Argentina yatembeza viatu, England yalia
Muktasari:
- Wachezaji wa Argentina walitumia nguvu nyingi kuzuia kasi ya England, hasa dhidi ya nyota kama Jude Bellingham na Elliot Anderson, ambao walikuwa wakisumbua safu yao ya ulinzi na kiungo.
ATLANTA, MAREKANI: KIPIGO cha England kutoka kwa Argentina katika nusu fainali ya Kombe la Dunia kilikuwa mchezo kilichangiwa na mabingwa hao watetezi kufanya faulo kwa wastani wa kila baada ya dakika nne kwenye mchezo huo.
Wachezaji wa Argentina walitumia nguvu nyingi kuzuia kasi ya England, hasa dhidi ya nyota kama Jude Bellingham na Elliot Anderson, ambao walikuwa wakisumbua safu yao ya ulinzi na kiungo.
Licha ya mfululizo huo wa makosa, Argentina kwa kiasi kikubwa iliweza kuepuka kupewa kadi nyingi za njano katika kipindi hicho, jambo lililozua mjadala miongoni mwa mashabiki wa England waliodai kuwa baadhi ya faulo hizo zilistahili adhabu kali zaidi.
England nayo ilionyesha kuwa haikuwa tayari kubebwa, ikijibu kwa mikwaju migumu na ukakamavu wa kimchezo.
Baada ya hali ya joto kuongezeka kwa muda wote wa mchezo, mambo yalifikia kilele baada ya filimbi ya mwisho, ambapo Jude Bellingham na mchezaji wa akiba wa Argentina, Valentin Barco, walihusika katika mabishano makali wakati Argentina ikishangilia ushindi wake wa kutinga fainali.
Katika kipindi cha kwanza, Argentina ilikuwa ikikumbana mara kwa mara na uamuzi wa mwamuzi Ismail Elfath kutokana na faulo walizokuwa wakifanya dhidi ya England. Hata hivyo, kipindi cha pili walipunguza makosa hayo huku England ikijaribu kulinda bao lake la kuongoza lililofungwa na Anthony Gordon dakika ya 55.
Licha ya ushindani mkali, Argentina ilifanikiwa kugeuza matokeo na kushinda 2-1, lakini mchezo huo utaendelea kukumbukwa kwa mapambano, faulo nyingi na presha kubwa iliyokuwa ndani ya uwanja.
Mwanaspoti inaangalia kila faulo iliyofanywa na Argentina katika mchezo huo.
2- FAULO: Paredes dhidi ya Bellingham
Mchezo ulikuwa umeanza kwa kasi kubwa, lakini ndani ya dakika mbili tu Jude Bellingham alijinyakulia faulo baada ya kusukumwa na Leandro Paredes katikati ya uwanja.
Kiungo huyo wa Argentina alionekana kutaka kutuma ujumbe mapema kwa nyota huyo wa England kwamba angekabiliwa na mchezo wa nguvu na presha kubwa kwa dakika zote 90. Kitendo hicho kilionyesha wazi kuwa Argentina ilikuwa imepanga kuzuia ushawishi wa Bellingham kwa kutumia ukali wa kimchezo tangu mwanzo wa pambano.
3-FAULO: Enzo Fernandez dhidi ya Elliot Anderson
Dakika ya tatu ya mchezo ilishuhudiwa hali ya taharuki baada ya Elliot Anderson kumnyang'anya mpira Lionel Messi kwa mara ya kwanza, kabla ya kukwatuliwa kwa faulo na Enzo Fernandez katikati ya uwanja.
6- FAULO: Giuliano Simeone dhidi ya Elliot Anderson
Elliot Anderson aliendelea kuwa mwiba kwa Argentina baada ya kuonyesha uwezo mkubwa wa kuuchezea mpira upande wa kushoto, akimpita kwa ustadi Giuliano Simeone.
Baada ya kuzidiwa ujanja, Simeone hakuwa na njia nyingine zaidi ya kumkwatua Anderson, jambo lililomwangusha chini na kumlazimu mwamuzi kuipa England faulo iliyostahili. Tukio hilo lilionyesha jinsi Anderson alivyoanza kuwasumbua mabeki wa Argentina tangu dakika za mwanzo wa mchezo.
9- FAULO: Giuliano Simeone dhidi ya Elliot Anderson (Tena)
Dakika chache baadaye, Giuliano Simeone alimlenga tena Elliot Anderson kwa mchezo wa nguvu.
Mwamuzi Ismail Elfath hakusita kupuliza filimbi na kuipa England faulo, huku tukio hilo likionyesha wazi kuwa Anderson alikuwa amewekwa kwenye uangalizi maalum kutokana na uwezo wake wa kuvuruga mipango ya Argentina.
16- FAULO: Giuliano Simeone dhidi ya Anthony Gordon
Giuliano Simeone aliendelea kuonyesha mchezo wa mabavu baada ya kumkwatua Anthony Gordon alipokuwa ameupokea mpira karibu na mstari wa katikati ya uwanja.
Ilikuwa ni faulo nyingine iliyoonyesha mkakati wa Argentina wa kuvunja kasi ya mashambulizi ya wapinzani wao mapema kabisa.
