Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Vita ya ushambuliaji, uzoefu na presha ya matokeo

PRESHA Pict

Muktasari:

  • Simba nayo kwenye mechi tano za ligi zilizopita, haijapoteza, ikishinda zote, wakati Wanderers ikishinda tatu na sare moja.

LILONGWE, MALAWI: MIGHTY Wanderers wanaingia kwenye pambano la Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Simba wakiwa na jambo moja la kujivunia, hawajapoteza katika mechi zao tano zilizopita za ligi, lakini wapinzani wao nao ni wakali.

Simba nayo kwenye mechi tano za ligi zilizopita, haijapoteza, ikishinda zote, wakati Wanderers ikishinda tatu na sare moja.

Wawakilishi hao wa Malawi watakutana na Simba Jumapili hii kwenye Uwanja wa Bingu uliopo Lilongwe nchini Malawi, katika mchezo ambao hautakuwa wa kawaida kwa pande zote mbili.

Wanderers katika mechi zao tano za mwisho wameshinda tatu na kutoka sare mbili. Walianza kwa kuifunga Civil Service 2-0, kisha wakatoka sare ya 1-1 dhidi ya Masters, wakashikilia sare nyingine ya 1-1 dhidi ya Moyale Barracks kabla ya kuifunga Kamuzu Barracks 2-0 na Red Lions 2-1.

Kwa hesabu hizo, Wanderers wamefunga mabao manane na kuruhusu manne katika mechi hizo tano.

Simba, kwa upande wake, inaingia kwenye mchezo huo ikiwa na rekodi inayovutia zaidi.

Wawakilishi hao wa Tanzania wameshinda mechi zote tano zilizopita, wakifunga mabao tisa na kuruhusu mawili.

Simba iliifunga Geita Gold 2-0, Coastal Union 1-0, Singida Black Stars 2-1, Pamba Jiji 2-1 na Kagera Sugar 2-0. Hii inaonyesha picha mbili tofauti kabla ya mchezo huo wa hatua ya awali Ligi ya Mabingwa Afrika.

Wanderers wanaingia wakiwa na uimara na kujiamini kutokana na kutopoteza, wakati Simba inaingia ikiwa na mfululizo wa ushindi na safu ya ulinzi ambayo imeruhusu mabao mawili katika mechi zake tano zilizopita. Lakini soka la kimataifa lina tabia yake.

PRE 09

SILAHA ZA WANDERERS

Kama Simba itataka kuondoka Lilongwe na matokeo mazuri, haitapaswa kuangalia tu rekodi ya Wanderers, bali pia kutambua wachezaji wanaoweza kubadilisha mchezo ndani ya dakika chache.

Isaac Kaliati ni mmoja wa wachezaji muhimu zaidi katika kikosi hicho. Kiungo huyo mshambuliaji ana uwezo wa kucheza nyuma ya washambuliaji, kuingia kwenye boksi na kutumia mipira iliyokufa.

Kaliati pia ana jicho la bao, jambo linalomfanya awe mchezaji ambaye Simba italazimika kumfuatilia kwa karibu.

Mbele yake kuna Lameck Mithi, mshambuliaji ambaye tayari ameonyesha uwezo wa kumalizia nafasi baada ya kufunga hat-trick dhidi ya Karonga United.

Huyu ni aina ya mshambuliaji ambaye akipewa nafasi anaweza kuifanya Simba iadhibiwe.

Mphatso Kamanga naye ni mchezaji wa kuangaliwa. Uwezo wake wa kucheza kati ya mistari na kuingia eneo la hatari unaweza kuleta matatizo kwa safu ya kiungo ya Simba.

Kisha kuna Gaddie Chirwa, mwenye kasi na uwezo wa kutumia nafasi, pamoja na Clement Nyondo, mshambuliaji mwenye uzoefu anayejua namna ya kutumia nafasi anazopata.

Wanderers pia wana Sama Thierry Tanjong, raia wa Cameroon ambaye ana nguvu na uwezo wa kushambulia nafasi.

