Baleba kazi anayo, United yaweka mzigo begani
Muktasari:
- Kuna kumbukumbu inayowafanya baadhi ya mashabiki wa Man United kuwa na hofu. Miaka miwili iliyopita, Manuel Ugarte alianza mchezo wake wa kwanza wa Ligi Kuu akiwa sambamba na Kobbie Mainoo kwenye Uwanja wa Old Trafford dhidi ya Tottenham. United ilipoteza 3-0, huku Ugarte akicheza chini ya Erik ten Hag, kabla ya kupewa nafasi nyingine ya kuanza katika ligi chini ya Ruud van Nistelrooy.
MANCHESTER, England. KIUNGO Carlos Baleba anatarajiwa kupewa nafasi yake ya kwanza katika kikosi cha Manchester United kwenye Ligi Kuu England dhidi ya Tottenham Jumamosi ijayo, lakini tayari kiungo huyo amebebeshwa mzigo mkubwa wa matarajio kabla hata hajacheza mchezo wake wa kwanza.
Kuna kumbukumbu inayowafanya baadhi ya mashabiki wa Man United kuwa na hofu. Miaka miwili iliyopita, Manuel Ugarte alianza mchezo wake wa kwanza wa Ligi Kuu akiwa sambamba na Kobbie Mainoo kwenye Uwanja wa Old Trafford dhidi ya Tottenham. United ilipoteza 3-0, huku Ugarte akicheza chini ya Erik ten Hag, kabla ya kupewa nafasi nyingine ya kuanza katika ligi chini ya Ruud van Nistelrooy.
Michael Carrick sasa anatumaini historia hiyo haitajirudia iwapo atamchezesha Baleba dhidi ya Spurs.
Baleba, ambaye alikaa benchi katika mchezo dhidi ya Fulham, anatarajiwa kuanza dhidi ya Tottenham ambayo bado haijapata ushindi. Kiungo huyo raia wa Cameroon atakuwa amepata takribani wiki tatu za mazoezi na kikosi kipya, huku United ikiwa ikihitaji nguvu zaidi katikati ya uwanja kutokana na udhaifu ulioonekana katika safu yake ya ulinzi.
Youri Tielemans anaonekana kutokuwa na aina ya sifa zinazohitajika kucheza sambamba na Mainoo katika michezo yenye presha kubwa kama hiyo, wakati Andrey Santos bado hajapewa nafasi ya kutosha tangu alipoanza kwa kusuasua dhidi ya Hull.
Uamuzi wa United kumfuatilia Baleba tangu dirisha la usajili la majira ya kiangazi lililopita ulionekana pia, kama ishara kwamba klabu hiyo ilikuwa imeanza kupoteza imani na Ugarte.
Hata hivyo, kwa kusubiri hadi wiki mbili za mwisho za dirisha hili kukamilisha usajili wa kiungo huyo wa zamani wa Brighton, United imejikuta ikianza safari ikiwa nyuma ya ratiba.
Baleba alitambulishwa kwa mashabiki wa Old Trafford mwezi uliopita wakati timu ikiwa bado haijapona kutokana na kipigo cha 1-0 dhidi ya Hull City katika mchezo wa kwanza wa msimu.
Baada ya hapo, sare dhidi ya Everton, vipigo kutoka kwa Manchester City na Brighton, pamoja na sare ya bahati dhidi ya Fulham, si mazingira rahisi kwa mchezaji mpya kuingia na kuanza kuibeba timu.
Kiungo huyo mwenye miaka 22 aligharimu karibu pauni70 milioni, huku United ikimtarajia kuwa mchezaji wa kiwango cha kubadilisha mambo katikati ya uwanja aina ya usajili ambayo klabu hiyo haijapata kwa muda mrefu.
United kwa sasa iko katika nafasi ya 12 ikiwa imeruhusu mabao manane katika mechi tano, huku uamuzi ya kocha katika mchezo dhidi ya Fulham yakipokelewa kwa kuzomewa na baadhi ya mashabiki.
