Swahiba wa Mo Salah afichua jambo zito
Muktasari:
- Mo Salah amekuwa mchezaji muhimu kwelikweli kwenye kikosi hicho cha Kocha Arne Slot kinachofukuzia mataji matatu msimu huu, lakini ishu ya mkataba wake ipo kwenye mashaka makubwa kama atabaki au ataondoka bure mwishoni wa msimu.
LIVERPOOL, ENGLAND: SWAHIBA wake supastaa wa Liverpool, Mohamed Salah, ambaye ni beki wa zamani wa miamba hiyo ya Anfield, Dejan Lovren amefunguka akidai mabosi wa timu hiyo hawampi heshima anayostahili rafiki yake na kufichua kuna nafasi kubwa ya mkali huyo kuondoka kuliko kusaini dili jipya.
Mo Salah amekuwa mchezaji muhimu kwelikweli kwenye kikosi hicho cha Kocha Arne Slot kinachofukuzia mataji matatu msimu huu, lakini ishu ya mkataba wake ipo kwenye mashaka makubwa kama atabaki au ataondoka bure mwishoni wa msimu.
Salah ni moja ya mastaa watatu wenye majina makubwa kwenye kikosi cha Liverpool ambao mikataba yao itafika ukomo mwishoni mwa msimu huu, huku wengine ni mabeki mahiri kabisa, Virgil van Dijk na Trent Alexander-Arnold.
Kwenye kesi ya Salah ishu kubwa ni pesa na urefu wa mkataba mpya na kama mabosi wa Liverpool watafanya atachokitaka mchezaji huyo, kipaumbele chake ni kuendelea kubaki Anfield kuliko kuondoka. Lakini, matajiri wa Saudi Pro League imeshaweka wazi dhamira ya kunasa saini ya mchezaji huyo, ambaye inamtazama kama mmoja wa masupastaa inaotaka wakacheza kwenye lig hiyo.
Na Lovren, ambaye ni rafiki mkubwa wa Mo Salah alisema mabosi wa Liverpool wanapaswa kufikia mahitaji anayotaka mchezaji huyo kama wanataka abaki hasa kutokana na anachokionyesha ndani ya uwanja huku akiwa na utimamu wa kutosha.
“Bado tunawasiliana. Tunazungumza sana, ndiyo,” alisema Lovren.
“Napaswa kuwa makini ninachokisema kwa sasa, kwa sababu nafahamu vitu vingi sana. Ukweli, sifahamu namba halisi, lakini chochote anachotaka kulipwa, kinastahili. Ni rahisi tu, huyu jamaa anafanya kazi yake uwanjani.
“Usiangalie umri wake, kuna watu watasema atafikisha 33, lakini mtazame Ronaldo, ana 40 na bado anacheza. Mohamed Salah bado anafunga mabao, bado yupo kwenye hali ya utimamu wa mwili na akili. Bado anachezea timu ya taifa, kwa hiyo tatizo ni nini? Ni mdogo kwa miaka saba au nane kwa kumlinganisha na Ronaldo. Kwa hiyo, tatizo la Salah ni nini? Hakuna mwenye majibu na ndiyo maana naona kuna ugumu.
“Naweza kuzungumza vitu fulani. Salah anaamini kuna baadhi ya vitu vinakosekana kwa upande wa klabu, naamini zitamalizwa hivi karibuni. Lakini, kwa hali ilivyo kwa sasa, kuna uwezekano mkubwa wa kuondoka kuliko kubaki. Kila mtu anataka abaki, hata mimi nataka abaki. Nilimpigia simu siku moja na kumwambia: 'Mo, hebu jifikirie mwenyewe kwanza. Ona kila kitu ulichofanya kwenye hii klabu na nini unachoweza kuendelea kuipa timu.'
“Mwisho wa yote, nimefikia hitimisho kwamba klabu haimpi heshima ya kutosha, au hawaoni kama anastahili chochote, lakini huo ni upande wa pili wa stori, hicho kinachoendelea huko nyuma ya pazia. Kila mtu atakubali akitazama namba, hakuna mchezaji mwenye takwimu nzuri kama Mohamed Salah, sio msimu huu, lakini mfululizo kwa misimu 5-6 iliyopita, sio tu namba, ni balaa.
“Nadhani hapewi nafasi sana licha ya kuwa na namba bora kama hizo, kwa sababu kama angekuwa Messi au Ronaldo, tungeona mazungumzo kila siku na kusikia kwa nini hajasaini mkataba mpya hakukuwa na ofa nzuri, lakini bahati mbaya, Mohamed Salah hapewi kipaumbele kinachostahili.”
Lovren alisema Salah anataka kubaki Liverpool kama itawezekana, lakini uhamisho wa kwenda kukipiga kwenye Saudi Pro League upo kwenye mpango kama atashindwa kufikia makubaliano na mabosi wa Anfield.
“Anaipenda Liverpool, ukweli anaipenda sana Liverpool,” alisema Lovren akiambia WinWin.
“Na anataka kubaki na hicho ndicho kitu muhimu kwake. Pengine anajiona mwenyewe akistaafu kwenye timu hiyo, mimi sina uhakika wa mambo yote, lakini mwisho wa yote si suala la nani yupo naye, bali linawahusu watu wengine. Hivyo, ngoja tuone kitakachotokea."