Scholes: Kiwango cha Salah kimeporomoka, anacheza kawaida sana
Muktasari:
- Scholes amesema amemfuatilia Salah na kubaini bado anacheza nafasi ile ile, lakini mambo yamekuwa tofauti msimu huu, hivyo hana shaka akisema mshambuliaji huyo ameonyesha kiwango cha chini kabisa.
Gwiji wa Manchester United, Paul Scholes, ametoa maoni yake kuhusu nyota wa Liverpool, Mohamed Salah, akieleza licha ya kuwa mchezaji wa kiwango cha juu, wakati mwingine anacheza kawaida sana.
Katika kipindi cha The Good, The Bad and The Football, Scholes amezungumzia kiwango cha Salah msimu huu wa 2025/26, ambapo mshambuliaji huyo kutoka nchini Misri ameanza kwa kiwango kinachonekana kuwa cha chini, ikilinganishwa na misimu iliyopita. Amefunga mabao matatu na asisti tatu katika mechi 10 za mashindano yote. Katika Ligi Kuu ya England, amefunga mabao mawili na kutoa asisti mbili katika mechi saba.
Scholes amesema amemfuatilia Salah na kubaini bado anacheza nafasi ile ile, lakini mambo yamekuwa tofauti msimu huu, hivyo hana shaka akisema mshambuliaji huyo ameonyesha kiwango cha chini kabisa.
“Bado anacheza katika nafasi ile ile, lakini anaonekana kufanya maamuzi mabaya mara kwa mara. Kama unakumbuka mwaka jana, alifunga mabao mengi, na mara nyingi alikuwa akikata kutoka upande wa kulia kuingia ndani kwa mguu wake wa kushoto na kutoa pasi nzuri kwa wachezaji wengine kufunga kirahisi.
"Lakini Jumamosi (dhidi ya Chelsea) kulikuwa na matukio kadhaa ambapo alikata upande wa ndani na kupiga mpira juu kabisa ya lango. Mwaka jana, mipira hiyo ilikuwa inaenda moja kwa moja kwenye kona ya juu ya goli. Ukimuangalia akija ndani kwa mguu wa kushoto, unajua ataipiga kwenye kona ya juu, lakini sasa hivi, anakosa kabisa anapiga juu kwa futi 20 au 30, na unajiuliza, ‘hana makali kama zamani’. Hicho ndicho ninachofikiri.”
Scholes ameendelea kueleza kuwa, hata Salah akiwa kwenye kiwango kizuri, bado hufanya makosa ya msingi.
“Ni mmoja wa wale wachezaji ambao kila unavyomtazama, hata akiwa mzuri sana, bado anafanya baadhi ya mambo mabaya kabisa uwanjani. Unanielewa? Mpira unaweza kumpiga mguuni au gotini na kutoka nje, atakosa kuudhibiti vizuri... lakini ghafla, anafanya kitu ambacho kinamfanya aonekane kama mchezaji bora duniani kwa wakati huo. Kwa sasa, anashindwa kupata ile sehemu yake bora kabisa.”
Mohamed Salah hajatoa mchango wowote wa bao (kufunga au kusaidia) katika mechi tatu zilizopita akiwa na Liverpool, ambazo zote wamepoteza.