Shakira amsifia Messi, Antonela
Muktasari:
- Messi mwenye, 39 aliiongoza Argentina kwa kutoa pasi mbili za mabao katika ushindi huo wa nusu fainali, akiendelea kuthibitisha bado ni tegemeo kubwa la timu hiyo licha ya umri wake.
MIAMI, MAREKANI: MWANAMUZIKI maarufu duniani, Shakira amempongeza nahodha wa Argentina, Lionel Messi kutokana na kiwango bora alichoonyesha katika ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya England uliowapeleka mabingwa watetezi hao fainali ya Kombe la Dunia 2026.
Messi mwenye, 39 aliiongoza Argentina kwa kutoa pasi mbili za mabao katika ushindi huo wa nusu fainali, akiendelea kuthibitisha bado ni tegemeo kubwa la timu hiyo licha ya umri wake.
Katika kurasa zake za mitandao ya kijamii, Shakira amesema anavutiwa na uwezo wa Messi kuendelea kucheza katika kiwango cha juu na kusisitiza mafanikio yake yanatokana na nidhamu, kujituma na kutokubali kukata tamaa.
“Anachokifanya Leo Messi ni zaidi ya kitu cha ajabu. Anaonyesha maadili ya mtu mwenye kujituma na nidhamu ambaye anashinda changamoto zote pamoja na umri. Ameonyesha thamani ya mtu haipimwi kwa umri wala maneno ya watu,” aliandika Shakira.
Mwimbaji huyo wa Colombia hakusita pia kumpongeza mke wa Messi, Antonela Roccuzzo, akisema amekuwa nguzo muhimu katika maisha ya nahodha huyo wa Argentina.
“Ninaamini kuwa na mwanamke kama Antonela pembeni yake kunampa nguvu na hamasa ya kuendelea kuthibitisha ubora wake,” aliongeza.
Antonela hakukawia kujibu salamu hizo, akizichapisha tena kwenye ukurasa wake wa Instagram kama ishara ya shukrani kwa maneno ya Shakira.
Messi, ambaye tangu mwaka 2023 amekuwa akiichezea Inter Miami Marekani, sasa anajiandaa kucheza fainali ya pili mfululizo ya Kombe la Dunia huku Argentina ikitarajia kukutana na Hispania katika pambano la kusaka ubingwa.
Iwapo Argentina itafanikiwa kutetea taji hilo, Messi ataandika historia ya kutwaa Kombe la Dunia mara mbili mfululizo na kuhitimisha safari yake ya kimataifa kwa mafanikio makubwa zaidi katika soka la dunia.