Sikia hii! Darwin Nunez sasa anaitaka Napoli

Muktasari:
- Nunez ni miongoni mwa mastaa ambao wameripotiwa kupewa ruhusa ya kuondoka na Liverpool endapo wa watapata timu zitakazokuwa tayari kulipa ada ya uhamisho inayohitajika na majogoo hao.
STRAIKA wa Liverpool na timu ya taifa ya Uruguay, Darwin Nunez, mwenye umri wa miaka 25, ameitaja Napoli kuwa ndio timu anayopendelea kujiunga nayo ikiwa ataondoka Anfield katika dirisha hili la majira haya ya kiangazi.
Nunez ni miongoni mwa mastaa ambao wameripotiwa kupewa ruhusa ya kuondoka na Liverpool endapo wa watapata timu zitakazokuwa tayari kulipa ada ya uhamisho inayohitajika na majogoo hao.
Liverpool tayari imeshaanza kutafuta hadi mbadala wake ikihusishwa na majina ya washambuliaji mbalimbali akiwamo Bryan Mbeumo wa Brentford.
Nunez ambaye mkataba wake unamalizika 2028, msimu uliopita alicheza mechi 47 za michuano yote, akafunga mabao 7 na asisti saba.
Anthony Elanga
NOTTINGHAM Forest imekataa ofa ya karibu pauni 45 milioni kutoka kwa Newcastle inayohitaji huduma ya winga raia wa Sweden mwenye umri wa miaka 23, Anthony Elanga.
Inaelezwa vigogo wa Nottingham wamekataa ofa hiyo kwa sababu haitoshi na wamesisitiza kuwa wanahitaji pauni 60 milioni au zaidi ili kumuuza Elanga.
Alexander Isak
NEWCASTLE iko tayari kumfanya mshambuliaji wao wa kimataifa wa Sweden, Alexander Isak, 25, kuwa mchezaji anayelipwa mshahara mkubwa zaidi katika historia ya timu hiyo ili kumzuia asiondoke katika dirisha hili ambapo anawindwa na Liverpool, Barcelona, na Arsenal.
Isak ni mmoja kati ya mastraika wanaowindwa na timu mbalimbali barani Ulaya hususani katika dirisha hili kutoka na moto anaowasha.
Jadon Sancho
KOCHA wa Fenerbahce, Jose Mourinho amependekeza jina la winga wa Manchester United na timu ya taifa ya England mwenye umri wa miaka 25, Jadon Sancho, akisisitiza kuwa anahitaji asajiliwe katika dirisha hili ili kuboresha safu yake ya ushambuliaji.
Ripoti zinadai Man United iko tayari kumuuza staa huyu kwa pauni 25 milioni. Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2026.
Marcus Rashford
BARCELONA ina mpango wa kuwasilisha maombi ya kutaka kumsajili mshambuliaji wa Manchester United na timu ya taifa ya England mwenye umri wa miaka 27, Marcus Rashford katika dirisha hili kwa mkopo wa msimu mmoja.
Man United inadaiwa kuwa ipo tayari kumuuza Rashfrod lakini kiasi cha pesa inachohitaji kinaonekana kuwa kikubwa zaidi ya kile ambacho Barca iko tayari kukitoa.
Wilfred Ndidi
EVERTON na Manchester United zimeingia katika vita kali ya kuiwania saini ya kiungo wa Leicester City na timu ya taifa ya Nigeria, Wilfred Ndidi, 28, katika dirisha hili.
Kuna uwezekano mkubwa staa huyu akaondoka kwa sababu katika mkataba wake kuna kipengele kinachomruhusu kuondoka kwa pauni 9 milioni baada ya Leicester kushuka daraja.
Jordan Henderson
NOTTINGHAM Forest na Marseille zinahitaji huduma ya kiungo wa Ajax na England mwenye umri wa miaka 35, Jordan Henderson, ambaye ana kipengele cha kuondoka bure kwenye mkataba wake.
Henderson anadaiwa kutaka kurejea England au kutafuta changamoto mpya sehemu nyingine. Mkataba wake na Ajax unatarajiwa kumalizika mwaka 2026.
Yoane Wissa
BRENTFORD inahitaji kiasi kisichopungua pauni 50 milioni kutoka kwa timu yoyote itakayohitaji saini ya mshambuliaji wake raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Yoane Wissa, katika dirisha hili.
Staa huyu anawindwa na timu kibao ndani na nje ya bara la Ulaya ikiwa pamoja na Nottingham Forest, Tottenham, Arsenal, Fenerbahce na Galatasaray.