Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simulizi ya ajabu Matheus Cunha na mkewe Gabriela

Muktasari:

  • Moja ya simulizi hizo, ni kitendo cha Gabriela kuhararakisha kuzaliwa kwa mtoto wao wa pili ili kutoa nafasi kwa Cunha kuwahi maandalizi ya msimu mpya wa ligi akiwa kama mchezaji mpya wa Manchester United.

KUNA mengi yanaendelea nyuma ya pazia katika ndoa ya staa wa Manchester United na timu ya taifa ya Brazil, Matheus Cunha, 27, na mkewe Gabriela Nogueira, na hizi ni aina ya simulizi ambazo mashabiki hupenda kuzifuatilia na kuzisikia kutoka kwa wachezaji maarufu.

Moja ya simulizi hizo, ni kitendo cha Gabriela kuhararakisha kuzaliwa kwa mtoto wao wa pili ili kutoa nafasi kwa Cunha kuwahi maandalizi ya msimu mpya wa ligi akiwa kama mchezaji mpya wa Manchester United, hivyo kwa ujumla nyuma ya mafanikio ya Cunha uwanjani kuna familia ambayo imekuwa sehemu muhimu ya maisha yake hasa mkewe Gabriela ambaye kwa miaka mingi amekuwa akimpa sapoti hadi sasa anapotazamwa kama staa mkubwa wa soka duniani.

Gabriela alizaliwa mjini Rio de Janeiro, Brazil, Oktoba 5, 1993, hivyo kwa sasa ana umri wa miaka 33 akiwa amemzidi mumewe Cunha miaka sita ya kuzaliwa lakini tofauti hiyo ya umri haijawahi kuwa kikwazo kwao.

Inaelezwa kuwa wawili hao walikuwa katika uhusiano kwa miaka saba kabla ya kuwatangazia mashabiki kuwa wapo pamoja. Waliweka uhusiano wao hadharani Mei 2018 kupitia Instagram wakati Gabriela akimtakia Cunha heri ya kuzaliwa.

Kutokana na aina ya kazi ya Cunha, Gabriela amekuwa akisafiri naye katika maeneo mbalimbali duniani, ukurasa wake wa Instagram umekuwa kama sehemu ya kumbukumbu muhimu za safari ambazo wamekuwa wakizifanya pamoja kila mara.

Walifunga ndoa Mei 25, 2024, muda mfupi baada ya Cunha kumaliza msimu wa Ligi Kuu England (EPL) akiwa na klabu yake ya zamani ya Wolves. Harusi yao ilifanyika ufukweni katika mji wao wa Rio de Janeiro nchini Brazil.

Mtoto wao wa kwanza ambaye ni wa kiume anaitwa Levi, alizaliwa Mei 2020 ikiwa ni takribani miwili tu baada ya wazazi wake kutangaza hadharani uhusiano wao.

Siku chache baada ya kuzaliwa Levi, mama yake Gabriela aliandika ujumbe Instagram akielezea furaha yake huku akimtaja Cunha kama baba sahihi kwa mtoto huyo.

"Ni kweli levi amezaliwa na yupo hapa kunikumbusha kila siku kwamba nilimchagua mwenzi bora wa kutembea naye, wa kunishika mkono na kuniambia kwamba kila kitu kitakuwa sawa. Nilihitaji tu kuona namna Cunha alivyomtazama mtoto wetu, ndipo nikatambua kwamba hakuna nafasi tena ya hofu ndani yangu!” aliandika Gabriela.

Tangu wakati huo, Levi amekuwa akisafiri pamoja na wazazi wake akihudhuria mechi mbalimbali za soka katika viwanja vingi vya EPL.

Kufikia Januari 2025, Gabriela alitangaza kuwa familia yao ilikuwa inatarajia kuongezeka baada ya kuwa mjamzito wa mtoto wao wa pili. Hatimaye Julai 2025 alijifungua mtoto wa kike ambaye walimpa jina la Liz.

Kwa mujibu wa mtandao wa SunSport, Gabriela aliwaomba madaktari kuharakisha muda wa kujifungua mtoto wao wa pili ili Cunha apate nafasi ya kushuhudia kuzaliwa kwa mtoto huyo kabla ya ziara ya maandalizi ya msimu mpya nchini Marekani akiwa na Man United.

Ikumbukwe Cunha alisaini kujiunga na Man United akitokea Wolves mnamo Juni 2025, baada ya klabu hiyo ya Old Trafford kutumia vizuri kipengele cha kuvunja mkataba wake.

“Gabriela alijua jinsi ilivyokuwa muhimu kwa Cunha kushiriki katika ziara ya maandalizi ya msimu ili aweze kuwafahamu wachezaji wenzake kabla ya msimu kuanza," chanzo kimoja kilisema na kuongeza:

“Hivyo walijadiliana kuhusu jambo hilo kama wanandoa na madaktari wakakubaliana kupanga upasuaji wa kujifungua kwa njia ya C-section siku ya Jumatatu, ili Cunha aweze kuwa pembeni yake wakati wa tukio hilo." 

Hivyo Cunha alikuwepo hospitalini hadi Gabriela alipojifungua, na baadaye familia hiyo iliposti picha Instagram ikithibitishwa kuzaliwa kwa mtoto wao wakiandika; "Hamjambo?, mimi ni Liz. Sasa tumekuwa wanne. Nimebarikiwa sana kuwa nanyi. Asante Mungu kwa kila kitu."

Kwa sasa Gabriela amejikita katika malezi ya familia akiwa ameipa kisogo kazi yake ya sheria, taaluma aliyoisomea kwa miaka mitano katika Chuo Kikuu cha Jimbo la Rio de Janeiro nchini Brazil.

Hivyo mbali na uwezo wake wa kufunga mabao, kutengeneza nafasi na kucheza katika nafasi mbalimbali za ushambuliaji, Matheus Cunha ni baba wa familia ya watoto wawili aliyojaliwa katika ndoa yake na mkewe Gabriela Nogueira.