Staa tenisi apoteza mke, kazi
Muktasari:
- Monfils, mwenye umri wa miaka 40, na Svitolina walikuwa katika uhusiano wa kimapenzi tangu 2018 na walioana miaka mitatu baadaye, ambapo wana mtoto wa kike mwenye umri wa miaka minne, ambaye Svitolina amesisitiza kuwa ataendelea kuwa kipaumbele chao kikuu wanapopitia kipindi hiki cha kutengana.
LYON, UFARANSA: SIKU moja baada ya mkewe, nyota wa tenisi duniani, Elina Svitolina, kutangaza kuachana na mumewe Gael Monfils ambaye ni mchezaji wa mchezo huo, mume ametangaza kustaafu.
Monfils amethibitisha ghafla kumaliza maisha yake ya tenisi akisema mchezo huo 'umepoteza maana yake yote' kufuatia uamuzi wa Elina kuvunja ndoa yao. Svitolina, mwenye umri wa miaka 32, alitangaza Jumatatu kwamba ametengana na nyota huyo mwenzake wa tenisi akieleza kuwa vita vya Urusi na Ukraine vimeathiri sana afya yake ya akili.
Monfils, mwenye umri wa miaka 40, na Svitolina walikuwa katika uhusiano wa kimapenzi tangu 2018 na walioana miaka mitatu baadaye, ambapo wana mtoto wa kike mwenye umri wa miaka minne, ambaye Svitolina amesisitiza kuwa ataendelea kuwa kipaumbele chao kikuu wanapopitia kipindi hiki cha kutengana.
Kwa mujibu wa gazeti la L'Équipe, kuvunjika kwa ndoa hiyo kulimfanya Monfils kuharakisha uamuzi wake wa kustaafu tenisi.
Gazeti hilo la Ufaransa limeeleza kuwa habari hizo 'zilimpiga kama mzigo mkubwa wa matofali', na kwamba tenisi 'ilipoteza maana yake yote kutokana na hali hiyo', likisisitiza kwamba Monfils aliamua kuwa 'hakuwa tena na uwezo wa kucheza'.
Mashabiki wa tenisi walishangaa wiki iliyopita walipoona jina la Monfils likiorodheshwa kuwa atakuwa katika orodha ya wachezaji wastaafu inayosimamiwa na Shirika la Kimataifa la Uadilifu wa Tenisi (ITIA). Kuwekwa kwake katika orodha hiyo kunamaanisha kuwa haruhusiwi tena kushiriki mashindano ya kitaalamu.
Oktoba mwaka jana, Monfils alitangaza kuwa alipanga kustaafu mwishoni mwa msimu wa 2026. Mashindano ya Paris Masters yanayotarajiwa kufanyika mwanzoni mwa Novemba yalionekana kuwa nafasi yake ya mwisho ya kuaga mashabiki wake wa nyumbani. Pia alikuwa amepewa nafasi maalumu ya kushiriki mashindano ya Grand Prix Auvergne-Rhône-Alpes yanayohusisha wachezaji wa kiwango cha ATP 250 yaliyokuwa yakifanyika Lyon wiki hii.
Waandaaji walithibitisha mapema mwezi huu kuwa Monfils amejiondoa kwa 'sababu binafsi', huku Lucas Pouille akichukua nafasi yake.
Maisha ya Monfils katika tenisi yalifikia mwisho rasmi kwenye mashindano ya US Open mwezi Septemba, alipofungwa katika raundi ya pili na Learner Tien.