Dili la Nabi Wydad mambo safi
Muktasari:
- Taarifa za ndani zililiambia Mwanaspoti kuwa, kuna uwezekano wa kocha huyo raia wa Tunisia ambaye aliwahi kufanya vizuri akiwa yanga, kutua Wydad ni mkubwa huku pande zinazohusika zikikamilisha mazungumzo ya mwisho kuhusu uteuzi wake na mambo yanayohusu benchi la ufundi.
NASREDDINE Nabi yupo mlangoni kujiunga na Wydad Athletic Club ya Morocco, huku mazungumzo ya kumkabidhi timu hiyo yakielezwa kufikia hatua za mwisho, baada ya uongozi wa klabu hiyo kuamua kuharakisha mpango uliokuwa umepangwa kutekelezwa Desemba, mwaka huu.
Taarifa za ndani zililiambia Mwanaspoti kuwa, kuna uwezekano wa kocha huyo raia wa Tunisia ambaye aliwahi kufanya vizuri akiwa yanga, kutua Wydad ni mkubwa huku pande zinazohusika zikikamilisha mazungumzo ya mwisho kuhusu uteuzi wake na mambo yanayohusu benchi la ufundi.
“Mpango wa awali ulikuwa Nabi ajiunge na Wydad Desemba, lakini kutokana na mwenendo wa timu chini ya kocha aliyepo, uongozi umeona hakuna sababu ya kuendelea kusubiri hadi wakati huo. Mazungumzo yamefika hatua za mwisho.”
“Nabi na Wydad wako kwenye mazungumzo ya kina, huku suala muhimu likiwa ni kumaliza mkataba wa kocha wa sasa, Paulo Sérgio. Lakini mazungumzo yamehusisha pia masharti ya mkataba wa Nabi na mapendekezo ya kikosi cha benchi la ufundi.
Wydad imekuwa na mwanzo usioridhisha katika ligi, ikikusanya pointi tano katika mechi nne za mwanzo, ikiwa na ushindi mmoja, sare mbili na kipigo kimoja. Sare ya bao 1-1 dhidi ya Amal Tiznit Oktoba 18, 2026 ilikuwa miongoni mwa matokeo yaliyoongeza maswali kuhusu mwenendo wa timu hiyo.
Nabi si mgeni katika soka la Morocco, kwani amewahi kufundisha AS FAR Rabat na Raja Casablanca. Akiwa AS FAR msimu wa 2023/24, aliiongoza timu hiyo kumaliza nafasi ya pili kwenye ligi na kufika fainali ya Kombe la Throne, huku akiwa na rekodi ya ushindi mechi 28, sare tano na vipigo vitano katika mechi 38.
Baadaye alijiunga na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini mwaka 2024, ambako alifundisha mechi 41 na kushida 18, sare tisa na vipigo 14. Pia aliiongoza klabu hiyo kutwaa Kombe la Nedbank mwaka 2025.
Nabi aliwahi pia kuandika historia akiwa Yanga, aliyoifundisha kuanzia Aprili 2021 hadi Juni 2023. Akiiongoza kwenye mechi 76 za Yanga, akipata ushindi 61, sare tisa na vipigo sita. Kipindi chake kilihusishwa na mafanikio ya ndani na mafanikio ya timu hiyo katika mashindano ya CAF, jambo lililomfanya aendelee kukumbukwa na mashabiki wa Jangwani mpaka leo.