Siri nyingine nyuma ya pete za ubingwa Knicks
Muktasari:
- Muundo huo wa kipekee umeandaliwa kuenzi ubingwa wa NBA ambao timu hiyo iliusubiri kwa muda mrefu, huku mashabiki pia wakipewa nafasi ya kununua pete za kumbukumbu. Hata hivyo, siyo kwa bei nafuu.
NEW YORK, MAREKANI: BINGWA wa Ligi ya Kikapu Marekani msimu uliopita wa 2025/26 alipatikana Juni 14, 2026, ambapo New York Knicks walitawazwa mabingwa baada ya kuifumua San Antonio Spurs kwenye mchezo wa tano kwa ushindi wa michezo 4-1.
Lakini, nyuma ya ubingwa wake, pete ya ubingwa ya Knicks waliyokabidhiwa wachezaji ina kitu cha kushangaza kilichofichwa ndani yake; mfano mdogo wa Uwanja wa Madison Square Garden unaoinuka kupitia mfumo maalumu wa kimakenika uliobuniwa kwa ustadi wa hali ya juu.
Muundo huo wa kipekee umeandaliwa kuenzi ubingwa wa NBA ambao timu hiyo iliusubiri kwa muda mrefu, huku mashabiki pia wakipewa nafasi ya kununua pete za kumbukumbu. Hata hivyo, siyo kwa bei nafuu.
Knicks ilizindua pete zake za ubingwa Jumanne, Oktoba 20, kabla ya mchezo wake wa kwanza wa msimu dhidi ya Philadelphia 76ers kwenye Uwanja wa Madison Square Garden. Hafla hiyo iliadhimisha ubingwa wa kwanza wa NBA kwa klabu hiyo baada ya miaka 53.
PETE YA UBINGWA INA ALMASI NGAPI?
Pete hizo zilizobuniwa na Jason Arasheben, mwanzilishi wa kampuni ya vito vya thamani ya Jason of Beverly Hills, zina karibu almasi na yakuti samawi 800 zenye jumla ya takribani karati 22. Pete hizo pia zimetengenezwa kwa dhahabu nyeupe na zina uzito wa zaidi ya gramu 160, zikikaribia gramu 200, kwa mujibu wa mahojiano ya mbunifu huyo na jarida la PEOPLE.
Rangi maarufu ya machungwa ya Knicks imewakilishwa kupitia yakuti zilizounda nembo ya timu, ambayo imezungukwa na almasi nyeupe.
Nyuma ya nembo hiyo, yakuti samawi zimepangwa kwa mtindo wa miale inayotoka katikati, muundo uliochochewa na mwonekano wa ndani ya Uwanja wa Madison Square Garden kutoka kwenye viti vya watazamaji.
Maelezo mengine ya muundo huo yanakumbusha matukio na mafanikio maalumu yaliyopatikana katika msimu wa ubingwa. Almasi 16 zilizokatwa kwa mtindo wa mstatili zinawakilisha ushindi 16 ambao timu hiyo ilipata katika mechi za mchujo (playoffs).
Almasi yenye karati 0.16 iliyowekwa kwenye mfano wa kombe la ubingwa la Larry O'Brien inakumbusha namna Knicks ilivyorejea kutoka nyuma kwa tofauti ya pointi 16 katika mchezo wa tano wa fainali dhidi ya San Antonio.
Maneno “World Champions” (Mabingwa wa Dunia) nayo yamepambwa kwa vipande 69 vya almasi, vinavyowakilisha jumla ya ushindi wa timu hiyo katika msimu wa kawaida na hatua ya mchujo.
Kila pete imewekewa utambulisho wa mchezaji husika. Majina yao na namba za jezi zimewekwa kwenye muundo huo, hivyo kila mchezaji anakuwa na pete inayomtambulisha binafsi badala ya wote kupewa pete zinazofanana.
Maandishi mengine mawili yamewekwa kwenye pete hizo kuonyesha safari ya timu hiyo kutwaa ubingwa. Maneno “Knicks in Five” yanakumbusha ushindi wa mechi tano dhidi ya San Antonio katika mfululizo wa fainali, huku maneno “10 weeks” yakirejelea kipindi cha wiki 10 ambacho mmiliki wa Knicks, James Dolan, aliwaomba wachezaji wajitoe na kujitolea kwa ajili ya harakati za kutwaa ubingwa.
