Liverpool yamfariji Mohamed Salah
Muktasari:
- Mchezaji huyo wa kimataifa wa Misri hakuingia hata kwenye nafasi tatu za juu ambazo walichaguliwa Ousmane Dembele, Lamine Yamal na Vitinha.
LIVERPOOL, ENGLAND: TIMU ya Liverpool ilimtumia supastaa wake Mohamed Salah ujumbe wa faraja baada ya kuthibitishwa kuwa mshambuliaji huyo hakushinda tuzo ya Ballon d’Or 2025.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Misri hakuingia hata kwenye nafasi tatu za juu ambazo walichaguliwa Ousmane Dembele, Lamine Yamal na Vitinha.
Salah alimalizia nafasi ya nne licha ya kuhusika katika mabao 57 msimu uliopita katika michuano yote akiisaidia timu yake kushinda ubingwa Ligi Kuu England.
Liverpool iliweka chapisho katika mitandao yake ya kijamii ikiandika: “Msimu wa kufurahia kwa Salah” kisha wakaweka na emoji ya moyo mwekundu.
Baada ya hapo walichapisha picha za kumbukumbu ya matukio na mafanikio ambayo Salah aliyapata msimu uliopita.
Picha ya kwanza ilionyesha Salah akiwa ameketi baada ya mchezo wa mwisho wa msimu, huku akiwa na medali ya Ligi Kuu England na pembeni yake kulikuwa na tuzo ya mchezaji bora wa msimu, tuzo ya mfungaji bora, tuzo ya mchezeshaji bora na tuzo ya mchezaji bora wa mwaka ya FWA.
Picha ya pili ilimuonyesha Salah akiwa na tuzo yake ya mchezaji bora wa msimu ya PFA aliyopokea mwezi uliopita kwenye sherehe zilizofanyika Manchester.
Vilevile zilionyeshwa picha mbalimbali akiwa katika furaha baada ya kushinda taji la Ligi Kuu pamoja na mafanikio mbalimbali zilioendelea kuchapishwa katika kurasa hizo.
Conor Bradley, Hugo Ekitike, Luis Diaz, Milos Kerkez, na Ryan Gravenberch, walioneka kulike na kuweka maoni katika chapisho hilo lililowekwa Instagram.