Prime
Simba na rekodi ya miaka mitano
SIMBA SC imeendelea na utamaduni wake wa kuanza msimu wa Ligi Kuu Bara kwa ushindi baada ya leo, Agosti 16, 2026 kuifunga Kagera Sugar mabao 2-0, katika mchezo wa kwanza wa msimu wa 2026-2027.
Ushindi huo umeifanya Simba kufikisha misimu mitano mfululizo ikishinda mchezo wake wa kwanza, bila kupata sare wala kupoteza katika kipindi hicho.
Simba ilianza mfululizo huo msimu wa 2022-2023 kwa kuifunga Geita Gold mabao 3-0, kabla ya kuendeleza rekodi hiyo katika misimu iliyofuata.
Msimu wa 2023/24, ilianza kwa ushindi wa mabao 4-2 dhidi ya Mtibwa Sugar, huku msimu wa 2024/25 ikiifunga Tabora United (sasa TRA United) mabao 3-0.
Msimu wa 2025/26, Wekundu hao wa Msimbazi waliendelea na mwendo huo kwa kuichapa Fountain Gate mabao 3-0, kabla ya leo kuifunga Kagera Sugar mabao 2-0.
Ismael Toure na Elie Mpanzu ndio walioandika majina yao kwenye ubao wa wafungaji katika ushindi huo wa leo, mechi ikichezwa Uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera.
Mara ya mwisho Kagera Sugar kucheza na Simba uwanjani hapo mechi iliyopigwa Desemba 21, 2024, ilifungwa mabao 5-2.
Mechi ya leo, dakika 45 za kipindi cha kwanza beki wa Simba, Ismail Toure alifunga bao la kuongoza akiunganisha mpira wa kona uliopigwa na Libasse Gueye ambaye msimu uliopita wa 2025-2026 alifunga mabao saba.
Kabla ya bao hilo lililoamsha shangwe za mashabiki, mshambuliaji mpya wa Simba, Ibrahim Doumbia alipiga shuti nje ya 18 ambalo liligonga mwamba dakika za mwanzoni.
Kipindi cha pili kilianza vibaya kwa Simba kwa mchezaji wake David Kameta 'Duchu' kuonyeshwa kadi nyekundu baada ya kufanya faulo.
Baada ya Duchu kuonyeshwa kadi nyekundu, Kocha Mkuu wa Simba, Steve Barker alifanya mabadiliko ya kuwatoa Morice Abraham, Doumbia na kuingia Mpanzu na Nathaniel Chilambo.
Mpanzu aliyeingia kipindi cha pili, aliifungia Simba bao la pili dakika 69 alichongewa krosi nzuri Gueye ambaye ndiye aliyesababisha bao la kwanza na kumfanya nyota huyo kutengeneza mabao mawili.
Mpanzu anafungua akaunti ya mabao ya msimu huu wa 2026-2027 baada ya uliopita kumaliza na saba, huku akiwa kinara wa asisti akifikisha 10.
Dakika ya 82, golikipa wa Simba, Djibrilla Kassali aliumia, akatolewa, nafasi yake ilichukuliwa na Hussein Abel.
KABLA YA HAPO
Kabla ya kuanza mfululizo wa ushindi wa misimu mitano, Simba ilianza msimu wa 2021-2022 kwa sare ya bila kufungana dhidi ya Biashara United, mchezo uliochezwa Septemba 28, 2021.
Mchezo huo ulikuwa na kumbukumbu ya kipekee baada ya mshambuliaji na nahodha wa Simba wakati huo, John Bocco, kukosa penalti dakika za mwisho baada ya mkwaju wake kudakwa na kipa James Ssetupa.
Hata hivyo, sare hiyo ndiyo iliyokuwa ya mwisho kwa Simba katika mchezo wake wa kwanza wa msimu, kwani tangu msimu wa 2022-2023 imekuwa ikianza kampeni kwa ushindi.
REKODI YA MIAKA 15
Simba imekuwa na rekodi nzuri ya kuanza misimu tangu 2012-2013, ikiwa haijawahi kupoteza mchezo wake wa kwanza katika kipindi hicho.
Msimu wa 2012-2013, ilianza kwa ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya African Lyon, Septemba 15, 2012.
Msimu uliofuata, 2013-2014, ilitoka sare ya mabao 2-2 na Rhino Rangers, kabla ya kupata sare nyingine ya mabao 2-2 dhidi ya Coastal Union msimu wa 2014-2015.
Msimu wa 2015-2016, Simba ilirejea kwenye ushindi kwa kuifunga African Sports bao 1-0, kisha msimu wa 2016-2017 ikaichapa Ndanda mabao 3-1.
Msimu wa 2017-2018 ulikuwa mwanzo wa kuvutia zaidi katika kipindi hicho, Simba ilipoifunga Ruvu Shooting mabao 7-0.
Baadaye iliifunga Tanzania Prisons bao 1-0 msimu wa 2018-2019, JKT Tanzania mabao 3-1 msimu wa 2019-2020 na Ihefu mabao 2-1 msimu wa 2020-2021.
Kisha ikaja sare ya Biashara United msimu wa 2021-2022, kabla ya kuanza kwa mfululizo wa ushindi wa misimu mitano unaoendelea hadi sasa.
HAINA KIPIGO
Kwa jumla, katika michezo 15 ya kwanza kwa Simba katika ligi tangu 2012-2013, timu hiyo imeshinda 12 na kutoka sare tatu, haijapoteza.
Katika kipindi hicho, imefunga jumla ya mabao 35, huku ikiruhusu mabao 14.
Mwanzo wake wenye matokeo makubwa zaidi ulikuwa msimu wa 2017-2018 ilipoifunga Ruvu Shooting mabao 7-0, wakati ushindi wa leo dhidi ya Kagera Sugar ukiwa miongoni mwa ushindi wake wa kwanza wenye tofauti ya mabao mawili.
Hivyo, licha ya kuanza kwa ushindi katika misimu mitano mfululizo tangu 2022-2023, rekodi kubwa zaidi ya Simba ni kutopoteza mchezo wake wa kwanza wa Ligi Kuu Bara kwa misimu 15 mfululizo katika kipindi hiki.
Hata hivyo, Simba imekuwa na mtihani mkubwa wa kubeba ubingwa wa ligi kwani haijafanikiwa tangu ilipobeba mara ya mwisho 2020-2021. Imeukosa misimu mitano mfululizo.
Katika kipindi cha kuanzia 2012-2013, Simba imebaba ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara nne pekee ambapo ni 2017-2018, 2018-2019, 2019-2020 na 2020-2021.
Azam katika kipindi hicho imechukua mara moja msimu wa 2013-2014, huku Yanga ikitawala kwa kubeba mara tisa.