Amorim anawawaza tu Mbeumo, Amad
Muktasari:
- Man United haitakuwa na huduma ya mastaa hao kwa siku kadhaa mbele kutokana na timu zao zote kutinga hatua ya 16 bora, ambapo Mbeumo yupo na Cameroon, Amad na Ivory Coast, wakati Mazrauoi yupo kwenye kikosi cha wenyeji wa Afcon 2025, Morocco.
RABAT, MOROCCO: MANCHESTER United kijasho kinawatoka kwa sababu ya kuwasubiri Bryan Mbeumo, Amad na Noussair Mazraoui, ambao wote wako kwenye majukumu ya kimataifa wakicheza Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) linaloendelea huko Morocco.
Man United haitakuwa na huduma ya mastaa hao kwa siku kadhaa mbele kutokana na timu zao zote kutinga hatua ya 16 bora, ambapo Mbeumo yupo na Cameroon, Amad na Ivory Coast, wakati Mazrauoi yupo kwenye kikosi cha wenyeji wa Afcon 2025, Morocco.
Kitu pekee kinachomfariji kocha Ruben Amorim ni kuona wachezaji wake hao wapo kwenye usimamizi mzuri wa afya zao huko kwenye majukumu ya timu za taifa.
Man United imeathirika pakubwa katika mechi za hivi karibuni, ambapo Mbeumo, Amad na Mazraoui wakiwa AFCON, huku inawakosa pia Bruno Fernandes, Harry Maguire, Matthijs de Ligt na Mason Mount kutokana na kuwa majeruhi.
Kukosekana kwa wachezaji kama Amad na Mbeumo kunamfanya kocha Amorim kubadili mfumo wa kuichezaji na kutumia fomesheni ya 4-2-3-1 kwa mara ya kwanza tangu alipoanza kuinoa timu hiyo miezi 13 iliyopita wakati wa mchezo wa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Newcastle United kwenye Boxing Day.
Hata hivyo, sare ya 1-1 dhidi ya Wolves, ambao wako mkiani mwa Ligi Kuu England, imemfanya Amorim kuwakumbuka mastaa wake hao wanaokipiga huko Afcon 2025.
Kwa hiyo, hakufurahishwa kuona Morocco, Cameroon na Ivory Coast zote zikivuka hatua ya makundi AFCON. Mazraoui, Mbeumo na Amad sasa wanajiandaa na mechi za hatua ya mtoano huko Morocco, huku Man United ikiwa na kasheshe la kucheza na Leeds United, Jumapili.
Mbeumo ataikabili Afrika Kusini kwenye hatua ya 16 bora, wakati Amad atacheza dhidi ya Burkina Faso na Mazraoui atakabiliana na Tanzania, Jumapili.