Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Jesus: sina hatia kwa Ronaldo

Muktasari:

  • Kauli ya Jesus imekuja baada ya Ronaldo kutangaza rasmi kustaafu kuitumikia timu ya taifa ya Ureno, akihitimisha safari ya miaka 23 iliyomfanya kuwa miongoni mwa wachezaji wakubwa zaidi katika historia ya soka la kimataifa.

 LISBON, URENO; KOCHA wa timu ya taifa ya Ureno, Jorge Jesus, amesema hana hatia yoyote kuhusu uamuzi wa nyota wa kikosi hicho, Cristiano Ronaldo, kustaafu soka la kimataifa, akifichua kuwa hakujua kama mshambuliaji huyo alikuwa akijiandaa kufanya uamuzi huo.

Kauli ya Jesus imekuja baada ya Ronaldo kutangaza rasmi kustaafu kuitumikia timu ya taifa ya Ureno, akihitimisha safari ya miaka 23 iliyomfanya kuwa miongoni mwa wachezaji wakubwa zaidi katika historia ya soka la kimataifa.

Uamuzi huo umefuatia mgogoro mkubwa kati ya Ronaldo na kocha huyo, uliozidi kuwa mkali baada ya nyota huyo kuachwa benchi katika mchezo wa Ligi ya Mataifa dhidi ya Norway.

Ronaldo, mwenye umri wa miaka 41, alionyesha kutoridhishwa na uamuzi huo, hali iliyosababisha uhusiano wake na kocha huyo kuyumba.

Akizungumza kwa mara ya kwanza baada ya tangazo la Ronaldo, Jesus alisema anaheshimu uamuzi wa mshambuliaji huyo na haoni sababu ya kujilaumu.

"Sijisikii kuwa na hatia yoyote kuhusu kuondoka kwake. Ninaheshimu uamuzi wake na historia yake haiwezi kupuuzwa.

"Ronaldo atabaki kuwa alama kubwa katika soka. Nimejenga naye urafiki mzuri katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu. Amefanya uamuzi wake na ninauheshimu sana," alisema Jesus.

Alipoulizwa kama anaamini yeye ndiye sababu ya Ronaldo kustaafu, Jesus alisema hakuwahi kuwa na taarifa kwamba mchezaji huyo alikuwa akifikiria kufanya hivyo kwa wakati huo.

"Labda niliharakisha baadhi ya mambo, lakini si kwa sababu yangu. Nafikiri uamuzi huo ulikuwa tayari ndani ya mawazo yake na ulikuwa ni jambo ambalo lingetokea wakati fulani," alisema.

Jesus aliongeza kuwa Ronaldo ndiye anayejua sababu halisi zilizomfanya achukue uamuzi huo na ni yeye pekee anayeweza kueleza zaidi.

REKODI YA KIHISTORIA

Ronaldo anastaafu timu ya taifa akiwa ameweka rekodi ya kufunga mabao 146 katika mechi 234 alizoichezea Ureno, ikiwa ni rekodi ya dunia kwa upande wa mabao ya timu za taifa kwa mujibu wa taarifa hiyo.

Katika kipindi hicho, aliisaidia Ureno kutwaa ubingwa wa Mataifa ya Ulaya mwaka 2016, pamoja na mataji mawili ya Ligi ya Mataifa.

Safari yake ya kimataifa ilianza zaidi ya miongo miwili iliyopita, huku akijijengea jina kubwa kutokana na mabao, rekodi na mchango wake katika mafanikio ya timu hiyo.

Katika ujumbe wake wa kuaga, Ronaldo alisema haikuwa rahisi kufanya uamuzi huo, lakini amefikia wakati wa kukabidhi jezi namba saba kwa kizazi kijacho.

"Kwa watu wa Ureno, siku imefika ya kurudisha jezi namba saba ya timu yetu ya taifa.

"Kwa miaka 23 nilikuwa na bahati na jukumu la kuivaa, kuitetea na kuiwakilisha katika viwanja mbalimbali duniani.

"Haikuwa uamuzi rahisi kwa sababu baadhi ya maamuzi hayafanywi kwa kutumia akili pekee, bali pia moyo," alisema Ronaldo.

Alikiri kuwa katika safari yake kulikuwa na nyakati za furaha, ushindi, kushindwa na hata nyakati ambazo alihisi hakuweza kuwapa Wareno kile walichokitarajia.

Hata hivyo, alisema hakuwahi kukata tamaa wala kuacha kujivunia kuichezea nchi yake.

Alisisitiza kuwa mafanikio, mataji na rekodi vinaweza kupitwa na wakati, lakini kumbukumbu na nafasi ambayo mchezaji anakuwa nayo katika mioyo ya mashabiki haviwezi kufutika.

MGOGORO

Kustaafu kwa Ronaldo kumekuja baada ya mvutano ulioanza kufuatia kuachwa kwake benchi katika mchezo dhidi ya Norway.

Kwa mujibu wa taarifa zilizoripotiwa, Ronaldo alikasirishwa na namna Jesus alivyoeleza sababu za kutomtumia katika mchezo huo licha ya kumruhusu kufanya mazoezi ya kujipasha moto.

Mshambuliaji huyo alidai kocha alikuwa amevunja ahadi ya kumpa dakika 30 za kucheza, jambo lililochangia kuibuka kwa mgogoro mkubwa.

Baadaye Ronaldo alikosa mazoezi kadhaa na kuondoka kambini kabla ya timu kumaliza michezo yake ya mapumziko ya kimataifa, akisafiri kwa ndege yake binafsi.

Jesus, kwa upande wake, alieleza kuwa hakuwa na mpango wa kumtumia Ronaldo katika mchezo huo, lakini alibadili mawazo baada ya kuona nyota huyo amerejea vizuri kimwili.

Alisema alimweleza Ronaldo kuwa huenda akamhitaji na mchezaji huyo alikubaliana naye.

Kutokana na tukio hilo, Shirikisho la Soka la Ureno lilimtoza Ronaldo faini ya pauni 215 na kumpa adhabu ya kufungiwa kwa mwezi mmoja, ambayo muda wake ulianza kuhesabiwa nyuma, hivyo kumruhusu kuwa huru kwa michezo iliyokuwa mbele yake.

Hata hivyo, sasa mjadala mkubwa umehamia kwenye namna Ureno itakavyoendelea bila nahodha na mfungaji bora katika historia yake.