Sir Ferguson atoa siri ya hofu yake
Muktasari:
- Ferguson, mwenye umri wa miaka 84, amesema alikuwa akiwaza kuhusu uwezekano wa kukumbwa na ugonjwa huo kutokana na muda mwingi aliotumia kupiga mipira kwa kichwa wakati wa uchezaji wake.
LONDON, ENGLAND: KOCHA wa zamani wa Manchester United, Sir Alex Ferguson amefichua hofu yake kuhusu ugonjwa wa shida ya akili (dementia), akisema historia yake ya kucheza soka inamfanya kuwa na wasiwasi kuhusu afya yake anavyoendelea kuzeeka.
Ferguson, mwenye umri wa miaka 84, amesema alikuwa akiwaza kuhusu uwezekano wa kukumbwa na ugonjwa huo kutokana na muda mwingi aliotumia kupiga mipira kwa kichwa wakati wa uchezaji wake.
“Niliwahi kuwa na wasiwasi kuhusu hilo kwa sababu nilipiga mipira mingi kwa kichwa. Wachezaji wote wa soka walifanya hivyo,” Ferguson aliliambia gazeti la The Observer.
“Dementia ni changamoto kwa mtu yeyote anayezeeka. Unakuwa na wasiwasi sana kuhusu hilo. Huwa najisema mwenyewe: ‘Nina miaka 84. Nikifika 85, nitakuwa salama,’” amesema.
Ferguson amekuwa akitoa msaada mkubwa kwa kaka yake, Martin, ambaye anaishi na dementia, kiasi cha kununua nyumba jijini Glasgow ili kuwa karibu naye.
Pia amekuwa mmoja wa waungaji mkono wakubwa wa taasisi zinazopambana na dementia, ikiwamo Race Against Dementia, iliyoanzishwa na nyota wa zamani wa Formula 1, Jackie Stewart.
Ferguson pia ameeleza namna shirika la Playlist for Life lilivyosaidia kuboresha maisha ya kaka yake kupitia muziki.
Amesema Martin bado anamtambua, jambo analoliona kuwa la faraja, huku muziki ukitumika kuchochea kumbukumbu zake.
Kwa mujibu wa Ferguson, mfumo huo unahusisha kumpa mgonjwa kisanduku chenye nyimbo anazozipenda, ambacho anaweza kubonyeza na kusikiliza muziki huo, jambo linaloweza kumrudisha kwenye kumbukumbu za zamani.
Kutokana na kuguswa na kazi hiyo, Ferguson alitoa mchango wa pauni 100,000 kwa shirika hilo, huku akiwasilisha orodha ya nyimbo kutoka kwa wasanii kama Frank Sinatra, The Beatles na Elvis Presley.
Ferguson, ambaye alistaafu ukocha mwaka 2013, ameendelea kuwa karibu na Manchester United na mara kwa mara huonekana uwanjani akiishuhudia timu hiyo.
Hata hivyo, gwiji huyo amewahi kukumbana na changamoto kadhaa za kiafya. Mwaka 2018 alipatwa na tatizo la kuvuja damu kwenye ubongo na madaktari walimpa nafasi ya asilimia 20 tu ya kupona.
Mwezi Mei mwaka huu, Ferguson alikumbwa tena na tatizo la kiafya kabla ya mchezo wa Manchester United dhidi ya Liverpool na kupelekwa hospitalini.
Mwezi uliopita pia alionekana akiwa amevaa buti maalumu la matibabu mguuni, hali iliyokuja kufahamika kuwa ilisababishwa na tatizo la kano ya Achilles.