Hivyo, Baleba anaingia kwenye mazingira ambayo yanahitaji mabega mapana.
United imewahi kupata viungo wa ulinzi walioweza kuziba pengo kwa muda, akiwamo Ander Herrera msimu wa 2016/17 na Casemiro msimu wa 2022/23, lakini haijapata suluhisho la kudumu kwa muda mrefu.
Mpango wa United ni kumtumia Baleba kwa miaka mingi ijayo. Tatizo ni kwamba kabla hata hajagusa mpira katika mchezo wake wa kwanza, tayari amebebeshwa matarajio makubwa ambayo si rahisi kuyakimbia.
Baleba pia anatakiwa kuthibitisha uwezo wake baada ya msimu wake wa mwisho Brighton kutokuwa na mwendelezo mzuri, akitolewa uwanjani wakati wa mapumziko mara nne.
Na atakapoingia uwanjani dhidi ya Tottenham Jumamosi ijayo jioni, atakuwa hajacheza mchezo wa ushindani kwa takribani miezi mitatu.
Mechi yake pekee ya maandalizi ya msimu kwa Brighton ilikuwa Julai 18 katika mchezo wa kirafiki uliofanyika bila mashabiki dhidi ya Wycombe Wanderers.
Hiyo ni tofauti kubwa na mazingira anayokwenda kukutana nayo Old Trafford, ambako mashabiki zaidi ya 70,000 tayari wameanza kuonyesha hasira kutokana na mwenendo wa timu.
Baleba alishuhudia kwa macho akiwa katika jukwaa maalumu wakati Brighton ilipowatoa United kwenye Carabao Cup, licha ya United kuwa mbele kwa mabao 2-0. Brighton iliweka rekodi kwa kuwa timu ya kwanza kwa miaka 50 kushinda Old Trafford baada ya kuwa nyuma kwa mabao mawili.
Na huo ndio uhalisia wa United kwa sasa.
Kwa bahati yake, Baleba hakulazimika kusikia mashabiki wa ugenini wakimdhihaki kwa kuimba jina lake na kuuliza, “Carlos, Carlos, matokeo yakoje?”
Mchezo dhidi ya Tottenham unaweza pia kumkutanisha na Mateus Fernandes na Sandro Tonali, wachezaji ambao United iliwahi kuwafikiria kuwasajili kabla Spurs hawajawazidi nguvu.
Tonali alionekana kuwa ghali na hakulingana kikamilifu na aina ya kiungo ambaye United ilikuwa ikimtafuta, huku Fernandes akiwa na gharama kubwa licha ya kuhusika na timu mbili zilizoshuka daraja kutoka Ligi Kuu England katika misimu miwili mfululizo.
Hata hivyo, wote ni wachezaji wenye uwezo wa kuisumbua United. Tonali tayari amewahi kufanya hivyo mara kadhaa akiwa Newcastle, huku Fernandes akionyesha ubora wake katika sare ya West Ham dhidi ya United kwenye Uwanja wa London Februari iliyopita.
Historia ya United pia inaonyesha kwamba si kila usajili mkubwa lazima uwe jina maarufu.
Carrick hakuwa mchezaji aliyependwa zaidi na mashabiki wakati alipojiunga na United mwaka 2006. Javier Mascherano ndiye aliyekuwa chaguo lililopewa uzito zaidi, huku mashabiki wa United wakitamani klabu iwashawishi Rino Gattuso au Andrea Pirlo kutoka AC Milan baada ya sakata la Calciopoli.
Sir Alex Ferguson pia alimfuatilia Owen Hargreaves katika dirisha hilo, lakini ilimchukua mwaka mwingine kumleta Old Trafford. Jaribio la kumsajili Marcos Senna wa Villarreal na Hispania siku ya mwisho ya dirisha la usajili pia lilishindikana.
Sasa zamu ni ya Baleba. Tofauti ni kwamba wakati huu, United inamhitaji si tu kuwa kiungo mpya, bali pia kuwa sehemu ya suluhisho la matatizo yanayoikabili timu.