Zaiylissa kisa dulla makabila, aitetea ndoa yake
Muktasari:
- Zaiylissa na Dulla walifunga ndoa Mei 2023, lakini walitengana Julai mwaka huo huo. Baadaye, Januari 24, 2024, mwigizaji huyo alifunga ndoa na aliyekuwa Ofisa Habari wa Simba na Yanga, Haji Manara. Hata hivyo, ndoa hiyo nayo ilifikia mwisho Aprili 9, 2025.
NI kama ukurasa mpya umefunguliwa katika simulizi la Zaiylissa na Dulla Makabila! Baada ya ndoa yao kuvunjika na kila mmoja kuendelea na maisha yake, sasa wawili hao wamekutana tena katika muziki, jambo lililoibua maswali kwa mashabiki waliokuwa wakifuatilia historia yao.
Zaiylissa na Dulla walifunga ndoa Mei 2023, lakini walitengana Julai mwaka huo huo. Baadaye, Januari 24, 2024, mwigizaji huyo alifunga ndoa na aliyekuwa Ofisa Habari wa Simba na Yanga, Haji Manara. Hata hivyo, ndoa hiyo nayo ilifikia mwisho Aprili 9, 2025.
Baada ya ndoa hiyo kuvunjika, Zaiylissa aliendelea na maisha yake binafsi na Februari 2026 akafunga ndoa na Said, ambaye alikuwa mchumba wake wa muda mrefu.
Sasa, akiwa katika ndoa hiyo mpya, Zaiylissa amekutana tena na Dulla katika wimbo Mapenzi Yasakwe na ameshiriki katika video yake. Ushirikiano huo umeibua gumzo kutokana na historia yao ya kimapenzi, huku baadhi ya mashabiki wakijiuliza wamewezaje kufanya kazi pamoja baada ya yaliyopita.
Kilichoongeza udadisi ni maelezo ya Zaiylissa, ndoa yake ya sasa bado ipo na mume wake ameridhia ushiriki wake katika video hiyo. Amesema pia Dulla aliomba ruhusa kwa mume wake kabla ya yeye kushiriki katika kazi hiyo.
Lakini baada ya yaliyopita, wawili hao wamefikiaje hatua ya kufanya kazi pamoja? Zaiylissa alipokeaje ombi la Dulla, na anasemaje kuhusu ndoa yake ya sasa? Haya ni mazungumzo ya Dakika 5 Na... na Zaiylissa.
Mwanaspoti: Baada ya wewe na Dulla kuachana, sasa mmeungana tena kupitia wimbo Mapenzi Yasakwe. Nini kimebadilika hadi mkakubali kufanya kazi pamoja?
Zaiylissa: Kwanza, ninaamini maisha yanaendelea na kila mtu ana nafasi ya kufanya kazi na watu mbalimbali. Mimi na Dulla tuna historia yetu, lakini hilo halimaanishi hatuwezi kufanya kazi pamoja. Kwa upande wangu, nililitazama suala hili kama kazi ya sanaa na fursa ya kuendelea na shughuli zangu.
Mwanaspoti: Ulipopata ombi la kushiriki kwenye wimbo huo, ulilipokeaje? Kwa kuzingatia historia yenu, ulikuwa uamuzi rahisi au kulikuwa na changamoto ulizopaswa kuzifikiria?
Zaiylissa: Ni jambo ambalo nilipaswa kulitazama kwa umakini kwa sababu tunajulikana na watu wengi, na historia yetu haiwezi kufutika. Hata hivyo, nilitakiwa kutenganisha yaliyopita na kazi inayotakiwa kufanyika sasa. Jambo muhimu lilikuwa kuhakikisha kwamba ninaelewa ninachokifanya na kwamba hakileti mkanganyiko katika maisha yangu ya sasa.
Mwanaspoti: Umesema mume wako wa sasa aliridhia ushiriki wako kwenye video hiyo. Ulipomweleza unakwenda kufanya kazi na aliyekuwa mume wako, alikupa majibu gani?
