SUAREZ: Mpira unaisha, pesa zinaongezeka

Muktasari:
- Katika mchezo huo safu ya ushambuliaji ya Miami iliongozwa na Lionel Messi na Luis Suarez ambaye alionekana kuwa tofauti kabisa na vile alivyozoeleka miaka mitano nyuma.
FLORIDA, MAREKANI: ALFAJIRI ya Jumapili, macho ya mashabiki wa soka duniani yalikuwa Florida Miami wakitazama mchezo wa ufunguzi wa michuano ya Kombe la Dunia la Klabu kati ya Al Ahly na Inter Miami uliopigwa kwenye dimba la Hard Rock.
Katika mchezo huo safu ya ushambuliaji ya Miami iliongozwa na Lionel Messi na Luis Suarez ambaye alionekana kuwa tofauti kabisa na vile alivyozoeleka miaka mitano nyuma.
Hata hivyo, licha ya kiwango chake kuonekana kushuka, staa huyu bado anaendelea kutajirika siku hadi siku kutokana na pesa anazoingiza kupitia mshahara na madili yake mengine nje ya uwanja.

ANAPIGAJE PESA
Kijumla Suarez anakadiriwa kuwa na utajiri unaofikia Dola 70 milioni ambayo umejengeka na mishahara mbalimbali aliyoipata akiwa na timu mbalimbali pamoja na mikataba yake ya udhamini na kampuni mbalimbali.
Kwa sasa staa huyu anapokea mshahara unaofikia Dola 1 milioni kwa mwaka akiwa na Inter Miami hiyo ikiwa ni mjumuisho wa bonasi mbalimbali.
Kabla ya kujiunga na Miami, Suarez pia alikuwa akichukua Dola 200,000 kwa mwezi Gremio.
Mbali ya mshahara wake, Suarez amepata pesa kupitia kampuni mbalimbali zinazomlipa kwa kutangaza bidhaa zao.
Ana mkataba mnono na Puma, pia ni balozi wa Beats Abitab, Antel, Cablevision, Garnier, Pepsi, na Samsung na zote kwa pamoja zinampa zaidi ya Dola 10 milioni kwa mwaka.

MSAADA KWA JAMII
Kwa nyakati tofauti, Suarez ameshiriki na kusaidia kuandaa mechi za hisani (charity matches) zenye lengo la kukusanya fedha kwa ajili ya kusaidia watu walioathirika na majanga ya asili, wagonjwa na watoto yatima.
Mechi hizo zimehusisha wachezaji wakubwa kutoka Amerika Kusini na Ulaya, na zimekusanya mamilioni ya pesa kusaidia miradi mbalimbali ya kijamii.
Amewahi pia kununua zaidi ya vifungashio 1000 vya chakula kwa ajili ya kusaidia watoto wasiojiweza huko Uruguay na amekuwa akicheza mechi mbalimbali za kirafiki zenye lengo la kukusanya pesa kwa ajili ya kusaidia watu mbalimbali wasiojiweza.

MJENGO
Nyumba yake yenye thamani zaidi ipo huko Florida Marekani ambayo ina thamani ya Dola 11 milioni aliyoinunua mwaka 2023, mbali ya hiyo pia ana nyuma nyingine huko Castelldefels, Catalonia, ambayo aliinunua kwa Dola 3.6 milioni mwaka 2018.
Anamiliki pia mijengo huko Montevideo na Salto nchini kwa Uruguay ambazo zote zina thamani ya Dola 1.5 milioni.

MAISHA NA BATA
Yupo kwenye ndoa na Sofia Balbi ambaye ni mchumba wake wa utotoni, wawili hawa walioana mwaka 2009 na hadi sasa wamefanikiwa kupata watoto watatu na mkubwa zaidi ni Benjamin Suarez ambaye anaonekana kufuata nyayo za baba yake na kwa sasa anacheza timu za vijana za Inter Miami na yupo pamoja na mtoto wa Messi.