Nyota tenisi asimamisha mechi kulalamikia bangi
Muktasari:
- Uwanja huo ni wa pili kwa ukubwa kati ya viwanja vikubwa vya mashindano hayo nchini Marekani, lakini licha ya hadhi yake, Sabalenka alisumbuliwa na harufu aliyodhani ni ya bangi kiasi kwamba akiwa katika mchezo wa tatu wa seti ya kwanza, alimuomba mwamuzi Eva Asderaki-Moore aangalie suala hilo baada ya kwanza kuzungumza na timu yake.
NEW YORK, MAREKANI; NYOTA maarufu wa tenisi na namba moja kwa ubora duniani, Aryna Sabalenka amelazimika kusimamishwa kwa muda mchezo wake wa raundi ya tatu dhidi ya Kamila Rakhimova baada ya kulalamika kwamba kuna mtu alikuwa akivuta bangi ndani ya Uwanja wa Louis Armstrong kwenye mashindano ya US Open.
Uwanja huo ni wa pili kwa ukubwa kati ya viwanja vikubwa vya mashindano hayo nchini Marekani, lakini licha ya hadhi yake, Sabalenka alisumbuliwa na harufu aliyodhani ni ya bangi kiasi kwamba akiwa katika mchezo wa tatu wa seti ya kwanza, alimuomba mwamuzi Eva Asderaki-Moore aangalie suala hilo baada ya kwanza kuzungumza na timu yake.
“Kuna mtu anavuta bangi,” alisema Sabalenka wakati akisubiri mchezo ukiwa 30-0 ili kuzungumza na Asderaki-Moore na kuongeza:
“Unaweza kuwafanya (wahudumu wa uwanja) washughulikie hilo? Harufu ni kali sana.”
Staa huyo ambaye ni namba moja duniani ambaye baadaye alishinda mchezo huo kwa seti mbili mfululizo, alikuwa akicheza kutokea upande wa kusini mwa uwanja karibu na sehemu ambayo timu ya wasaidizi wake ilikuwa imekaa katika eneo maalumu la wachezaji.
Mwamuzi huyo wa kiti aliwasiliana haraka kwa redio kuomba msaada, huku akitoa ishara kwa mkono kwa wenzake. Baada ya hapo, wafanyakazi wa US Open waliingia kwenye umati wa mashabiki wakijaribu kubaini chanzo cha harufu hiyo.
Harufu ya bangi siyo jambo la kushangaza sana kuzunguka eneo la Billie Jean King National Tennis Center ulipo uwanja huo kutokana na kuwa ndani ya eneo kubwa la mapumziko ya umma, ambako watu wanaruhusiwa kisheria kuvuta bangi wanapokuwa wakipumzika kwenye maeneo ya wazi. Hata hivyo, kuvuta bangi pamoja na aina zote za uvutaji wa sigara ni marufuku ndani ya eneo la mashindano hayo. US Open imeombwa kutoa maelezo kuhusu tukio hilo.
Wakati wa hatua za kufuzu na kabla ya mashindano kuanza, wachezaji kadhaa kutoka Uingereza walielezea harufu hiyo ya kipekee inayopatikana katika eneo hilo kuwa inawatesa na mmojawao, Katie Boulter alionekana kutoridhishwa zaidi na harufu hiyo akisema imekuwapo muda mrefu.
“Nimewahi kukutana nayo. Ukienda kwenye viwanja vya mazoezi na vile vilivyo ndani ya bustani, unaisikia harufu hiyo sana,” alisema Boulter, ambaye alitolewa Jumatano iliyopita na Karolina Muchova.
“Mimi si shabiki mkubwa wa bangi. Najua wachezaji wengi wamekuwa wakilalamika kuhusu baadhi ya viwanja. Nimewahi kucheza Uwanja wa 17 na niliisikia harufu hiyo wakati wa mchezo wangu. Ni jambo ambalo sipendi kulisikia katikati ya mchezo wangu.”