MADISON SQUARE GARDEN
Kitu kinachovutia zaidi katika pete ya ubingwa ya Knicks ni mfumo wake tata wa ubunifu. Ukiizungusha sehemu ya ndani ya pete, mfano mdogo wa Uwanja wa Madison Square Garden huinuka kutoka katikati yake ukiwa na maelezo mbalimbali ya usanifu wa uwanja huo.
Muundo huo pia unajumuisha sehemu za ndani ya uwanja, ikiwemo mfano wa eneo la chini lenye viti vya watazamaji pamoja na uwanja wa mchezo wa kikapu. Wazo la wabunifu lilikuwa kuufanya Uwanja wa Madison Square Garden wenyewe kuwa sehemu ya kumbukumbu ya ubingwa huo, badala ya kuweka tu nembo ya timu kwenye kipande cha vito vya thamani kubwa.
Katika mahojiano na jarida la GQ, Arasheben alieleza kuwa Madison Square Garden ndiyo iliyokuwa msukumo wa muundo huo.
“Ni lazima isimulie hadithi inayozidi tu uzuri wa mwonekano wake,” anasema mbunifu huyo akielezea changamoto ya kutengeneza pete ya ubingwa. Knicks ilikuwa imetumia miaka 53 bila kutwaa ubingwa wa NBA, jambo lililoufanya mradi huo kuwa na maana kubwa zaidi.
Arasheben alitaka pete hiyo ionyeshe utambulisho wa timu pamoja na hisia zilizotokana na ubingwa ambao vizazi kadhaa vya mashabiki vilikuwa vikisubiri kuusherehekea. Matokeo yake ni pete iliyounganisha vifaa vya kifahari na mfumo tata kibunifu unaoifanya kuwa tofauti na pete nyingine za ubingwa.
PETE UNAINUNUAJE?
Ingawa pete halisi zilitengenezwa kwa ajili ya wachezaji na viongozi wa timu, mashabiki wanaweza kununua za kumbukumbu kupitia mpango maalumu wa kampuni hiyo ya vito unaoitwa Championship Fan Program.
Bei ya pete halisi walizopewa wachezaji haijawekwa wazi kwa umma. Hata hivyo, kumewekwa machaguo mawili ya pete za kumbukumbu kwa mashabiki kupitia mpango maalumu wa Knicks Fan Program.
Toleo la Premier ndilo lenye bei kubwa zaidi kati ya pete hizo mbili zinazouzwa kwa mashabiki likiwa limetengenezwa kwa dhahabu nyeupe na almasi halisi, huku likiwa na nakala 200 pekee ambazo kila moja ina namba yake maalumu.
Wanunuzi wanaweza kuweka jina na kuchagua ukubwa wa pete wanayotaka. Kampuni hiyo inakadiria kuwa muda wa utengenezaji na usafirishaji ni kati ya wiki nane hadi 10.
Kifurushi hicho kinajumuisha boksi maalumu la kifahari kwa ajili ya kuhifadhi pete, dhamana ya muda mrefu yenye masharti maalumu pamoja na cheti cha kuthibitisha uhalisi wake. Pete hiyo ina thamani ya Dola 19,995 (takriban Sh53 milioni).
Toleo jingine la pete hiyo ni la Legacy ambalo ndilo lenye bei nafuu zaidi, lakini limetengenezwa kwa vifaa tofauti linalogharimu Dola 1,795 (zaidi ya Sh4.8 milioni). Badala ya dhahabu nyeupe na almasi halisi, limetengenezwa kwa madini ya fedha maarufu kama 'sterling silver' na mawe ya cubic zirconia.
Wanunuzi pia wanaweza kuweka majina yao na kuchagua ukubwa wa pete. Muda wa makadirio ya utengenezaji na usafirishaji ni wiki nane hadi 10, sawa na toleo la Premier.
Mpango wa kampuni iliyopewa zabuni kwa mashabiki pia unajumuisha bidhaa nyingine za kumbukumbu ya ubingwa huo. Kwa mfano, kuna pambo maalumu la mezani (paperweight) linalouzwa kwa Dola 299 (takriban Sh791,358), ambalo ni bidhaa tofauti ya kumbukumbu na siyo aina nyingine ya pete.