Kwa nini mastaa England wanakimbilia Italia?
Muktasari:
- Ingawa majina yao yanajulikana sana, mchezaji wa kwanza wa England kuichezea ya Italia siyo maarufu sana; ni aliyekuwa mwanajeshi, Charles Adcock, alihamia Padova muda mfupi baada ya Vita vya Pili vya Dunia, baada ya kuonekana akicheza soka akiwa katika jeshi la Uingereza.
MILAN, ITALIA: JIMMY Greaves, Ray Wilkins, David Beckham, Paul Gascoigne na Kyle Walker wanafanana kwa jambo gani? Wote wamecheza mechi zaidi ya 50 katika timu ya taifa ya England, sambamba na timu za Italia.
Ingawa majina yao yanajulikana sana, mchezaji wa kwanza wa England kuichezea ya Italia siyo maarufu sana; ni aliyekuwa mwanajeshi, Charles Adcock, alihamia Padova muda mfupi baada ya Vita vya Pili vya Dunia, baada ya kuonekana akicheza soka akiwa katika jeshi la Uingereza.
Kwa namna ya kushangaza, Adcock hakuwahi kucheza soka la ligi katika nchi yake. Baada ya kutumia miaka michache nchini Italia alirejea England 1953 na kuichezea Peterborough United, iliyokuwa ikishiriki mashindano ya soka yasiyo ya ligi kuu.
Katika kipindi cha miaka 80 tangu Adcock alipohamia Italia, zaidi ya wachezaji 50 wa England wamecheza Ligi Kuu Italia (Serie A). Msimu huu, kuna wachezaji wengi zaidi wa England katika klabu za Italia kuliko wakati mwingine wowote, ambapo kati ya 21 wanaocheza wengi wao ni Waingereza akiwamo John Stones na Djed Spence, ambao walitua Inter Milan baada ya fainali za Kombe la Dunia 2026.
Zamani kulikuwa na wimbi la wachezaji maarufu wa England waliocheza Serie A katika miaka ya 1980, akiwamo Trevor Francis, mchezaji wa kwanza kuuzwa kwa ada ya Pauni 1 milioni aliyejiunga na Sampdoria 1982. Huko alikutana na Mark Hateley na Wilkins, ambao wote walitumia misimu mitatu AC Milan katikati ya miaka ya 1980.
Gascoigne alikuwa nyota mkubwa wa England nchini Italia katika miaka ya 1990, akifuatana na wachezaji waliocheza katika klabu mbalimbali katika kipindi cha taaluma zao, kama Franz Carr na Danny Dichio. Katika miongo hiyo miwili, wakati wowote ule, ni Waingereza wachache tu waliokuwa wakicheza Serie A, tofauti na sasa ambapo wapo 15 katika klabu za Italia.
Mashabiki wa soka nyumbani, England, walifuatilia kwa karibu maendeleo ya Waingereza hao waliokwenda kucheza Italia kupitia kipindi cha Gazzetta Football Italia, kilichoendeshwa na James Richardson. Siku hizi, matangazo ya Serie A yanafanywa na TNT yakiongozwa na mchambuzi na mtangazaji Adam Summerton.
“Sababu zake ni nyingi na zinahusiana kwa namna mbalimbali,” anasema Summerton akizungumzia wimbi la Waingereza wanaokwenda Italia.
“Yote yanaanzia kwa wale waliofungua njia. Mtu kama Liam Henderson, ambaye amekuwa Italia tangu mwaka 2018. Chris Smalling naye alikuwa mwingine aliyehamia huko mwaka 2019.”
Smalling alitumia miaka mitano katika Klabu ya Roma akitokea Manchester United na alikuwa mchezaji bora wa mechi katika fainali ya kwanza ya ligi 2022, wakati Roma ilipotwaa taji chini ya kocha José Mourinho.
“Wakurugenzi wa michezo wa Italia wamesema wanathamini sana bidii, weledi na uvumilivu wa wachezaji wa Scotland hasa,” anasema Summerton na kuongeza:
“Pia, wamejijengea sifa ya kuwa wachezaji wazuri katika vyumba vya kubadilishia nguo. Hilo linavutia sana unapokuwa unaunda timu.”
Summerton anaamini pia kuwa mtazamo kuhusu wachezaji wa Uingereza umebadilika. Kundi jipya la wachezaji lina watu wenye mitazamo mipana zaidi, ambao wanafurahia kikamilifu tamaduni tofauti.
“Dunia imekuwa ndogo zaidi, na mchezaji wa kisasa anaonekana kuwa na uwezekano mkubwa wa kuona fursa badala ya ugumu katika changamoto zinazotokana na kucheza nje ya nchi. Wachezaji mara nyingi huzungumzia namna uzoefu huo unavyowafanya wakue kiukomavu na kuwa watu na wachezaji waliokamilika zaidi,” anasema Summerton.
