Wikiendi ya moto Championship
Muktasari:
- Katika mechi zilizochezwa jana Ijumaa, Bigman FC iliyoichapa Mbeya Kwanza kwa mabao 2-1, wiki iliyopita, ilikuwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani, jijini, Tanga kuikaribisha Songea United iliyotoka kuifunga maafande wa Transit Camp kwa mabao 3-2.
RAUNDI ya tisa ya Ligi ya Championship imeanza jana Ijumaa kwa mechi mbili kuchezwa na tatu zikichezwa leo Jumamosi na nyingine kesho Jumapili, ikiwa ni wikiendi ya moto kwa vigogo mbalimbali kutokana na ushindani unaoendelea msimu huu.
Katika mechi zilizochezwa jana Ijumaa, Bigman FC iliyoichapa Mbeya Kwanza kwa mabao 2-1, wiki iliyopita, ilikuwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani, jijini, Tanga kuikaribisha Songea United iliyotoka kuifunga maafande wa Transit Camp kwa mabao 3-2.
Vinara wa Ligi hiyo, KMC FC yenye pointi 18, baada ya kuifunga Stand United ‘Chama la Wana’ bao 1-0, jana ilikuwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, jijini, Dar es Salaam kuikaribisha Rhino Rangers iliyotoka sare ya bao 1-1 na Gunners FC.
Katika mechi za leo, Stand United ‘Chama la Wana’ iliyochapwa bao 1-0 na KMC FC, itakuwa kwenye Uwanja wa CCM Kambarage, mjini, Shinyanga, kuikaribisha KenGold FC ya jijini, Mbeya yenye kumbukumbu ya kuchapwa na Mbuni FC ya Arusha mabao 3-2.
Katika mechi nane ilizocheza Stand United, imeshinda nne, sare moja na kupoteza tatu, ikiwa nafasi ya saba na pointi 13, huku KenGold ikishinda miwili, sare miwili na kupoteza minne, ambapo kikosi hicho kinashika nafasi ya 11 na pointi nane.
kwenye Uwanja wa Aga Khan, jijini, Arusha, IAA SC iliyotoka sare ya mabao 2-2, dhidi ya Kigamboni United wiki iliyopita, itaikaribisha maafande wa Tanzania Prisons ya jijini, Mbeya, yenye kumbukumbu nzuri ya kutoka kuichapa TMA FC mabao 5-0.
IAA SC inayoshiriki Ligi ya Championship kwa mara ya kwanza msimu wa 2026-2027, katika mechi nane ilizocheza imeshinda mbili, sare nne na kupoteza mbili, ikishika nafasi ya tisa na pointi 10, huku ikifunga mabao manane na kuruhusu pia 10.
Kwa upande wa Prisons, inashika nafasi ya pili na pointi 16, nyuma ya vinara KMC FC yenye 18, ambapo kikosi hicho cha maafande kimeshinda mitano, sare moja na kupoteza miwili kati ya minane, huku kikifunga mabao 13 na kuruhusu matano.
Prisons itaendelea kumtegemea mshambuliaji nyota wa kikosi hicho, Oscar Paul aliyefunga mabao sita kati ya 13, ya timu hiyo, huku IAA SC ikiwategemea zaidi Ombeni Sefue na Goodluck Tapioh ambao ndio waliofunga mabao mawili kila mmoja wao.
Mechi ya mwisho leo Jumamosi, itachezwa kwenye Uwanja wa Samora, mjini, Iringa, ambapo TMA FC inayoburuza mkiani ikiwa nafasi ya 16 na pointi mbili, itakuwa na kibarua kigumu cha kucheza na Mtibwa Sugar inayoshika nafasi ya tatu na pointi 15.
TMA FC iliyohamishia makazi yake mjini, Iringa ikitokea jijini, Arusha, katika mechi nane, imeshinda moja, sare mbili na kupoteza mitano, huku kwa upande wa Mtibwa Sugar ikishinda minne, sare mitatu na kupoteza mmoja tu hadi sasa msimu huu.
Raundi ya tisa itahitimishwa kesho Jumapili kwa mechi tatu kuchezwa na Bandari Tanzania iliyotoka kuchapwa bao 1-0 na Mtibwa Sugar, itakuwa kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara, kuikaribisha Kigamboni United kutoka Dar es Salaam.
Katika mechi nane ilizocheza Bandari Tanzania imeshinda minne, sare mbili na kupoteza pia miwili, ikishika nafasi ya nne na pointi 14, huku Kigamboni United ikishinda mitatu, sare mitatu na kupoteza miwili, ikiwa nafasi ya nane na pointi 12.
Kigamboni United inaingia katika mechi hii ikimtegemea mshambuliaji nyota wa kikosi hicho, Abdulkarim Segeja ambaye hadi sasa ameifungia mabao sita, akizidiwa matatu na kinara, Hamdan Sarhani wa maafande wa Transit Camp anayeongoza na tisa.
Maafande wa Transit Camp iliyochapwa mabao 3-2, dhidi ya Songea United, itakuwa kwenye Uwanja wa Uhuru, jijini, Dar es Salaam kuikaribisha Mbuni FC ya jijini, Arusha, yenye kumbukumbu nzuri ya kutoka kuifunga KenGold FC ya Mbeya mabao 3-2.
Katika mechi nane ilizocheza Transit Camp, imeshinda minne, sare moja na kupoteza mitatu, ikiwa nafasi ya sita na pointi 13, huku kwa upande wa Mbuni FC, ikishinda miwili, sare miwili na kupoteza minne, ikishika nafasi ya 12 na pointi nane.
Miongoni mwa washambuliaji wa kuchungwa ni Hamdan Sarhani wa Transit Camp, ambaye nyota huyo amekuwa katika kiwango bora hadi sasa, akiongoza katika mbio za ufungaji akiwa amefunga mabao tisa kati ya 13, yaliyofungwa na kikosi hicho kizima.
Kwa upande wa Mbuni FC, itaendelea kuwategemea washambuliaji wawili wanaofanya vizuri kwa sasa, wakiongozwa na Ezekiel Zonobi mwenye mabao manne na Mussa Mpina aliyefunga matatu wakihusika na mabao saba kati ya tisa ya kikosi hicho kizima.
Mechi ya mwisho kesho Jumapili itachezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri, jijini, Dodoma, ambapo wenyeji, Gunners FC iliyotoka sare ya bao 1-1, dhidi ya Rhino Rangers, itaikaribisha Mbeya Kwanza yenye kumbukumbu ya kuchapwa na Bigman FC mabao 2-1.
Katika mechi nane ilizocheza Gunners, imeshinda moja, sare tano na kupoteza miwili, ikiwa nafasi ya 10 na pointi nane, huku kwa upande wa Mbeya Kwanza, ikishinda miwili, sare moja na kupoteza mitano, ikishika nafasi ya 13 na pointi saba.
Kocha Mkuu wa Gunners FC, Mohamed Ismail ‘Laizer’, alisema mwenendo wa timu hiyo sio mzuri kutokana na aina ya makosa ambayo wachezaji wanayafanya katika eneo la kujilinda, ingawa, anaendelea kushughulikia ili kuendana na ushindani huo.
Kwa upande wa Kocha Msaidizi wa Mbeya Kwanza, Henry Joseph Shindika alisema miongoni wa changamoto za kikosi hicho ni makosa binafsi ya mchezaji mmoja, japo, bado wana nafasi ya kurekebisha hali hiyo na kujiweka katika mazingira mazuri.