Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ulivyo ushindani wa Alikiba, Mondi katika sura ya kimataifa

Muktasari:

  • Wawili hao ambao walishirikiana katika wimbo wa Kigoma Allstars, Nyumbani (2010), muziki wao umebeba picha ya mabadiliko mapya na ya kisasa katika Bongo Fleva. Hata hivyo, kuna kipindi ushindani wao ulionekana kutoka nje ya malengo ya kisanaa kutokana na kurushiana maneno katika mitandao ya kijamii, maneno ambayo mashabiki huyabeba na kuyaendeleza.

KWA miaka mingi ushindani wa Diamond Platnumz na Alikiba amekuwa akizungumzwa katika Bongo Fleva kutokana na nguvu kubwa ya ushawishi walionayo katika kundi kubwa la mashabiki.

Wawili hao ambao walishirikiana katika wimbo wa Kigoma Allstars, Nyumbani (2010), muziki wao umebeba picha ya mabadiliko mapya na ya kisasa katika Bongo Fleva. Hata hivyo, kuna kipindi ushindani wao ulionekana kutoka nje ya malengo ya kisanaa kutokana na kurushiana maneno katika mitandao ya kijamii, maneno ambayo mashabiki huyabeba na kuyaendeleza.

Kwa soko la ndani ni kama Alikiba na Diamond wameshamaliza kuonyesha kile ambacho wanaweza na tunaweza kusema hakuna anayewadai. Je, huku kimataifa ushindani wao upo katika mizani ipi?.

Ili kupata picha ya hilo, tunaenda kuangazia mambo matatu - tuzo kubwa za kimataifa walizoshinda, wasanii walioshirikiana nao, na kampuni au lebo kubwa ambazo wamefanya nazo kazi.


1. TUZO

Tangu Alikiba na Diamond wameanza muziki, tuzo za muziki zenye hadhi ya juu zaidi kimataifa kwa upande wao ambazo wamewahi kushinda ni MTV Europe Music Awards (EMAs) ambazo zilianza kutolewa Novemba 1994.

Hadi sasa Diamond amewania tuzo hizo mara tano akiwa ndiye pekee wa Bongofleva mwenye rekodi hiyo. Ameshinda tuzo tatu kwa ujumla, msimu wa 2015 alishinda mbili, na 2023 akibeba moja.

Yeye Alikiba ameshinda mara moja, katika msimu wa 2016 alitakata kipengele cha Msanii Bora Afrika mbele ya Wizkid, Olamide (Nigeria), Cassper Nyovest na Black Coffee (Afrika Kusini).

Tuzo za MTV EMAs hufanyika kila mwaka katika nchi tofauti barani Ulaya, na huandaliwa na kampuni ya Paramount International Networks kwa lengo la kutambua mchango wa wasanii na muziki katika utamaduni.

MTV EMAs zilikuja baada ya MTV Video Music Awards (VMAs) ambazo hutolewa Marekani ila hizi hutunza video za muziki pekee, hivyo lengo lingine la MTV EMAs lilikuwa kuwafikia wasanii wengi nje ya MTV VMAs.


2. KOLABO

Nyota ya Alikiba kimataifa upande wa kolabo ilianza kuangaza kabla ya Diamond baada ya kushirikiana na mwimbaji wa RnB kutokea Marekani, R Kelly ambaye kwa wakati huo anatumikia kifungo gerezani.

Alikiba ndiye msanii pekee wa Bongofleva aliyechaguliwa kushikiri katika mradi wa One8 uliotoa wimbo, Hands Across The World (2010), ulioandikwa na kutayarishwa na R. Kelly huku ukishirikisha wasanii wengi wakubwa.

Mbali na Alikiba, pia alikuwepo Amani (Kenya), Navio (Uganda), 2Face (Nigeria) 4x4 (Ghana), Fally Ipupa (DR Congo), JK (Msumbiji)  na Movaizhaleine (Gabon).

Na kwa Afrika kupitia nyimbo zake binafsi, Alikiba amefanya kazi na Mayorkun, Rudeboy (wa P Square), Patoranking, Maud Elka, Blaq Diamond na kadhalika.

Upande wake Diamond, pengine ndiye msanii namba moja Bongo kwa kufanya kolabo nyingi na wasanii wengi wakubwa wa kimataifa kuanzia Amerika hadi Afrika.

Staa huyo wa WCB Wasafi, amewashirikisha mastaa wa Marekani kama Ne-Yo (Marry You), Rick Ross (Waka), Omarion (African Beauty), Jason Derulo (Komasava), huku yeye akishirikishwa na Alicia Keys (Wasted Energy) na Ciara (Low).

Kwa Afrika Diamond amefanya kazi mastaa kama P Square, Davido, Mr. Flavour, Burna Boy, Koffi Olomide, Yemi Alade, Blaq Diamond, Fally Ipupa, Tiwa Savage, Jah Prayzah na Angelique Kidjo, mshindi wa Grammy mara tano.


3. LEBO

Kwa nyakati tofauti Diamond na Alikiba wamepata nafasi ya kufanya kazi na lebo kubwa za muziki duniani zikisimamia hasa biashara ya muziki wao katika soko la kimataifa.

Alikiba ndiye wa kwanza kupata fursa hiyo baada ya kusainiwa na Sony Music Entertainment Africa, mkataba ambao umeshamalika lakini chini ya lebo hiyo alitamba na nyimbo zake kali ikiwemo Aje (2016) na Seduce Me (2017).

Aliwahi kuandika rekodi kama msanii wa kwanza aliyesainiwa Sony Music kwa video ya wimbo wake (Aje) kutazamwa (views) zaidi ya milioni 5 katika mtandao wa YouTube, kitu kilichopelekea lebo hiyo kumpatia tuzo (plaque).

Upande wake Diamond, alianza kufanya kazi na Universal Music Group (UMG), kisha Warner Music Group ambao hadi sasa anaendelea kufanya nao kazi, kwa mkataba ambao Diamond aliutaja kuwa wa fedha nyingi.

Universal Music ndio waliosimamia albamu ya tatu ya Diamond, A Boy From Tandale (2018) yenye nyimbo 18, huku Warner Music wakisimamia Extended Playlist (EP) ya kwanza ya mwanamuziki huyo, First of All (2022) yenye nyimbo 10.