Hii maana yake ni kwamba Simba haitakabili safu ya mbele yenye mchezaji mmoja pekee wa kuogopwa. Kuna watu kadhaa wanaoweza kuleta madhara.

PRE 06

WANAWEZA KUSHAMBULIA KUPITIA PEMBENI

Kwenye upande wa kulia, Stanley Sanudi ni mchezaji wa kuangaliwa.

Beki huyo ana uzoefu, anapanda kusaidia mashambulizi na ana uwezo wa kutoa mipira ya mwisho.

Katika mchezo wao dhidi ya Bullets, baadhi ya mashambulizi hatari ya Wanderers yalitokana na ushirikiano wa Sanudi na Kaliati.

Hivyo, Simba italazimika kuwa makini si tu inapopoteza mpira katikati, bali pia inaposhindwa kudhibiti maeneo ya pembeni.

PRE 04

KATI KUNA VITA

Blessings Singini na Felix Zulu wanaweza kuwa sehemu muhimu ya mpango wa Wanderers katika kuzuia Simba isitawale mchezo.

Singini ana uwezo wa kuongeza nguvu katikati na pia kuingia kwenye eneo la ushambuliaji, wakati Zulu anaweza kusaidia kuvunja mashambulizi na kuanzisha mipango mipya ya timu yake.

Kwa Simba, vita hii ya katikati inaweza kuwa moja ya maeneo muhimu zaidi.

Ikiwa viungo wake Ibraheem Jabaar na Yusuph Kagoma wataruhusu Wanderers kupata muda wa kucheza na kugeuza mpira haraka, wachezaji kama Kaliati na Kamanga wanaweza kupata nafasi ya kuingia kwenye maeneo hatari.


ULINZI

Wanderers pia wana Emmanuel Nyirenda, beki na nahodha ambaye si mlinzi wa kawaida.

Nyirenda ameshaonyesha uwezo wa kwenda mbele na kufunga, kama alivyofanya katika ushindi wa 2-0 dhidi ya Kamuzu Barracks alipofunga dakika ya 90+2.

Hilo linaonyesha kuwa Simba haitakiwi kumchukulia beki huyo kama mchezaji wa kubaki nyuma pekee.

Langoni yupo Chancy Mtete, kipa ambaye amewahi kuonyesha uwezo wa kuiongoza Wanderers kupata matokeo muhimu, ikiwemo ushindi wa 1-0 dhidi ya FCB Nyasa Big Bullets kwenye Ngao ya Jamii. Pia amekuwa akipokezana na Dalitso Khungwa.


KAULI YA KOCHA

Mchezo huu pia unakuja wakati ambao Wanderers wanapitia mabadiliko kwenye benchi la ufundi.

MacDonald Nginde Mtetemera amechukua nafasi ya muda baada ya Bob Mpinganjira kusimamishwa kufuatia kipigo cha kushangaza cha 2-1 dhidi ya Ekhaya FC katika fainali ya Airtel Top 8.

Akizungumzia mchezo huo, Kocha wa muda wa Mighty Wanderers, MacDonald Nginde Mtetemera, amesema yuko tayari kuiongoza timu hiyo katika mchezo muhimu wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Simba SC.

“Nataka kuomba familia ya Wanderers ibaki pamoja. Hakuna kitakachotuzuia ikiwa tutakuwa na umoja,” amesema Mtetemera.

Kocha huyo wa muda ameonyesha pia matumaini kwamba Wanderers wanaweza kufanya vizuri dhidi ya Simba na kusonga mbele katika mashindano hayo, licha ya kutambua ukubwa wa changamoto iliyopo mbele yao.

“Kwenye karatasi ni mchezo mgumu, lakini uwanjani mambo yanaweza kuwa tofauti. Tutafanya kila kitu kuhakikisha tunasonga mbele,” amesema.

Mtetemera anaingia kwenye mchezo huo akiwa na jukumu kubwa la kuiunganisha timu baada ya mabadiliko yaliyotokea kwenye benchi la ufundi.

Wanderers pia wamewaomba mashabiki wao kumpa ushirikiano kocha huyo wa muda katika kipindi hiki.

