Sikia hii ya Amorim Man United
Muktasari:
- Kocha Amorim alikuwa wa kwanza kushuka kwenye basi wakati timu ilipowasili hotelini Waldorf Astoria na kuonyesha kwamba amesimama mbele kuongoza.
CHICAGO, MAREKANI: KOCHA wa Manchester United, Ruben Amorim ameongoza msafara akishuka wa kwanza kutoka kwenye basi la timu wakati walipofika kwenye hoteli moja huko Chicago, Marekani ambako wataweka kambi kwa ajili ya pre-season.
Kocha Amorim alikuwa wa kwanza kushuka kwenye basi wakati timu ilipowasili hotelini Waldorf Astoria na kuonyesha kwamba amesimama mbele kuongoza.
Lakini, kwenye kuongoza ndani ya uwanja mambo bado si mambo kwa kocha Amorim, ambaye kwa sasa yupo kwenye msako wa kutafuta huduma ya straika mpya wa kuja kufunga mabao kwenye kikosi hicho.
Miamba hiyo ya Old Trafford ilifunga mabao 44 tu kwenye Ligi Kuu England msimu uliopita, ambapo Man United ilimaliza nafasi ya 15, ikiwa ya chini zaidi kuwahi kushika katika kipindi cha miaka 51, hivyo itahitaji straika mpya kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi.
Lakini, ni siku 22 au zaidi zimebaki kabla ya msimu mpya kuanza, ambapo Man United itakuwa nyumbani Old Trafford kukipiga na Arsenal katika mchezo wao wa kwanza wa Ligi Kuu England na bado haijapata Namba 9 wa kuongoza safu yao ya ushambuliaji. Ilimsaka straika Liam Delap, ambaye amejiunga na Chelsea akitokea Ipswich, wakati Viktor Gyokeres wa Sporting Lisbon anakaribia kujiunga na Arsenal na mkali wa Eintracht Frankfurt, Hugo Ekitike ameshatua zake Liverpool.
Mastaa wake wapya aliowanasa dirisha hili Matheus Cunha na Bryan Mbeumo wamefunga mabao 15 na 20 mtawalia kwenye Ligi Kuu England msimu uliopita, kuliko mabao ya washambuliaji wawili wa Man United Rasmus Hojlund na Joshua Zirkzee. Lakini, kwa namba zuri za mabao ya Cunha na Mbeumo haina maana kwamba timu hiyo haihitaji huduma ya straika mwenye uwezo wa kufunga mabao yanayoanzia 20 na kuendelea kwa msimu.
Straika wa mwisho wa Man United kufunga mabao 20 au zaidi kwenye Ligi Kuu England ni Robin van Persie, ambaye ndiye aliongoza timu hiyo kushinda taji la mwisho la ligi ilipokuwa chini ya Sir Alex Ferguson msimu wa 2012-13.
Ishu ya kufunga mabao iliendelea kuwa tatizo Man United kwenye mechi yao ya kirafiki dhidi ya Leeds United iliyofanyika Stockholm, Sweden, Jumamosi iliyopita ambapo timu hizo zilitoka sare ya bila kufungana.
Na sasa Man United imerudi kwenye mpango wao wa kunasa saini ya straika wa Paris Saint-Germain, Randal Kolo Muani, aliyekuwa kwenye rada yao miaka miwili iliyopita kabla ya kulipa Pauni 72 milioni kumnasa Hojlund. Dili la kubadilishana na winga Alejandro Garnacho, linaweza kuhusika kwenye mpango huo, huku ikimsaka pia straika wa Chelsea, Nicolas Jackson na wa RB Leipzig, Benjamin Sesko.