Son Heung-min aingia anga za Wasaudia

Muktasari:
- Inaelezwa mabosi wa Tottenham wapo tayari kumuuza nyota huyo wa kimataifa wa Korea mwenye umri wa miaka 32, kwa lengo la kupata pesa za kufanyia usajili.
STRAIKA wa Tottenham Hotspur, Son Heung-min anawindwa na timu kibao za Saudi Arabia katika dirisha hili.
Inaelezwa mabosi wa Tottenham wapo tayari kumuuza nyota huyo wa kimataifa wa Korea mwenye umri wa miaka 32, kwa lengo la kupata pesa za kufanyia usajili.
Son ambaye alijiunga na Spurs akitokea Bayer Leverkusen 2015 anaripotiwa kumezewa mate na timu za Saudia ambazo zinaamini zikimpata zitapanua wigo wa kufuatiliwa Asia.
Kuna uwezekano mkubwa Spurs ikafikia uamuzi wa kumuuza kwa sababu amebakisha mkataba wa mwaka mmoja na timu zinazomhitaji ikiwemo Al-Hilal zipo tayari kutoa Pauni 70 milioni.
Bryan Mbeumo
MMSHAMBULIAJI wa Brentford na Cameroon, Bryan Mbeumo, mwenye umri wa miaka 25, anatarajiwa kupokea mshahara wa Pauni 250,000 kwa wiki akiwa na Manchester United anayotarajiwa kukamilisha usajili hivi karibuni. Mshahara huo unatarajiwa kuwa ni mara tano ya mshahara wake wa sasa anaoupokea akiwa na Brentford.
Martin Zubimendi
KIUNGO wa kati wa Real Sociedad, Martin Zubimendi, mwenye umri wa miaka 26, ameweka wazi kwamba hana uhakika ikiwa atajiunga na Arsenal katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi au la, kwa sababu hakuna kilichoamuliwa hadi sasa. Zubimendi ambaye ni miongoni mwa wachezaji waliotajwa kuhitajika na Arsenal tangu dirisha lililopita, mkataba wake unamalizika 2027.
Mike Maignan
CHELSEA imefanya mawasiliano na AC Milan kuhusu uwezekano wa kumsajili kipa wa timu hiyo na Ufaransa, Mike Maignan, 29, ambaye amebakiza mwaka mmoja katika mkataba. Benchi la ufundi la Chelsea linatafuta kipa mwingine baada ya kutoridhishwa na kiwango alichoonyesha Robert Sanchez katika msimu uliopita.
Aaron Ramsdale
WAWAKILISHI wa kipa wa Southampton, Aaron Ramsdale, wamefanya mazungumzo kuhusu kujiunga na West Ham United akitokea Southampton katika dirisha hili. Taarifa zinadai Ramsdale anaweza kuuzwa kwa kiasi kisichopungua Pauni 20 milioni. Kipa huyo anataka kuachana na Southampton baada ya timu hiyo kushuka daraja.
Luka Modric
KIUNGO wa kati wa Real Madrid na Croatia, Luka Modric, 39, amefanya makubaliano kwa njia ya mazungumzo na AC Milan na anaweza akajiunga katika dirisha hili la majira ya kiangazi baada ya kumalizika kwa michuano ya Kombe la Dunia la klabu la Fifa. Modric alitangaza kuwa ataondoka Real Madrid mwisho wa msimu ikiwa ni baada ya kuichezea timu hiyo kwa mafanikio makubwa.
Ferran Torres
ASTON Villa imeanza mazungumzo kwa ajili ya kumsajili mshambuliaji wa Barcelona na timu ya taifa ya Hispania, Ferran Torres, mwenye umri wa miaka 25, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Taarifa zinaeleza kwamba Aston Villa ipo tayari kutoa kiasi kisichopungua Pauni 42 milioni. Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika 2027.
Jordan Henderson
KIUNGO wa kimataifa wa England, Jordan Henderson, 34, ameendelea kufanya mazungumzo na Sunderland anayoweza kujiunga nayo katika dirisha hili. Sunderland ambayo imepanda daraja msimu huu, imevutiwa sana na Henderson na inaamini ikimpata ataongeza kitu katika chumba cha kubadilishia nguo kutokana na uzoefu wake.