Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

SOWETO DERBY; Orlando, Kaizer Chiefs kinapigwa

SOWETO Pict

Muktasari:

  • Mara ya mwisho vigogo hao wa Ligi Kuu Afrika Kusini (PSL) walipokutana walitoka sare ya bao 1-1, ambapo Kamogelo Sebelebele wa Pirates na Mmodi Pule (Chiefs) walifunga mabao katika kipindi cha pili cha mchezo uliopigwa Aprili 26, 2026.

MUNICH, UJERUMANI: LEO, Jumamosi mashabiki wa Orlando Pirates na Kaizer Chiefs watakuwa wanaziombea mema timu zao katika mchezo wa Dabi ya Soweto unaopigwa kwenye Uwanja wa FNB uliopo Johannesburg, Afrika Kusini unaoanza saa 10:30 jioni.

Mara ya mwisho vigogo hao wa Ligi Kuu Afrika Kusini (PSL) walipokutana walitoka sare ya bao 1-1, ambapo Kamogelo Sebelebele wa Pirates na Mmodi Pule (Chiefs) walifunga mabao katika kipindi cha pili cha mchezo uliopigwa Aprili 26, 2026.

Kabla ya mchezo huo, Pirates ilikuwa na matokeo bora katika mechi za karibuni za dabi dhidi ya Chiefs. Hii inajumuisha ushindi wa mabao 3-0 ugenini Februari 2026 na ushindi wa mabao 3-2 nyumbani Machi 2024.

Pirates inaendelea na mbio za ubingwa wa PSL, ikiwa nyuma kwa pointi moja dhidi ya Sundowns ikiwa nazo 22. Kwa upande wao Amakhosi wana alama 14 wakishika nafasi ya tano.

Kwa upande mwingine, Chiefs imekuwa ikipata shida kupata ushindi katika mashindano ya ndani na ya kimataifa. Ingawa mechi za dabi mara nyingi huwa hazitabiriki, Pirates inaonekana kuwa katika kiwango bora zaidi kuliko mpinzani wake.

Tiketi zote kwa ajili ya mechi hiyo zilikuwa 94,736 zimeuzwa wiki moja iliyopita kwa ajili ya mchezo huo wa Dabi ya Soweto  ambapo Kaizer Chiefs itakuwa mwenyeji wa Orlando Pirates katika Uwanja wa FNB uliopo Johannesburg.


SOWE 01

DABI YA SOWETO ILIVYOANZA

Yote yalianza Januari 24, 1970, wakati Orlando Pirates ilipokutana na Kaizer Chiefs iliyokuwa na umri wa siku 17 katika Uwanja wa Orlando, Soweto, Johannesburg. Kwa kushangaza, mchezo huo ungeweza kuwa mechi isiyo na umuhimu mkubwa ya kuwania nafasi ya tatu kati ya timu mbili za Soweto, lakini mazingira yaliyozunguka pambano hilo yalilifanya isiwe mechi ya kawaida.

Timu zote mbili zilikuwa zimepoteza mechi zao za nusu fainali za Rogue Beer Cup, lakini kutokana na mchezo huo wa kuwania nafasi ya tatu, pambano kubwa zaidi katika kalenda ya soka ya Afrika Kusini, Soweto Derby, likazaliwa. Hiyo ilikuwa mechi ya kwanza kati michezo 184 iliyochezwa hadi sasa.

Hilo halikuwa pambano jingine la kawaida, ilikuwa mechi iliyojaa hisia kali na uhasama, iliyochochewa na mvutano uliokuwa ukijengeka kwa mwaka mmoja, huku ikiwa ni pambano ambalo baba alitaka kumfundisha mwanawe somo.

SOWE 04

Mwanzilishi wa Kaizer Chiefs, Kaizer Motaung, alikuwa amelelewa kisoka na Orlando Pirates, timu ambayo aliitumikia na kujipatia umaarufu kabla ya kuondoka na kwenda kucheza soka nchini Marekani katika Klabu ya Atlanta Chiefs.

Hata hivyo, aliporejea 1969, Chincha Guluva, kama alivyokuwa akifahamika kwa upendo na mashabiki wa Kaizer Chiefs maarufu kama Amakhosi au Buccaneers, alijiunga na upande mmoja katika mgogoro uliohusisha wachezaji watatu waliofukuzwa Orlando Pirates; Thomas ‘Zero’ Johnson, Edward ‘Msomi’ Khoza na Ratha ‘Jimmy Greaves’ Mokgoatleng, ambaye kwa sasa ni Jaji katika kesi ya mauaji ya Senzo Meyiwa.

