Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Soko la mdaka mishale!

MISHALE Pict

Muktasari:

  • Kipa huyo Mtaliano ameambiwa na kocha wa PSG, Luis Enrique kwamba hana maisha kwenye kikosi hicho na hivyo kumfanya kutuma ujumbe wa kuaga na kuposti kwenye ukurasa wake wa Instagram.

PARIS, UFARANSA: KIPA wa boli, Gianluigi Donnarumma ameziweka klabu za Ligi Kuu England kwenye hatari ya kuanzisha vita kali baada ya kutangaza anaachana na Paris Saint-Germain.

Kipa huyo Mtaliano ameambiwa na kocha wa PSG, Luis Enrique kwamba hana maisha kwenye kikosi hicho na hivyo kumfanya kutuma ujumbe wa kuaga na kuposti kwenye ukurasa wake wa Instagram.

“Bahati mbaya, kuna mtu ameamua kwamba sitaendelea kuwa sehemu ya kundi hili na kutoa mchango wangu katika kuifanya timu kufanikiwa,” alisema na kuongeza. “Nimehuzunika na nimevunjika moyo.”

Mapema Jumanne, kocha Enrique alisema kwamba kipa Donnarumma ameondoshwa kwenye kikosi cha PSG kilichotarajia kumenyana na Tottenham Hotspur kwenye mechi ya Super Cup usiku wa jana Jumatano, aliposema:  “Donnarumma yupo nje ya kikosi baada ya kufanya uamuzi wangu. Nahusika kwa hilo kwa asilimia 100.”

“Nataka aina nyingine ya kipa hivyo nimefanya uamuzi. Gigio ni mmoja wa makipa bora duniani. Katika maisha ya soka, kama inavyotokea kwa makocha wote, haukua uamuzi rahisi kabisa, lakini nawajibika kwa yote.”

Donnarumma umri wake ni miaka 26 na alibeba ubingwa wa Euro alipokuwa na kikosi cha Italia mwaka 2021 na alibeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya na miamba hiyo ya PSG, Mei mwaka huu, hivyo timu nyingi tu zitataka kumsajili.

Na bado kuna muda wa kutosha hadi hapo dirisha hili la usajili la majira ya kiangazi litakapofungwa Septemba 1, lakini swali lililopo ni wapi atakwenda kipa huyo? Hizi hapa timu tatu za Ligi Kuu England zinazoweza kumnasa kipa huyo.


  1. Manchester City

Huko Etihad kumeripotiwa kuwapo na pilikapilika zinazohusu makipa, huku kocha Pep Guardiola akiripotiwa kuvutiwa na huduma ya Donnarumma.

Kwenye dirisha hili, Man City imemsajili kipa James Trafford kwa ada ya Pauni 31 akitokea Burnley. Lakini, kinachoelezwa, kipa Ederson naye yupo njiani kwenda Galatasaray, hivyo dili hilo likitokea, huenda miamba hiyo ya Etihad ikatua kwa Donnarumma kunasa saini yake baada ya kuelezwa kwamba makubaliano binafsi tayari yameshafikiwa na sasa kilichobaki ni ada yake tu.

PSG imeamua kumweka kando Donnarumma baada ya kumsajili kipa mwingine, Lucas Chevalier, ambaye alitarajia kuwapo golini usiku wa jana Jumatano.


2. Manchester United

Kuna maswali mengi kuhusu kiwango cha kipa Andre Onana tangu alipotua Man United akitokea Ajax, ambapo vitu vilikuwa vibaya sana msimu uliopita.

Kuna nyakati kocha Ruben Amorim alilazimika kumwondoa Onana golini na kumpa nafasi Altay Bayindir.

Mwanzoni mwa dirisha hili la majira ya kiangazi, Man United ilifanya mawasiliano na Aston Villa kuulizia upatikanaji wa kipa Emi Martinez na ilikuwa ikihusishwa pia na Senne Lammens wa Royal Antwerp.

Lakini, kipa Donnarumma siku zote amekuwa akiongoza na mipango mikubwa na kitendo cha Man United kushindwa kucheza michuano ya Ulaya kwa kumaliza nafasi ya 15 msimu uliopita, linaweza kuwafanya kukosa saini ya kipa huyo Mtaliano.

Kinachoelezwa PSG imeshindwana na Donnarumma baada ya kutaka mshahara mkubwa, wakati huo Man United yenyewe inaondoa kundi kubwa la wachezaji wanaolipwa mshahara mkubwa.


3. Chelsea

Kipa Robert Sanchez hajawahi kuonyesha ushawishi mkubwa huko Chelsea na ndio maana miamba hiyo ya Stamford Bridge imefanya jaribio la kumsajili Mike Maignan mapema kwenye dirisha hili.

Chelsea imemuuza Djordje Petrovic kwenda Bournemouth kwa Pauni 25 milioni na Kepa Arrizabalaga kwenda Arsenal kwa Pauni 5 milioni, huku ikimruhusu Marcus Bettinelli kwenda Man City.

Bado ina makipa Filip Jorgensen na Mike Penders kwenye kikosi, huku mmoja akipelekwa kwa mkopo Strasbourg.

Chelsea bado haijafuta mpango wake kwa kipa Maignan. Lakini, kuwapo na nafasi ya kumsajili Donnarumma, kunaweza kuwafanya Chelsea kuwahi haraka ili kumbadili Sanchez mwenye makosa mengi golini.