24- FAULO: Giuliano Simeone dhidi ya Jordan Pickford
Kutoka kwenye mpira wa kona, Giuliano Simeone alimzuia kipa wa England, Jordan Pickford, kwa kumshika kwa nguvu kupita kiasi wakati akijaribu kuruka kuudaka mpira.
32' - FAULO: Enzo Fernandez dhidi ya Jude Bellingham
Jude Bellingham aliendelea kuwa mwiba kwa safu ya kiungo ya Argentina baada ya kuonyesha dribbling ya kiwango cha juu na kuwapita wapinzani wake kuelekea eneo la hatari.
Akiwa amesogea umbali mfupi nje ya boksi, Enzo Fernandez hakuwa na chaguo zaidi ya kumkwatua nyota huyo wa Real Madrid ili kuzuia shambulizi hilo.
34- FAULO: Giuliano Simeone dhidi ya Marc Guehi
Hii ilikuwa moja ya faulo za kushangaza zaidi katika mchezo.
Giuliano Simeone alianza kwa kumvuta kaptura Marc Guehi, kisha akamkamata jezi, baadaye akamsukumia kichwa kifuani na hatimaye akamkwatua kwa mguu, hatua iliyomwangusha beki huyo wa England.
35- FAULO: Nahuel Molina dhidi ya Jude Bellingham
Beki wa Argentina, Nahuel Molina, aliyekuwa akipata wakati mgumu kumkabili Djed Spence katika kipindi cha kwanza, alionyesha kufadhaika kwa kumwangusha Jude Bellingham kwa faulo ya nyuma.
Molina hakufanya jitihada zozote za kuucheza mpira, bali alimkata moja kwa moja nyota huyo wa England karibu na eneo hatari, na kuipa England mpira wa adhabu.
42- KADI YA NJANO: Lisandro Martinez dhidi ya Morgan Rogers
Hatimaye mwamuzi alimwadhibu mchezaji wa Argentina kwa kutoa kadi ya njano kwa Lisandro Martinez, baada ya kumzuia Morgan Rogers aliyekuwa akiongoza shambulizi la kushtukiza la England.
Martinez alimwangusha Rogers kwa makusudi ili kuvunja mashambulizi hayo, jambo lililomlazimu mwamuzi kumwonyesha kadi ya njano.
43- FAULO: Nahuel Molina dhidi ya Elliot Anderson
Baada ya Elliot Anderson kumwibia mpira Lionel Messi ndani ya nusu ya uwanja wa England, Argentina ililazimika kusitisha haraka shambulizi hilo.
Beki wa kulia Nahuel Molina alimkaba Anderson kwa ukali na kumkwatua miguuni, hatua iliyomlazimu mwamuzi kupuliza filimbi na kuipa England mpira wa adhabu.
45+3- FAULO: Leandro Paredes dhidi ya Reece James
Mwishoni mwa kipindi cha kwanza, Reece James na Leandro Paredes walikwenda kuwania mpira mmoja ndani ya nusu ya uwanja wa Argentina.
Katika harakati hizo, Paredes alinyanyua mguu juu kupita kiasi na kumgonga beki huyo wa England kwa mchezo wa hatari, jambo lililomlazimu mwamuzi kutoa faulo kwa England.
Tukio hilo liliongeza orodha ya faulo za Argentina katika kipindi cha kwanza, huku Paredes akiendelea kuwa mmoja wa wachezaji waliocheza faulo nyingi dhidi ya nyota wa England.
MAPUMZIKO
51- KADI YA NJANO: Cristian Romero dhidi ya Jude Bellingham
Beki wa Argentina, Cristian Romero, alionyeshwa kadi ya njano baada ya kumzuia kwa makusudi Jude Bellingham aliyekuwa ameanzisha shambulizi la kushtukiza.
Romero alimkumbatia na kumvuta Bellingham karibu na mstari wa katikati ya uwanja ili kuzuia asisogee mbele, jambo lililomlazimu mwamuzi kumpa onyo la kadi ya njano.
68- FAULO: Cristian Romero dhidi ya Djed Spence
Sekunde chache baada ya Jordan Pickford kufanya kazi ya ziada kwa kuokoa shuti la hatari la Nico Gonzalez karibu na eneo la goli, Djed Spence alikimbilia mpira ili kuuondoa kwenye hatari.
Hata hivyo, Cristian Romero alimzuia kwa kumvuta jezi na kumwangusha chini kabla hajauondoa mpira, jambo lililomlazimu mwamuzi kupuliza filimbi na kuipa England mpira wa adhabu.
81- FAULO: Nico Gonzalez dhidi ya Harry Kane
Baada ya Argentina kuweka presha kubwa mfululizo kwenye lango la England, Harry Kane alionyesha uzoefu wake kwa kujilinda vizuri pembeni mwa eneo la hatari.
Katika harakati hizo, Nico Gonzalez alichelewa kuingia kwenye mpira na kumkanyaga kwa kumkwatua Kane kwa mbinu isiyokuwa na wakati sahihi.
Mwamuzi aliingilia kati na kuipa England mpira wa adhabu, huku Kane akifanikiwa kupata faulo muhimu iliyosaidia timu yake kupunguza kasi ya mashambulizi ya Argentina.