Katika taarifa iliyotolewa Jumanne, klabu hiyo iliwataka mashabiki kusimama pamoja na Mtetemera na kumpa sapoti katika kipindi hiki cha mpito.

“Tunawaomba kwa heshima wote kusimama pamoja na kumuunga mkono kocha wetu mpya aliyeteuliwa na kumpa sapoti kamili katika kipindi hiki,” ilisema taarifa ya klabu.

Mtetemera anaamini kuwa licha ya Simba kuwa mpinzani mwenye uzoefu mkubwa katika mashindano ya CAF, Wanderers wana nafasi ya kuandika matokeo tofauti ndani ya dakika 90.

PRE 01

SIMBA INA KITU CHA ZIADA

Simba yenyewe haipaswi kuingia uwanjani ikiwa imebebwa na takwimu pekee. Ushindi wa mechi tano mfululizo na kuruhusu mabao mawili katika michezo hiyo ni ishara ya timu iliyo katika hali nzuri, lakini Ligi ya Mabingwa Afrika inahitaji kiwango kingine cha umakini.

PRE 05

Wanderers wana faida ya kucheza nyumbani, mashabiki wao watakuwa nyuma yao na wanataka kuthibitisha kwamba mabadiliko ya benchi la ufundi hayajavuruga malengo yao.

Simba ina faida ya uzoefu wa mashindano ya Afrika na mwenendo mzuri wa hivi karibuni, huku nyota wake kama Libasse Gueye, Clatous Chama, Anicet Oura na Elie Mpanzu wakiongoza vizuri eneo la ushambuliaji.

Kule nyuma kwenye ulinzi, Rushine De Reuck anaongoza vizuri safu hiyo akishirikiana na Ismael Toure pale kati, golini akiwepo Mahamadou Kassali.

Kocha Mkuu wa Simba, Steve Barker, amesema: “Ni mechi muhimu kwetu kwa sababu tunahitaji kuendeleza mwenendo mzuri, haitokuwa rahisi kutokana na aina ya mpinzani tunayecheza naye, ni timu yenye muunganiko mzuri wa kiuchezaji, hivyo ni lazima tuchukue tahadhari.”

PRE 03

Msauzi huyo aliongeza kwamba: “Mechi zetu tano za Ligi Kuu Bara tulizocheza zimetuongezea motisha ya kupambana, malengo yetu ni kuhakikisha mechi hii ya ugenini tunafanya vizuri kwa maana ya kupata ushindi mzuri, utakaoondoa presha tutakapocheza hapa nyumbani.

“Tunafahamu hakuna mchezo rahisi, lakini tumeshawasoma wapinzani wetu na tunafahamu vitu vingi kuhusu wao, mambo yanaweza kubadilika lakini ukweli ni kwamba tunakwenda kutafuta ushindi na siyo sare.”

Mara ya mwisho Simba kucheza kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Bingu, iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Nyasa Big Bullets ya Malawi, Septemba 10, 2022, yaliyofungwa na nyota Mzambia Moses Phiri dakika ya 30 na John Bocco dakika ya 84.

Mechi hiyo ilikuwa ya hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ambapo msimu huo wa 2022-2023, Simba ilishinda nyumbani mabao 2-0, Septemba 18, 2022, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam na kufuzu kwa jumla ya mabao 4-0.

PRE 02

Msimu wa 2025-2026, Simba iliishia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa mkiani mwa kundi D na pointi tano, huku msimu huu ikiwa na malengo ya kucheza nusu fainali ya michuano hiyo.

Mafanikio makubwa kwa Simba katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ni kuishia hatua ya robo fainali, ikianzia mwaka 1994, kisha ikaendeleza rekodi hiyo bora msimu wa 2018-2019, 2020-2021, 2022-2023 na 2023-2024.

Endapo Simba itafika nusu fainali msimu huu, itakuwa imeifikia rekodi yake ya mwaka 1974, ambapo kwa wakati huo michuano hiyo iliitwa Klabu Bingwa Afrika ambayo kwa sasa ni Ligi ya Mabingwa Afrika.