Sesko kaikataa Man United kisa Newcastle United
Muktasari:
- Sesko ambaye hivi karibuni amekuwa akitajwa sana kwamba anaweza kutua Manchester United anauzwa kwa jumla ya Pauni 70 milioni.
NEWCASTLE United imewasilisha ofa ya Pauni 65.5 milioni kwenda RB Leipzig kwa ajili ya kumnunua mshambuliaji wa kimataifa wa Slovenia, Benjamin Sesko mwenye umri wa miaka 2
Sesko ambaye hivi karibuni amekuwa akitajwa sana kwamba anaweza kutua Manchester United anauzwa kwa jumla ya Pauni 70 milioni.
Licha ya uwepo wa timu mbili zinazomhitaji, taarifa zinaeleza kuwa Sesko ameshafanya uamuzi wake kuhusu atakakocheza msimu ujao.
Mshambuliaji huyo wa RB Leipzig amekuwa katikati ya vita kali ya usajili kati ya Manchester United na Newcastle hivi karibuni.
Kwa mujibu wa gazeti la Delo, Sesko ameamua kujiunga na Newcastle, licha ya ofa nono ambayo amewekewa mezani na Man United.
Gazeti hilo la Kislovenia linaripoti kuwa pendekezo la Newcastle ndilo lililoshinda baada ya tetesi za muda mrefu zilizomhusisha Sesko na timu nyingi barani Ulaya ikiwemo Arsenal ambayo ilijiondoa mapema katika dirisha hili la majira ya kiangazi,na kumsajili Viktor Gyokeres badala yake.
Man United ilihamishia nguvu kwa Sesko baada ya kuachana na harakati za kumsajili mshambuliaji wa Aston Villa, Ollie Watkins.
Mashetani hawa wekundu walimtumia mkurugenzi wao wa usajili, Christopher Vivell, ambaye aliwahi kufanya kazi na Sesko akiwa RB Salzburg kama sehemu ya ushawishi ili kumpata lakini bado inaonekana kuwa ngumu..
Kocha Ruben Amorim naye alikuwa amempa kipaumbele Sesko, baada ya kuwapata Matheus Cunha katika safu yake ya ushambuliaji.
Alexander Isak
LIVERPOOL wako tayari kuwasilisha ofa ya pili kwa ajili ya kumsajili mshambuliaji wa Newcastle, Alexander Isak, 25, dirisha hili. Mabosi wa Liverpool wanadaiwa kuwa bado hawajakata tamaa kumpata Isak ambaye ofa yao ya kwanza waliyoiwasilisha ili kumsajili imekataliwa. Isak mwenyewe ameshawasiliana na mabosi wa Newcastle na kuwaeleza juu ya nia yake ya kutaka kuondoka na changamoto kubwa imekuwa ni kiasi cha pesa cha Pauni 150 milioni ambacho timu hiyo inakihitaji.
Christopher Nkunku
BARCELONA imekataa ofa ya Chelsea ya kumjumuisha mshambuliaji wao wa kimataifa wa Ufaransa, Christopher Nkunku mwenye miaka 27, kama sehemu ya dili la kutaka kuipata saini ya kiungo wao wa kimataifa wa Hispania, Fermin Lopez katika dirisha hili. Cheslea ambayo bado inaendelea kujenga timu, ilipendekeza ofa hiyo kuhakikisha inaipuku Man United ambayo pia inahitaji saini ya Lopez. Mabosi wa Barca wapo tayari kumuuza kiungo huyu lakini kiasi kisichopungua Pauni 70 milioni.
Fermin Lopez
MANCHESTER United ipo tayari kuwasilisha ofa ya Pauni 61 milioni kwenda Barcelona ili kuipata huduma ya kiungo wa timu hiyo, Fermin Lopez katika dirisha hili. Lopez mwenye umri wa miaka 22, ni moja ya mastaa waliongia vizuri katika mfumo wa kocha Hans Flick lakini Man United inamatumaini ya kumpata kwa sababu ya hali ya kiuchumi ya Barca. Mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwaka 2029.
Jorrel Hato
BEKI kisiki wa Uholanzi, Jorrel Hato mwenye umri wa miaka 19, amekamilisha vipimo vya afya ikiwa ni katika hatua za mwisho kabla hajajiunga rasmi na Chelsea akitokea Ajax katika dirisha hili kwa uhamisho unaokadiriwa kufikia Pauni 35.5 milioni. Hato ambaye mwaka huu amecheza michuano ya Euro kwa vijana wenye umri wa miaka 21, mkataba wake na Ajax unatarajiwa kumalizika mwaka 2028.
Yann Bissek
CRYSTAL Palace inadaiwa kugonga mwamba katika jaribio lao la kumsajili beki wa Inter Milan na Ujerumani, Yann Bissek mwenye miaka 24, kwa ofa yao ya Pauni 28 milioni waliyoiwasilisha siku chache zilizopita. Bissek ambaye mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwaka 2029, ni mmoja kati ya wachezaji ambao hawakupata nafasi ya kutosha katika kikosi cha kwanza cha Inter kwa msimu uliopita.
Michael Cooper
WEST Ham bado inafanya mazungumzo na Sheffield United kwa ajili ya kuipata huduma ya kipa wa timu hiyo, Michael Cooper, mwenye umri wa miaka 25 katika dirisha hili la majira ya kiangazi. Msimu uliopita akiwa na Sheffield katika mashindano ya Ligi Daraja la Kwanza England, Cooper alichez alicheza mechi 46.
Ademola Lookman
MABOSI wa Atalanta wameendelea kushikilia msimamo wao wa kuhitaji Pauni 43.5 milioni kutoka kwa timu yoyote itakayohitaji nuduma ya mshambuliaji wao, Ademola Lookman, mwenye umri wa miaka 27. Hivi karibuni mabosi wa Atalanta walikataa ofa ya Pauni 36.5 milioni kutoka kwa Inter Milan inayohitaji huduma yao ya staa huyo.
Ademola ambaye ni mmoja kati ya washambuliaji wanaofanya vizuri Italia, mkataba wake na Atalanta unatarajiwa kumalizika mwaka 2027.