Wawili kuiwakilisha Tanzania ITF Junior Series
Muktasari:
- Mashindano hayo yanatarajiwa kuanza Septemba 23 hadi Oktoba 2, 2026, huku Tanzania ikilenga kutumia mashindano hayo kupata matokeo mazuri pamoja na kuwajengea uwezo, ushindani na uzoefu wa kimataifa kwa nyota hao.
TIMU ya Taifa ya Tenisi kwa kutumia kiti mwendo imewaandaa wachezaji wawili, Tamela Kinaweda na Aidan Selestine, kuiwakilisha Tanzania katika mashindano ya ITF Junior Series chini ya umri wa miaka 18 yatakayofanyika Afrika Kusini.
Mashindano hayo yanatarajiwa kuanza Septemba 23 hadi Oktoba 2, 2026, huku Tanzania ikilenga kutumia mashindano hayo kupata matokeo mazuri pamoja na kuwajengea uwezo, ushindani na uzoefu wa kimataifa kwa nyota hao.
Kocha wa timu hiyo, Riziki Salum, amesema maandalizi ya wachezaji hao yamefanyika kwa kuzingatia ushindani wa mashindano hayo, akiamini kiwango walichokifikia kinaweza kuwasaidia kufanya vizuri dhidi ya wapinzani wao kutoka mataifa mbalimbali.
“Vijana tumewaanda vizuri, Mazoezi tuliyowapa tunaamini wana uwezo wa kufanya vizuri kwani ni mashindano yanayoangalia vwango ili mchezaji achaguliwe lazima awe amepifikia kiwango fulani,” amesema Salum.
Salum amesema Aidan tayari ana uzoefu wa mashindano hayo baada ya kushiriki mwaka jana nchini Afrika Kusini, ambako alimaliza akiwa nafasi ya tano barani Afrika na kushika nafasi ya 40 duniani.
“Alishiriki mwaka jana Afrika Kusini na mwaka huu ameenda tena. Mwaka jana alikuwa nafasi ya tano Afrika na namba 40 duniani,” alisema Salum.
Kwa upande wake, Aidan aliongeza kuwa anaingia kwenye mashindano hayo akiwa na lengo la kuboresha matokeo aliyoyapata kwenye mashindano yaliyopita.
“Malengo yangu ni kufanya vizuri zaidi ya mashindano yaliyopita ya ITF Junior Series,” amesema Aidan.
Salum pia ametoa wito kwa wadau kuendelea kuunga mkono maendeleo ya tenisi kwa kutumia kiti mwendo, akisema sapoti hiyo ni muhimu katika kuwasaidia vijana kupata nafasi zaidi za kushiriki mashindano ya kimataifa na kuendeleza vipaji vyao.