Senzo ni mwanasoka wa zamani wa Afrika Kusini aliyekuwa kipa na nahodha wa Orlando Pirates, alipigwa risasi na kuuawa wakati wa uvamizi nyumbani kwake Oktoba 26, 2014.

Wachezaji hao watatu walikiuka taratibu za klabu kwa kukubali mwaliko wa kushiriki mashindano ya soka ya Krismasi nchini Botswana bila idhini ya Orlando Pirates, jambo lililosababisha klabu kuchukua hatua za kinidhamu dhidi yao.

Hata hivyo, hatua hizo za kinidhamu hatimaye zilichochea mabadiliko makubwa katika soka nchini humo, na kusababisha kuzaliwa kwa mojawapo ya upinzani mkubwa zaidi katika soka la dunia.

SOWE 03

Motaung alianzisha Kaizer Chiefs 1969 akiwa pamoja na wachezaji hao watatu. Kabla ya hapo, kismingi Dabi ya Soweto ilikuwa ushindani kati ya Orlando Pirates na Moroka Swallows, uliochochewa zaidi na ukaribu wa kijiografia kati ya timu hizo.

Lakini, Pirates na Chiefs zilipofungwa katika mechi zao za nusu fainali za Rogue Beer Cup, kukutana kwao katika mchezo wa kuwania nafasi ya tatu kulizaa Dabi ya Soweto ya aina tofauti, iliyochochewa na historia, hisia na hamu iliyokuwa ikiongezeka ya kila timu kutaka kuizidi nyingine.

“Kwa Chiefs kukutana na Pirates ilikuwa kama ‘mwana kukabiliana na baba yake’, kwa sababu Motaung kwa kiasi kikubwa alilelewa na Bucs, angalau katika masuala ya soka,” inaeleza sehemu ya makala iliyochapishwa kwenye tovuti ya Kaizer Chiefs kuhusu chimbuko la ushindani huo.

“Matarajio yalikuwa makubwa. Uwanja wa Orlando ulijaa shamrashamra na msisimko katika Jumamosi hiyo ya kihistoria. Kaizer Motaung alicheza mechi bora zaidi maishani mwake, mara nyingi akiwapita kwa chenga mabeki wote wa Bucs.

SOWE 02

Winga wa kulia Alfred ‘Bomber’ Chamane na Patrick ‘Ace’ Ntsoelengoe, aliyekuwa mdogo zaidi kwa umri miongoni mwa wachezaji wa Chiefs, nao walicheza vizuri.

“Hata hivyo, ni Percy Moloi aliyeipa Pirates bao la kuongoza kwa shuti kali. Kosa la ulinzi lilisababisha Bucs kupata bao jingine. Lakini klabu hiyo iliyokuwa na umri wa siku 17 ilipambana na kusawazisha kabla ya mapumziko, kutokana na mabao mawili ya Ntsoelengoe,” inasomeka sehemu ya makala hiyo.

Ikikumbuka matukio ya pambano hilo maalumu, makala hiyo inaeleza: “Katika kipindi cha pili, Kaizer Motaung alionyesha tena kwa nini alikuwa shujaa mkubwa kwa mashabiki wa soka wa Marekani alipokuwa akiichezea Atlanta Chiefs. Lakini badala yake, ni Pirates iliyopata bao na kusonga mbele kwa mabao 5-3, huku kiungo mkabaji Petros ‘Ten-Ten’ Nzimande akiifungia Chiefs.

Baadaye, beki imara Jackie Masike alipiga shuti kali kutoka umbali mrefu, na kufanya matokeo kuwa 5-4.”

Orlando Pirates ilishinda pambano hilo la kwanza kwa mabao 6-4, kutokana na bao la dakika za mwisho lililofungwa na Bernard ‘Dancing Shoes’ Hartze. Kuanzia wakati huo, kila pambano kati ya timu hizo limekuwa likibeba uzito wa ushindani huohuo, huku kila timu ikitaka kuonyesha ubabe wake dhidi ya nyingine na kujitwalia haki ya kujigamba hadi watakapokutana tena.

Siku hiyo, Dabi ya Soweto ilizaliwa. Na sasa, zaidi ya miaka 50 baadaye, ushindani huo unaendelea kuvutia vizazi mbalimbali vya mashabiki wa soka. Takwimu zinaonyesha Kaizer Chiefs imeshinda mechi 75, huku Orlando Pirates ikishinda 49 ilhali sare ni mara 60, na katika kuendeleza ari hiyo, maandalizi ya kuelekea Dabi ya Soweto yamepamba moto kuelekea pambano la 185 linalochezwa leo, Jumamosi.