United haijawa na mwendelezo mzuri wa matokeo katika ligi msimu huu, lakini anaamini wana uwezo wa kurejea kwenye ubora wao.
Alisema anatumaini mabadiliko hayo hayatakuja katika mchezo wao dhidi ya Aston Villa.
Wakati maandalizi ya mchezo huo yakiendelea, Emery pia anatarajiwa kuendelea na mazungumzo ya kuongeza mkataba wake Aston Villa, hatua inayoweza kumaliza uvumi unaomhusisha na Manchester United.
Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2029.
Emery alisema tayari amefanya mazungumzo mazuri na mwenyekiti wa klabu hiyo, Nassef Sawiris, na pande hizo zinatarajia kuendelea na mazungumzo katika mapumziko ya mechi za kimataifa.
"Nimefanya mkutano mzuri na mwenyekiti. Mazungumzo yalikuwa chanya sana. Wiki ijayo tutazungumza tena ili kujaribu kukamilisha tuliyoyajadili katika mkataba," alisema.
NDOTO YA UBINGWA
Kocha huyo mwenye umri wa miaka 55 pia amefichua kuwa ana ndoto ya kuifikisha Aston Villa kwenye hatua ya kushindania na hatimaye kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Emery alitumia mifano ya Leicester City, iliyotwaa ubingwa wa Ligi Kuu England mwaka 2016, pamoja na Borussia Dortmund na Villarreal, kuonyesha kuwa katika soka hakuna jambo lisilowezekana.
"Aston Villa ilitwaa ubingwa wa Ulaya mwaka 1982. Je, walikuwa timu iliyotabiriwa kushinda? Sidhani.
"Katika soka kila kitu kinawezekana. Villarreal tulifika nusu fainali miaka minne iliyopita, wakati Borussia Dortmund ilifika fainali miaka mitatu iliyopita.
"Timu ambazo hazipewi nafasi kubwa wakati mwingine hupata fursa ya kupigania mataji. Nina ndoto zangu na huwa naweka malengo makubwa," alisema.
Aliongeza kuwa bado ana imani na mradi wa Aston Villa na anaamini klabu hiyo inaweza kuendelea kupiga hatua kubwa chini ya uongozi uliopo.