Albamu 10 kali kutoka Bongo Records

Muktasari:
- Wakati huu historia inamtambua Majani kama miongoni mwa watu wenye mchango mkubwa katika kuikuza Bongofleva kupitia studio na rekodi lebo yake - Bongo Records ambayo ametengeneza majina makubwa katika muziki huo. Fahamu zaidi.
KABLA ya P-Funk Majani kuwa mtayarishaji wa muziki mwenye mafanikio makubwa, awali kabisa alikuwa ni rapa na DJ. Hiyo ilikuwa mwanzoni mwa miaka 1990 wakati huo alikuwa anaitwa DJ Skills of Pain na alikuwa na kundi lake la muziki.
Wakati huu historia inamtambua Majani kama miongoni mwa watu wenye mchango mkubwa katika kuikuza Bongofleva kupitia studio na rekodi lebo yake - Bongo Records ambayo ametengeneza majina makubwa katika muziki huo. Fahamu zaidi.
1. Solo Thang na Juma Nature ndio wasanii wa kwanza kusainiwa Bongo Records rasmi katika mtindo wa kibiashara, ila hapo awali lebo hiyo ilisimamia kazi za wasanii kama Dolla Sol, Hashim Dogo, pamoja na kundi la No Name ambalo Majani pia alikuwamo.
2. Juma Nature alikuwa anatembea kwa mguu kutoka Temeke hadi Kijitonyama kuifuata Bongo Records, wakati huo baadhi ya watu hawakuamini uwezo wake hadi kumwambia P-Funk Majani kuwa Nature ni MC Cartoon, ila Majani akaamini Nature ana kitu.
Ikumbukwe wimbo uliomtoa Juma Nature ni ‘Kighetogheto’ uliotayarishwa na P-Funk Majini ndani ya Bongo Records, lakini huu ni toleo pili, wa kwanza (original version) Nature aliurekodi studio za Sound Crafters kwa Enrico Figueredo.
3. P-Funk Majani alikutana na Mandojo na Domokaya mkoaani Arusha akiwa kwenye ziara (tour) ya albamu ya pili ya Juma Nature, Ugali (2003) ambapo alivutiwa na uwezo wao na kuwakaribisha Bongo Records kwa ajili ya kufanya kazi.
4. Wimbo wa kwanza kwa Mandojo na Domokaya kurekodi Bongo Records ni ‘Nikupe Nini’ ambao ndio uliwatoa na ulijumuishwa katika albamu yao ya kwanza, Taswira (2005) iliyokuwa na nyimbo nyingine kali kama Digi, Wanok Nok, Niaje na kadhalika.
5. Ngwea alipata mkataba wa kurekodi albamu yake ya kwanza, A.K.A Mimi (2004) ndani ya Bongo Records baada ya kufanya vizuri na wimbo wake ‘Ghetto Langu’ uliotengenezwa na Majani, ikiwa ni baada ya msanii huyo kuchangiwa Sh100,000.
Hadi sasa A.K.A Mimi (2004) inatajwa na wengi kama albamu bora zaidi kutokea Bongo Records maana ilitoa nyimbo nyingi maarufu kama Mikasi, Napokea Simu, Bado Nimo, Ghetto Langu, Sikiliza, Mademu Wangu, Weekend, She Got A Gwan na kadhalika.
6. Jay Moe alianza kusaini Bongo Records mwaka 2000 akiwa ndani ya kundi la Wateule lililoanzishwa 1998 na Jay Moe mwenyewe, Jaffarai, Solo Thang n.k, kufika 2001 ndipo akasaini kama solo na kutoa albamu yake ya kwanza.
7. Kuna wakati Bongo Records walikuwa wanarekodi hadi nyimbo 300 kwa mwaka, wasanii walikuwa ni wengi wanaohitaji huduma yao kiasi kwamba iliwalazimu kurekodi na kumaliza walau nyimbo mbili au tatu kwa siku.
8. Chini ya Bongo Records, P-Funk Majani ameshiriki kutengeneza albamu nyingi kali na maarufu, na hizi ni baadhi; Machozi Jasho na Damu (2001) - Professor Jay, Ugali (2003) - Juma Nature, Ulimwengu Ndio Mama (2002) - Jay Moe na Safari (2005) - Ferooz. Nyingine ni Elimu Dunia (2004) - Daz Baba, Sauti ya Dhahabu (2002) - TID, Mkuki Moyoni (2003) - Afande Sele, Si Uliniambia (2005) - MB Dogg, Taswira (2005) - Mandojo na Domokaya, Vina Mwanzo Kati na Mwisho (2005) - Fid Q, A.K. A Mimi (2004) - Ngwea na kadhalika.
9. Kwa mujibu wa Ferooz, albamu yake, Safari (2005) iliuza nakala (kanda) 200,000 katika wiki yake ya kwanza sokoni, hivyo akarudi kwa msambazaji kugonga muhuri wa nakala nyingine tena, na akadiria kuwa albamu yote ilifikia mauzo ya Sh150 milioni. Kwa sehemu kubwa mauzo ya albamu hii yalichagizwa na wimbo ‘Starehe’ akimshirikisha Professor Jay, na huo ndio wimbo wa kwanza kwa msanii huyo kushuti video yake akitumia Sh1 milioni ambayo wakati huo ilikuwa fedha nyingi kuiwekeza kwenye video.
10. Naye TID aliyeanza muziki akiwa ndani ya kundi la Black Gangsters 1997 hadi 1999 albamu yake, Sauti ya Dhahabu (2002) chini ya Bongo Records ikitoa nyimbo maarufu kama Zeze na Siamini, mwanamuziki huyo anasema iliingiza Sh30 milioni.