Shughuli imekamilishwa huko! Amorim atimuliwa
Muktasari:
- Kocha huyo Mreno alitoa mashambulizi makali kwa mabosi wa Old Trafford baada ya sare ya 1-1 dhidi ya Leeds United, Jumapili.
MANCHESTER, ENGLAND: MANCHESTER United imemfuta kazi Ruben Amorim baada ya kauli yake ya kuwakosoa mabosi.
Kocha huyo Mreno alitoa mashambulizi makali kwa mabosi wa Old Trafford baada ya sare ya 1-1 dhidi ya Leeds United, Jumapili.
Amorim, 40, anaondoka kwenye klabu hiyo baada ya miezi 14 huku timu ikiwa na mapito mengi ya ndani na nje ya uwanja. Ameshinda mechi 24 kati ya 63 alizoinoa Man United, huku akiwa na wastani wa ushindi wa asilimia 38.71 tu. Hakuna kocha mwingine wa Man United aliyekuwa na rekodi mbovu ya rekodi ya ushindi tangu Frank O’Farrell, aliyefutwa kazi 1971. Alishinda mechi 30 kati ya 81 na kuwa na wastani wa ushindi wa asilimia 37.04.
Ripoti zinadai kwamba Amorim alitakiwa kuondoka haraka, huku kiungo wa zamani wa miamba hiyo, Darren Fletcher akikabidhiwa timu kama kocha wa kipindi cha mpito.
Amorim aliweka rehani kibarua chake huko baada ya kuamua kuwakosoa mabosi wa klabu hiyo hadharani. Kocha huyo Mreno ameripotiwa amejiweka kwenye kitanzi juu ya usalama wa kazi yake huko Old Trafford kutokana na kutoa maneno ya mashambulizi kwa bodi ya timu hiyo.
Amorim, 40, alilalamikia ishu ya "kocha mkuu" baada ya kutambulika kama "meneja". Na Amorim alirusha kijembe hicho kumlenga mkurugenzi wa soka wa klabu hiyo, Jason Wilcox baada ya kukwama kwa uhamisho wa winga wa Bournemouth, Antoine Semenyo.
Amorim aliahidi kwamba hawezi kung'atuka, lakini anataka kupewa nguvu kwenye klabu hiyo hasa katika kipindi hiki cha usajili.
Amesema: “Nipo hapa kama meneja wa Manchester United, sio kama kocha mkuu wa Manchester United. Na hilo lipo wazi. Nafahamu jina langu si Tuchel, wala si Conte, na pia si Mourinho, lakini ni meneja wa Manchester United. Sitang'atuka. Nitaendelea kufanya kazi yangu hadi hawa jamaa watakapokuja hapa na kunibadili.
“Ninachotaka kusema nakwenda kuwa meneja wa timu hiyo, sio kocha tu. Na nipo wazi kwenye hilo. Na hilo litakwenda kumalizika katika kipindi cha miezi 18 na baada ya hapo kila mtu ataendelea na mambo yake. Hayo ndio makubaliano.
“Hiyo ni kazoi yangu, sio kuwa kocha. Kama watu hawawezi kukabiliana na Gary Nevilles na ukosoaji wake, tunahitaji kubadili hii klabu. Nilichotaka kuwaambia, nimekuja hapa kuwa meneja wa Manchester United, sio kuja kuwa kocha.”
Man United ilikuwa kwenye maandalizi ya kumsajili Semenyo kabla ya Manchester City kuibuka na kuwa mstari wa mbele kwa sasa. Lakini, haipo wazi kama Amorim alimhitaji zaidi Semenyo au kuna maeneo mengine kwenye kikosi ambayo atahitaji kuyaboresha.
Man United mpango wake ni kufanya maboresho kwenye eneo ya kiungo ya kati, lakini jambo hilo litafanyika kwenye dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Wachezaji wanane wa kikosi cha kwanza cha timu hiyo walikosa mechi mbili za mwisho, huku Man United ikishinda mechi tatu tu kati ya 11 zilizopita.
Licha ya kupata matokeo mabovu, Man United imepanda na kushika nafasi ya tano kwenye msimamo wa Ligi Kuu England baada ya kutokea nyuma na kupata sare dhidi ya Leeds. Na Amorim amebainisha mambo ya nyuma ya pazia kabla ya kuwabwatukia mabosi wake waamua kumpa sapoti au kumfuta kazi baada ya mechi hiyo ya Elland Road.
Man United mara chache sana imefanya usajili wa dirisha la majira ya baridi tangu ilipomnasa kiungo Bruno Fernandes, Januari 2020. Wachezaji wengine waliosajiliwa kwenye dirisha la Januari mwaka jana ni Patrick Dorgu na Ayden Heaven, ambao Amorim aliwathibitisha.
Wilcox alifanya kazi chini ya mkurugenzi mtendaji mkuu wa Man United, Omar Berrada huko Man City kabla ya wawili hao kutua Old Trafford, 2024.
Mkurugenzi wa usajili wa Man United, Christopher Vivell, naye pia alihusishwa kwenye maneno hayo ya Amorim. Na hilo linakuja baada ya Vivell kudaiwa kutofurahishwa na sare ya bao 1-1 iliyopata Man United dhidi ya Fulham, Agosti mwaka jana.
Baada ya mechi hiyo, kocha wa Fulham, Marco Silva na kiungo Alex Iwobi walielezea jinsi walivyoweza kuufanyia kazi mfumo wa Amorim wa 3-4-2-1. Mabosi hao, Wilcox na Berrada pamoja na mmiliki mwenza, Sir Jim Ratcliffe walipokuwapo uwanjani Molineux, wakati Man United ilipoichapa Wolves 4-1, Desemba 8, lakini walikuwa kwenye mjadala mkubwa baada ya Wolves kupata bao. Man United iliwapoteza Amad, Bryan Mbeumo na Noussair Mazraoui waliokwenda kwenye Afcon 2025 baada ya sare ya 4-4 dhidi ya Bournemouth na nahodha Fernandes aliumia kwenye mechi dhidi ya Aston Villa huko Villa Park.
Tangu alipotua Man United, Amorim amefanya usajili wa mastaa Heaven, Dorgu, Diego Leon, Matheus Cunha, Bryan Mbeumo, Benjamin Sesko na Senne Lammens.
REKODI ZAAMORIM MAN UNITED
Mechi: 63
Ushindi: 24
Sare: 18
Vichapo: 21
Wastani wa ushindi: 38.10%