Tatu za EPL vitani kuwania saini ya Raheem Sterling
Muktasari:
- Kwa mujibu wa chanzo hicho, kocha mpya wa Chelsea, Enzo Maresca, ameweka wazi kuwa Sterling hayumo kwenye mipango yake ya msimu wa 2025/26, na hivyo kumruhusu kutafuta timu nyingine.
TOVUTI ya TalkSport imefichua kuwa mshambuliaji wa Chelsea na timu ya taifa ya England, Raheem Sterling, anawindwa na klabu tatu za Ligi Kuu England ambazo ni Fulham, Crystal Palace na West Ham United, zinazotaka kumsajili katika dirisha hili la majira ya kiangazi.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, kocha mpya wa Chelsea, Enzo Maresca, ameweka wazi kuwa Sterling hayumo kwenye mipango yake ya msimu wa 2025/26, na hivyo kumruhusu kutafuta timu nyingine.
Sterling, 29, alijiunga na Chelsea Julai 2022 akitokea Manchester City kwa ada ya takribani Pauni 47.5 milioni na hadi sasa amebakiza miaka miwili kwenye mkataba wake unaomalizika mwaka 2027. Anaripotiwa kuwa miongoni mwa wachezaji wanaolipwa zaidi katika kikosi cha Chelsea, akiwa na mshahara wa takribani Pauni 325,000 kwa wiki.
Katika msimu uliopita akiwa kwa mkopo Arsenal alicheza mechi 28 za michuano yote, akafunga bao moja na kutoa asisti tano.
West Ham inaona Sterling anaweza kuwa suluhisho la haraka katika safu ya ushambuliaji, hasa baada ya kuachana na baadhi ya wachezaji wakongwe kama Michail Antonio.
Fulham pia wanamwona Sterling kama mbadala mzuri wa Willian ambaye imeachana naye mwisho wa msimu huu.
Chelsea wanapanga kupunguza mzigo wa mishahara kwa kuachana na baadhi ya wachezaji wakubwa ambao hawatoi mchango wa kutosha na Sterling anaonekana kuwa miongoni mwa wanaoweza kuuzwa ili kuipatia klabu fedha na nafasi kwa wachezaji wapya.
Carlos Baleba
MANCHESTER United imeanza mawasiliano ya awali kupitia mawakala na klabu ya Brighton ili kumsajili kiungo wa kati kutoka Cameroon, Carlos Baleba, 21.
Baleba ambaye alijiunga na Brighton mwaka 2023 akitokea Lille kwa ada ya takribani Pauni 23 milioni katika msimu uliopita alicheza mechi 40 za michuano yote, akufunga mabao manne na kutoa asisti mbili, mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwaka 2028.
Malick Thiaw
NEWCASTLE imewasilisha ofa ya Euro 30 milioni kwa ajili ya beki wa kati wa AC Milan na timu ya taifa ya Ujerumani, Malick Thiaw, 23, katika dirisha hili. Hata hivyo, Milan imekataa ofa hiyo ikisisitiza kuwa haina mpango wa kumuuza mlinzi huyo aliyecheza mechi 34 msimu uliopita kwenye Serie A. Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2027, inaelezwa mabosi wa Milan wapo tayari kumuuza staa huyu lakini ni kwa Euro 40 milioni.
Mateo Kovacic
KIUNGO wa Manchester City, Mateo Kovacic, 31, amepokea ofa kutoka klabu kadhaa za Saudi Arabia, lakini raia huyo wa Croatia amesisitiza kutaka kuendelea kusalia Etihad Stadium kwani anaamini bado anaweza kuendelea kucheza soka la kiushidani. Kovacic aliyesajiliwa na Man City akitokea Chelsea mwaka 2023, amekuwa mchezaji ni kati ya wachezaji wa akiba kocha Pep Guardiola.
Douglas Luiz
NOTTINGHAM Forest iko katika hatua nzuri kukamilisha usajili wa kiungo wa kati kutoka Brazil, Douglas Luiz, 27 kutoka Juventus. Ikiwa dili hiyo itakamilika, Juventus wanaweza kuangalia uwezekano wa kumsajili kiungo wa kati wa Nottingham Forest na timu ya taifa ya Ivory Coast, Ibrahim Sangare, 27. Luiz amekuwa hakupata nafasi ya kutosha katika kikosi cha kwanza cha Juventus.
Harvey Elliott
RB Leipzig ipo katika hatua nzuri kwenye mazungumzo ya kumsajili kiungo wa kati wa Liverpool, Harvey Elliott, 22. Katika msimu uliopita, Elliott alicheza mechi 28 za michuano yote, akafunga mabao matano na kitoa asisti tatu. Leipzig inataka kumsajili staa huyu kwa ajili ya kuboresha zaidi kikosi chao ambacho karika dirisha hili kimeondokewa na wachezaji kadhaa muhimu. Mkataba wa Elliott unaisha mwaka 2027.
Christian Eriksen
KIUNGO wa zamani wa Manchester United, Christian Eriksen anawindwa na Burnley ambayo inahitaji kumsajili katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi kwa ajili ya kuboresha zaidi kikosi chao.
Eriksen ambaye kwa sasa yupo huru tangu aachane na Man United Julai mwaka huu,hivi karibuni pia alikuwa akihitajika na Wrexham inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza England.
Mason Greenwood
OLYMPIQUE de Marseille imesisitiza kwamba mshambuliaji wao wa kimataifa wa Jamaica, Mason Greenwood hauzwi katika dirisha licha ya ripoti zinazodai kwamba ana ofa nono kutoka Saudi Arabia. Greenwood ambaye ni miongoni mwa wachezaji tegemeo wa kikosi cha kwanza cha Marseille, mkataba wake unaisha 2029.