Zaiylissa: Mume wangu anaelewa kazi yangu na anajua sanaa inahitaji kushirikiana na watu mbalimbali. Kwa hiyo, nilipomweleza kuhusu kazi hiyo, aliielewa. Kwangu, jambo la msingi ni kuwa na mawasiliano mazuri ndani ya ndoa na kuhakikisha kwamba kila mmoja anaelewa mazingira ya mwenzake.
Mwanaspoti: Dulla ndiye aliyeomba ruhusa kwa mume wako ili ushiriki kwenye video. Ulipata hisia gani ulipojua amechukua hatua hiyo?
Zaiylissa: Nililiona hilo kama jambo linalohitaji maelewano na heshima kati ya watu wanaohusika. Kwa sababu nina ndoa yangu ya sasa, ni muhimu mambo yanayoweza kuibua maswali yazungumzwe kwa uwazi. Kilichokuwa muhimu ni kuhakikisha kazi inafanyika kwa kuelewana na kila mtu anajua nafasi yake.
Mwanaspoti: Kuna kipindi uliweka msimamo wa kutotaka Dulla akuzungumzie kwenye mitandao ya kijamii. Sasa mnafanya kazi pamoja. Ni nini kimebadilika katika mawasiliano yenu?
Zaiylissa: Kila jambo lina wakati wake na mazingira yake. Kutokubaliana katika kipindi fulani hakumaanishi kwamba watu hawawezi kufanya kazi pamoja baadaye. Mimi naamini ni muhimu kuheshimu maisha ya kila mmoja na kutenganisha mambo binafsi na shughuli za kikazi. Hata tunaposhirikiana, bado kila mmoja ana maisha yake anayopaswa kuyaheshimu.
Mwanaspoti: Jina la wimbo Mapenzi Yasakwe linaweza kuwafanya mashabiki kuhusisha ujumbe wake na historia yenu. Je, wimbo huu una simulizi la kisanii pekee au kuna sehemu inayotokana na uzoefu wako wa maisha?
Zaiylissa: Watu wanaweza kuutafsiri wimbo kwa namna tofauti, hasa wanapojua historia ya wasanii wanaohusika. Lakini ningependa watu waangalie pia kazi yenyewe na ujumbe unaowasilishwa. Si kila kazi ninayofanya na msanii mwingine inamaanisha kwamba tunazungumzia maisha yetu binafsi.
Mwanaspoti: Umesisitiza ndoa yako ya sasa bado ipo na mume wako anaelewa mazingira ya kazi yako. Ungependa watu waelewe nini kuhusu ndoa yako na namna unavyoweza kufanya kazi na mtu uliyewahi kuwa naye kwenye ndoa?
Zaiylissa: Ningependa watu waelewe kwamba ndoa yangu ipo na ushiriki wangu kwenye kazi hii haumaanishi kuna tatizo katika ndoa yangu. Mume wangu anaelewa kazi ninayofanya na ananipa nafasi ya kujishughulisha na mambo mbalimbali ya maendeleo. Muhimu ni kuaminiana, kuheshimiana na kuelewa kazi ni sehemu ya maisha yangu.
Mwanaspoti: Baada ya kuonekana tena na Dulla kwenye kazi hii, baadhi ya mashabiki wanaweza kujiuliza kama mnaweza kurudiana kimapenzi. Ungependa kuwaambia nini kuhusu uhusiano wenu wa sasa, na je, uko tayari kufanya naye kazi nyingine?
Zaiylissa: Ningewaomba watu wasihitimishe mambo kwa kuangalia video pekee. Kufanya kazi pamoja hakumaanishi kwamba watu wamerudiana kimapenzi. Kwa sasa, nina maisha yangu na ndoa yangu, na ninaheshimu hilo. Kuhusu kufanya kazi nyingine, hilo litategemea aina ya kazi, mazingira yake na makubaliano yatakayokuwepo.