Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sheria za Arteta huko Arsenal usipime

Muktasari:

  • Moja kati ya sheria zake zinadaiwa kuwanufaisha sana madereva taksi wa eneo la Kaskazini mwa Jiji la London ambako timu hiyo ndiyo maskani yake.

LONDON, ENGLAND: KOCHA wa Arsenal, Mikel Arteta ameweka sheria kali ambazo anaamini zitaisaidia timu hiyo kushinda taji la Ligi Kuu England baada ya kuangukia pua dakika za mwisho kwa zaidi ya misimu mitatu.

Moja kati ya sheria zake zinadaiwa kuwanufaisha sana madereva taksi wa eneo la Kaskazini mwa Jiji la London ambako timu hiyo ndiyo maskani yake.

Arteta ameweka sheria madhubuti inayowataka wachezaji kukutana kwenye uwanja wa mazoezi kabla ya mechi yoyote,  iwe ya nyumbani au ugenini, sheria ambayo imekusudiwa kuimarisha mshikamano wa timu.

Kwa mujibu wa SunSport, Arteta ni mkali katika mambo madogo madogo na anaamini ili kukamilisha msimu huu kwa ubingwa wa EPL, kila mchezaji lazima awe sawa kimawazo na mwenendo na wenzake.

Mhispaniola huyo huzingatia kila kitu, ikiwemo lugha ya mwili na jinsi wachezaji wanavyoshirikiana kabla ya mechi.

Tofauti na klabu nyingine za London kama Chelsea, Crystal Palace na Tottenham, ambazo wachezaji huruhusiwa kuendesha magari yao moja kwa moja hadi uwanjani saa mbili au tatu kabla ya mechi, Arteta anataka kila mchezaji lazima aende kwanza kwenye uwanja wa mazoezi London Colney, kisha wasafirishwe kwa pamoja kwa basi hadi uwanjani.

Hali hii imesababisha wachezaji wengi kuamua kukodi madereva wa teksi waendeshe magari yao kwa siku nzima.

Madereva hao huwachukua kutoka nyumbani mwao hadi kwenye kituo cha mazoezi, kisha hurudi kuchukua familia zao kuzipeleka Uwanjani na baada ya mchezo huwapeleka tena nyumbani.

Wanaposafiri kwa mechi za ugenini, wachezaji hawaruhusiwi kuchukuliwa na wake au familia pale wanapowasili uwanja wa ndege, wote wanalazimika kurudi kwenye kituo cha mazoezi kwa basi kabla ya kuchukuliwa tena na madereva wa teksi kurudi nyumbani.

Mmoja wa madereva aliiambia tovuti ya The Sun: "Kwa kweli kwetu sisi tunafurahia kila mechi na tunatarajia tupate simu kutoka kwa wachezaji, kwa sababu wakikupigia kukupa kazi hiyo kimsingi huwa ni zaidi ya nusu ya mapato yetu ya wiki na ni kazi tulivu haina purukushani. Pia nani asiyetaka kuwa sehemu ya mpira wa miguu siku hizi hata kama ni kwa kuendesha magari yao."

Kwa kila mechi ya nyumbani inaelezwa wachezaji wa Arsenal hutumia takribani Pauni 1,000 na msimu mzima hufikia Pauni 20,000 kwa huduma hiyo.

Hapo awali, Arteta aliwahi kulegeza baadhi ya kanuni, jambo lililosababisha aliyekuwa nahodha, Pierre-Emerick Aubameyang, kuchelewa kufika katika moja ya mechi.