Kuhusu suala hilo, Chama cha Tenisi cha Marekani (USTA) kilitoa taarifa kikisema: “Ingawa hatuwezi kudhibiti kile kinachotokea nje ya eneo la uwanja, tunaendelea kuwa makini katika kuhakikisha eneo hili linaendelea kuwa sehemu isiyoruhusu uvutaji wa sigara. Hii inahusisha utekelezaji wa sheria na kanuni, na timu zetu za usalama pamoja na huduma kwa wageni pale zinapofahamishwa kwamba kuna mtu anayevuta sigara. “Tunawafahamisha kwamba ingawa uvutaji unaweza kuwa halali katika Jimbo la New York, hairuhusiwi katika maeneo ya bustani ikiwemo kituo hiki cha tenisi. Tunaendelea kushirikiana na taasisi za serikali na tunaamini hatua zimepunguza uvutaji wa sigara karibu na uzio wa eneo letu.”
Sabalenka alimshinda kwa urahisi Rakhimova, anayeshika nafasi ya 92 duniani, na kuendelea na safari yake ya ushindi wa seti mbili mfululizo kuelekea kile anachotarajia kuwa taji lake la tatu mfululizo la US Open.
Akizungumzia tukio hilo baadaye huku akitabasamu, Sabalenka alisema: “Nilikuwa kama, jamani, mnaweza kufanya chochote, mnaweza kuvuta chochote, mnaweza kupumzika kwa namna yoyote mnayotaka, lakini tafadhali msifanye hivyo wakati wa mchezo wa tenisi. Ni vigumu kidogo kuvumilia harufu hiyo wakati unapojaribu kushindana kwa kiwango chako cha juu.
“Lakini jamani, nafikiri hakuna mengi zaidi ya kusema kuhusu bangi. Naomba tu watu wasiitupe karibu na uwanja wa tenisi,” alisema, kabla ya kuongeza kwa mzaha kuhusu mchezo wake: “Labda mchezo wangu ni wa kasi sana kwao, ndiyo maana wanataka kuupunguza!”
Licha ya usumbufu huo wa mapema, Sabalenka alirejea kwenye mchezo bila matatizo makubwa na kuendelea kuutawala seti ya kwanza.
Seti ya pili ilikuwa tofauti kwani ilidumu karibu mara mbili ya muda wa seti ya kwanza, huku Rakhimova akizoea mchezo na kumpa ushindani Sabalenka tangu mwanzo akimlazimisha kucheza hadi sare ya pointi (deuce) mara nne katika mchezo wake wa kwanza.
WAKONGWE NJE
Katika hatua nyingine, wakongwe wa tenisi, Serena na Venus Williams walitolewa katika raundi ya kwanza ya mashindano ya wanawake ya wawili wawili kwenye mashindano hayo, baada ya kupoteza uongozi wa pointi 5-0 katika ‘tie-break’ ya pointi 10 iliyoamua mshindi.
Dada hao mashuhuri walipokea mwaliko maalumu wa kushiriki michuano dakika za mwisho, baada ya awali kuungana katika Cincinnati Open msimu huu kufuatia kurejea kwa Serena kwenye mashindano.
Serena, bingwa wa mataji 23 ya Grand Slam kwa upande wa wanawake, alikuwa amejiondoa kwenye mashindano miaka minne iliyopita, wakati alicheza kile ambacho mashabiki wengi wa tenisi waliamini kingekuwa mchezo wake wa mwisho katika Uwanja wa Arthur Ashe wa US Open.
Mapema msimu huu, Serena alipokea mwaliko maalumu wa kushiriki michuano ya Wimbledon, lakini mambo yaligeuka baada ya kufungwa kwa seti tatu katika mchezo mkali na Joint, ambaye alikutana naye tena mjini New York. Miezi miwili baadaye, Serena alishindwa kulipiza kisasi dhidi ya Muaustralia huyo anayeshika nafasi ya 72 duniani. Joint sasa ana rekodi ya ushindi wa 2-0 dhidi ya bingwa huyo mara nyingi, baada ya Serena na Venus kufungwa kwa seti 6-3, 6-7(6), 6-7(7).
Kinadada hao wa Williams walipokewa kishujaa walipoingia uwanjani kuanza mechi, huku uwanja ukiwa umejaa mashabiki waliokuwa na hamu ya kuwaona tena ndugu hao wababe wa tenisi wakicheza kwenye Arthur Ashe kwa mara ya kwanza tangu 2022.