“Wengi wao wanalenga kuzikumbatia tamaduni, lugha na hata vyakula vya huko. Umahiri wa Scott McTominay katika kuthamini nyanya za mtindo wa Kineapoli umekuwa maarufu. Wengi wanapata uzoefu mzuri, jambo ambalo kwa kawaida litawafanya wengine nao kutaka kujaribu.”
Wachezaji wa Scotland wamechangia kuboresha mtazamo kuhusu soka la Uingereza nchini Italia. Lewis Ferguson, aliyehamia Bologna 2022, alichaguliwa kuwa kiungo bora wa Serie A 2023-24. Pia alikuwa nahodha wa klabu hiyo ilipoifunga Milan katika fainali ya Coppa Italia mwaka jana.
Baada ya mafanikio ya Ferguson, Scott McTominay alijiunga na Napoli na kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa Serie A, huku klabu hiyo ikishinda ubingwa wa ligi. Sababu nyingine ni kwamba wachezaji hao wanathamini historia na tamaduni tajiri za soka la Italia.
“Fikayo Tomori (Mwingereza mwingine) amezungumzia namna anavyoitazama nembo ya Milan kwenye suti yake ya michezo kila siku na kujivunia sana kuichezea klabu kubwa kama Milan,” anasema Summerton.
Tomori pia alijitahidi kujifunza Kiitaliano na muda mfupi baada ya kujiunga na klabu hiyo 2020, alikuwa tayari akifanya mahojiano kwa lugha hiyo. Hali hiyo inapingana na dhana kwamba wachezaji wa Uingereza hawapendi kuzoea tamaduni za nchi wanazokwenda kucheza.
Aidha, mafunzo katika akademi za soka za Ligi Kuu England yameendelea kuboreshwa kiasi cha kuzalisha wachezaji wenye uwezo mkubwa wa kiufundi, wanaoweza kuendana na mahitaji ya Serie A.
Mfano mmojawao ni Omari Hutchinson, aliyekuwa sehemu ya akademi ya Chelsea na ambaye hivi karibuni amejiunga na AC Milan kwa mkopo akitokea Nottingham Forest. Uhamisho wa Hutchinson pia unaonyesha suala jingine la kiuchumi, yaani tofauti kubwa ya uwezo wa kifedha kati ya Ligi Kuu England na ligi nyingine za Ulaya.
“Wachezaji wazuri ambao huenda wasiwe na nafasi ya kudumu katika kikosi cha klabu ya Ligi Kuu England wanaiona Italia kama fursa ya kuwa wachezaji muhimu zaidi katika ligi kubwa, wakichezea klabu zenye majina makubwa,” anasema Summerton.
Wimbi la Waingereza wanaohamia Italia linaonekana wazi zaidi kupitia Inter Milan iliyomsajili Curtis Jones kutoka Liverpool katika dirisha kubwa la usajili lililopita ili aungane na Spence na Stones. Kabla ya kuwasili kwao, Inter ilikuwa imewasajili wachezaji watatu tu wa England katika historia yake; Gerry Hitchens 1961, Paul Ince 1995 na Ashley Young 2020.
Stones alihama Manchester City na kwenda Milan dirisha lililopita la usajili, na furaha yake ya kujiunga na Inter ilikuwa wazi.
“Nina hisia nyingi sana. Nina furaha, najivunia na nina shauku kubwa. Sikuweza kufikiria mahali pazuri zaidi pa kufanya hivyo.”
Summerton anapiga hesabu ni nani atakayevutia zaidi msimu huu? “Dalili za awali kutoka kwa Jones ni nzuri. Ni aina ya mchezaji ambaye Cristian Chivu, kocha wa Inter, alikuwa akimhitaji sana,” anasema.
Uchezaji wake alipokuwa akiichezea Liverpool dhidi ya Inter katika Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uliopita uliweka msingi wa uwezekano wa uhamisho huo.
“Pia nina shauku kubwa ya kumuona Trevoh Chalobah. Amejiunga na mojawapo ya miradi inayosisimua zaidi katika soka la dunia kwa sasa, huko Como. (kocha) Cesc Fabregas anafanya kazi nzuri sana. Chalobah ameanza msimu vizuri na tayari timu hiyo ina uimara mkubwa katika ulinzi.”
Chalobah anajua nini cha kutarajia kutoka kwa Fabregas kwa sababu waliwahi kufanya mazoezi pamoja Chelsea.
“Nakumbuka jinsi alivyokuwa akiwataka sana wachezaji vijana. Namfahamu vizuri sana,” anasema Chalobah, beki wa kati.
Kufanya kazi na gwiji wa soka katika klabu yenye malengo makubwa ni jambo linalomvutia Chalobah. Na kama Summerton anavyoeleza: “Anapata nafasi ya kuishi karibu na Ziwa Como na kucheza soka la Ligi ya Mabingwa pia. Kuna mambo mengi ya kufurahia.”