Slavko Vinčić kuamua Hispania vs Argentina
Muktasari:
- Vinčić, mwenye umri wa miaka 46, amepewa jukumu la kuamua hatima ya ubingwa katika mchezo huo mkubwa utakaochezwa Julai 19, 2026 kwenye Uwanja wa MetLife, New Jersey, Marekani.
ATLANTA, MAREKANI: SHIRIKISHO la Soka la Kimataifa (FIFA) limemtangaza mwamuzi wa kimataifa kutoka Slovenia, Slavko Vinčić, kuwa msimamizi wa mchezo wa fainali ya Kombe la Dunia 2026 utakaowakutanisha mabingwa watetezi Argentina na Hispania.
Vinčić, mwenye umri wa miaka 46, amepewa jukumu la kuamua hatima ya ubingwa katika mchezo huo mkubwa utakaochezwa Julai 19, 2026 kwenye Uwanja wa MetLife, New Jersey, Marekani.
Mwamuzi huyo wa Slovenia ni miongoni mwa waamuzi wenye uzoefu mkubwa katika mashindano ya kimataifa, akiwa amewahi kuchezesha michezo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya pamoja na Kombe la Dunia la 2022.
Fainali hiyo itakayopigwa Jumapili ijayo itawakutanisha Argentina, inayotetea ubingwa wake, dhidi ya Hispania ambayo imeonyesha kiwango bora katika michuano ya mwaka huu na kufuzu hatua hiyo baada ya kuiondoa Ufaransa katika nusu fainali, huku Argentina ikiitoa England.
Vincic atasaidiwa na waamuzi wenzake kutoka Slovenia, Tomaz Klancnik na Andraz Kovacic, huku wakiiandikia historia nchi yao kwa kuwa timu ya kwanza ya waamuzi kutoka Slovenia kusimamia fainali ya Kombe la Dunia.
Akizungumza baada ya kupokea taarifa hiyo, Vincic amesema alishindwa kuzuia hisia zake kutokana na furaha kubwa aliyokuwa nayo.
"Mwanzoni nilishtuka, halafu nikajawa na furaha. Nilikuwa natetemeka. Ni heshima kubwa sana kupewa fainali ya Kombe la Dunia. Hii ni ndoto ya kila mwamuzi tangu anapoanza kazi hii," amesema Vincic.
Ameongeza kuwa anajivunia kuiwakilisha Slovenia katika tukio kubwa zaidi la michezo duniani na kuahidi yeye pamoja na timu yake kufanya kazi kwa weledi mkubwa.
Mwamuzi huyo mwenye umri wa miaka 46 si mgeni kwenye mechi kubwa barani Ulaya. Mwaka 2024 alichezesha fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kati ya Real Madrid na Borussia Dortmund iliyofanyika Wembley, huku mwaka 2022 akisimamia pia fainali ya Europa League kati ya Rangers na Eintracht Frankfurt.
Vincic pia amekuwa mwamuzi katika michuano miwili ya Euro, ikiwemo Euro 2024 ambapo alisimamia ushindi wa Hispania dhidi ya Ufaransa katika hatua ya nusu fainali kabla ya Hispania kutwaa ubingwa.
Katika Kombe la Dunia, alichezesha mechi yake ya kwanza nchini Qatar mwaka 2022, ambapo Argentina ilipata mshtuko wa kufungwa 2-1 na Saudi Arabia katika mchezo wa ufunguzi wa kundi. Hata hivyo, Argentina ilijikomboa na baadaye kutwaa ubingwa wa dunia.
Fainali ya Jumapili itakuwa mechi ya sita ya Kombe la Dunia kwa Vincic katika maisha yake ya uamuzi, na ya nne katika kampeni ya mwaka 2026, baada ya kuanza kwa kusimamia sare ya mabao 1-1 kati ya Brazil na Morocco hatua ya makundi.
Sasa macho yote yataelekezwa kwa mwamuzi huyo wa Slovenia atakapokuwa katikati ya uwanja kusimamia pambano kubwa litakalowakutanisha mabingwa wa Ulaya, Hispania, dhidi ya mabingwa watetezi wa dunia, Argentina.